Hatua sita za kiafya na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinaweza kuokoa maisha milioni 1.6 kila mwaka – WHO
Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) inasema hatua sita zinazoweza kuchukuliwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda afya ya binadamu zina uwezo wa kuokoa maisha ya watu milioni 1.6 kila mwaka, huku zikizalisha manufaa ya kiuchumi yenye thamani ya matrilioni ya dola.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo mpya ya WHO iliyotolewa Novemba 04, 2026, hatua sita zikitekelezwa kwa kiwango kikubwa duniani zinaweza kuleta manufaa ya kiuchumi yanayokadiriwa kufikia dola trilioni 3.9 za Marekani kila mwaka. Aidha, zinaweza kuongeza mapato ya serikali duniani na manufaa mengine ya kifedha yanayokadiriwa kufikia dola trilioni 5.4 kwa mwaka.
Hatua hizo zinatajwa kuwa ni pamoja na kuanzisha mifumo ya tahadhari za kiafya kuhusu mawimbi ya joto kali, kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama yanayohimili athari za mabadiliko ya tabianchi, huduma za msingi za usafi wa mazingira, pamoja na miundombinu ya usafi binafsi na unawaji mikono.
Hatua nyingine ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi na teknolojia salama za kupikia na kupasha joto majumbani, pamoja na kuweka sera bora za kupanga bei ya nishati ya mafuta ya kisukuku, ikiwemo kuondoa ruzuku zisizo na tija na kutoza kodi stahiki kwa nishati hizo.
WHO inasema hatua hizo hazitalinda afya ya watu pekee, bali pia zitasaidia kupunguza uzalishaji wa gesi zinazochangia ongezeko la joto duniani na kuimarisha uchumi wa nchi.
Akizungumzia matokeo ya ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, anasema ingawa mabadiliko ya tabianchi yamekuwa pia janga la afya ya umma, madhara yake mengi yanaweza kuzuilika kwa kutumia suluhu ambazo tayari zinapatikana.
Ameongeza kuwa wakati serikali zikijiandaa kwa awamu nyingine ya mazungumzo ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, suala la kulinda afya za watu linapaswa kuwa kiini cha hatua zote za kukabiliana na changamoto hiyo.
Ripoti hiyo ambayo imekuja zikiwa zimesalia siku sita kabla ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP31, utakaofanyika nchini Uturuki inaeleza kuwa utekelezaji wa hatua hizo sita duniani kote unaweza kuzuia vifo milioni 1.6 kila mwaka ambapo idadi hiyo ni sawa na kuzuia kifo kimoja kati ya kila vifo 40 vinavyotokea duniani.
Vilevile, hatua hizo zinaweza kusaidia kuzuia uzalishaji wa tani bilioni 16.7 za hewa ya ukaa, kiasi kinacholingana na asilimia 31 ya uzalishaji wa gesi zote za ukaa duniani kwa mwaka, bila kuhusisha uzalishaji unaotokana na matumizi ya ardhi, mabadiliko ya matumizi ya ardhi na misitu.
WHO inabainisha kuwa katika hatua tano kati ya hizo sita, kila dola moja ya Marekani inayowekezwa inaweza kuleta manufaa yenye thamani ya dola 24. Manufaa hayo yanatarajiwa kuwa makubwa zaidi katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, hatua ambayo inaweza kusaidia kupunguza tofauti za kiuchumi na upatikanaji wa huduma za afya.
Miongoni mwa hatua hizo, mifumo ya tahadhari za kiafya kuhusu joto kali imeonekana kuwa na manufaa makubwa ikilinganishwa na gharama za utekelezaji wake. WHO inakadiria kuwa kila dola moja inayowekezwa katika mifumo hiyo inaweza kuleta manufaa yenye thamani ya dola 835. Hii ni kutokana na uwezo wake wa kutumia mifumo iliyopo kutoa tahadhari mapema na kuzuia magonjwa na vifo vinavyosababishwa na joto kali kwa gharama ndogo.
Hata hivyo, sera bora za kupanga bei ya mafuta ya kisukuku ndizo zinazotarajiwa kuleta manufaa makubwa zaidi kwa ujumla. WHO inakadiria kuwa sera hizo zinaweza kuzuia vifo milioni 1.2 kila mwaka, huku zikizalisha manufaa ya kiuchumi ya dola trilioni 3 na mapato ya kifedha ya dola trilioni 5.4 kwa mwaka.
WHO imesema mwaka 2026 umeshuhudia nchi mbalimbali duniani zikikabiliwa na majanga ya hali ya hewa yaliyovunja rekodi, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuchukua hatua za haraka kulinda maisha ya watu na mazingira.
Shirika hilo sasa linazitaka serikali, washirika wa maendeleo na taasisi za ufadhili kutumia ushahidi huo wa kiuchumi kuwekeza katika hatua hizo zilizothibitishwa kuwa na manufaa, kwa ajili ya kulinda afya za watu, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha uchumi wa nchi.