Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa mara ya kwanza Kenya yapima 'maendeleo ya watoto wadogo'

Mfanyakazi mmoja wa huduma ya afya anarekodi data huku mama mmoja wa Kenya akimshika mtoto wake, ambaye anashikilia thermometer, katika mazingira ya nje akiwa na lori la matibabu nyuma.
© WHO/Genna Print Mama na mtoto wanashiriki katika programu huduma za afya ya kinamama na watoto zinazotolewa na WHO nchini Kenya.

Kwa mara ya kwanza Kenya yapima 'maendeleo ya watoto wadogo'

Afya

Kenya imefanya kwa mara ya kwanza utafiti wa kitaifa unaopima maendeleo ya watoto kuanzia umri wa miezi mitatu, ukiangalia ukuaji wao kimwili, lugha, uwezo wa kufikiri na kushirikiana na wengine.

Utafiti wa Afya na Idadi ya Watu wa Kenya wa mwaka 2025/2026, uliozinduliwa jijini Nairobi Novemba 3, umebaini kuwa asilimia 85 ya watoto wenye umri wa miezi 3 hadi 23 na asilimia 83 ya wenye umri wa miezi 24 hadi 59 wanaendelea vizuri kulingana na hatua zinazotarajiwa za ukuaji wao.

Hata hivyo, utafiti umeonesha tofauti kubwa za maendeleo ya watoto kati ya kaunti mbalimbali nchini humo.

Kwa mfano:

  • Pokot Magharibi  ina asilimia 52 ya watoto wenye umri wa miezi 3 hadi 23 wanaofikia hatua zinazotarajiwa za maendeleo.
  • Kakamega inaongoza kwa asilimia 97 katika kundi hilo la umri.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO, takwimu hizo zitasaidia serikali za kaunti kuelekeza huduma za malezi, lishe na uchocheaji wa maendeleo ya awali ya watoto katika maeneo yenye mahitaji makubwa.

Katika viashiria vingine vya afya, utafiti umeonesha kupungua kwa vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano kutoka 41 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2022 hadi 37 mwaka 2025.

Aidha, asilimia 91 ya wanawake walijifungulia katika vituo vya afya mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 88 mwaka 2022, huku wanawake waliopata angalau mahudhurio manne ya kliniki wakati wa ujauzito wakiongezeka kutoka asilimia 66 hadi 72.

Utafiti huo uliongozwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Kenya kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, huku Umoja wa Mataifa kupitia mashirika yake, UNICEF, WHO, UNFPA na UN Women ukitoa msaada wa kiufundi na kifedha.

Kwa kina zaidi kuhusu utafiti huu na matokeo yake bofya hapa