Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan: Mashambulizi ya droni na uhaba wa mafuta vyazima matumaini ya raia wanaohitaji msaada wa dharura

Denise Brown, Mratibu Mkazi na Mratibu wa Kibinadamu UMOJA WA MATAIFA nchini Sudan, anamtembelea mama na mtoto mchanga katika kliniki ya afya katika Jimbo la Kaskazini wakati wa ziara ya ugani.
OCHA Denise Brown, Mratibu Mkazi na uratibu wa Kibinadamu UMOJA WA MATAIFA nchini Sudan, wakati wa ziara ya ugani katika kliniki za Afya za SHF za Jimbo la Kaskazini.

Sudan: Mashambulizi ya droni na uhaba wa mafuta vyazima matumaini ya raia wanaohitaji msaada wa dharura

Msaada wa Kibinadamu

Hali ya kibinadamu nchini Sudan inazidi kuwa tete huku mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (droni) yakilenga miundombinu muhimu ya kiraia, ikiwemo vituo vya nishati na mafuta,  kuvuruga huduma za afya na maji na kuweka hatarini maisha ya maelfu kwa maef ya raia. 

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu nchini humo, Denise Brown, anasema mashambulizi hayo yanaweka rehani maisha ya maelfu ya raia , wakati uhaba wa mafuta ukikwamisha pia operesheni za misaada ya kibinadamu ya kuokoa maisha.

“Wenzetu kutoka Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO) walikuwa katika hospitali moja nje kidogo ya Khartoum. Umeme ulikatika kutokana na mashambulizi haya ya ndege zisizo na rubani. Hospitali hiyo haina jenereta wala paneli za sola. Hivyo, wagonjwa 25 waliokuwa wakitegemea huduma ya kusafisha damu walishindwa kuendelea na matibabu hayo. Hakukuwa na namna nyingine ya kuwasaidia kwa sababu hapakuwa na umeme.”

Karatasi zimetawanywa ovyo ofisini mjini Khartoum kufuatia shambulio. (Maktaba)
© Avaaz/Giles Clarke Karatasi zimetawanywa ovyo ofisini mjini Khartoum kufuatia shambulio. (Maktaba)

Hiyo ni hali halisi ya kila siku, na Bi. Brown anasema kukatika kwa umeme hospitalini kumesababisha wagonjwa 25 waliokuwa wakipatiwa huduma ya kusafisha figo (dialysis)  kukosa matibabu hayo muhimu. Huduma kwa wanawake wanaojifungua na watoto pia zimeathirika.

Wakati huo huo, uhaba wa mafuta umesababisha misururu mirefu ya magari katika mji mkuu Khartoum, huku mamia ya malori ya Umoja wa Mataifa yakiwa yamekwama, yakishindwa kufikisha chakula, vifaa vya lishe na misaada mingine ya kibinadamu kwa watu wanaohitaji.

Anasema hali hiyo inazidisha madhila ya vita, yakiwa ni Pamoja na ukosefu wa mvua na utapiamlo mkali unaokabili maeneo mbalimbali ya nchi, hususan Darfur na Kordofan.

“Kwa kweli, tusipokuwa na mafuta, hatuwezi kusafirisha misaada. Hatuwezi kuwafikishia chakula watu wanaokihitaji. Wala hatuwezi kuwasaidia watoto wanaokabiliwa na unyafuzi au utapiamlo mkali wa kupindukia.”

Mratibu huyo anasema changamoto nyingine ni mashambulizi dhidi ya misafara ya misaada. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, limekabiliwa na mashambulizi saba dhidi ya misafara yake mwaka huu pekee, na kusababisha vifo na upotevu wa chakula kilichokuwa kimekusudiwa kuwasaidia raia walio katika mazingira magumu.

Bi. Brown amezitaka pande zinazohusika na mashambulizi hayo kuyasitisha mara moja, akisisitiza kuwa miundombinu ya kiraia lazima ilindwe kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

“Hili si suala la siasa. Hili ni suala la watu. Ni kuhusu kuwaweka wananchi wa Sudan mbele katika kila kinachoendelea na kuhakikisha kwamba angalau tunakidhi mahitaji yao ya msingi.”

Mwanamume mzee Mwafrika amebeba masanduku matatu ya IOM UN Uhamiaji yaliyorundikwa mabegani mwake nje ya kontena la kijani kibichi la usafirishaji, huku wanaume kadhaa wakisubiri kwenye foleni kwenye ghala.
© IOM UN unaendelea kutoa misaada kwa watu walio katika mazingira magumu nchini Sudan.

Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na wahisani kuongeza ufadhili wa operesheni za kibinadamu nchini Sudan, akisema upungufu wa fedha tayari umeilazimu WFP kupunguza idadi ya watu wanaopatiwa msaada wa chakula pamoja na mgao wanaopokea.

Bi Brown amesisitiza kuwa raia wa Sudan wanahitaji msaada wa haraka ili waweze kukidhi mahitaji yao ya msingi huku vita vikiendelea.