Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Phoebe Okowa toka Kenya ni miongoni mwa majaji 5 waliochaguliwa kuhudumu ICJ

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa wakiwa wameketi kwenye benchi wakati wa kikao rasmi cha mahakama huko The Hague.
© ICJ Mahakama ya Kimataifa ya Haki.

Phoebe Okowa toka Kenya ni miongoni mwa majaji 5 waliochaguliwa kuhudumu ICJ

Haki za binadamu

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wamewachagua majaji watano wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), baada ya kufanyika kwa duru kadhaa za upigaji kura Jumanne, tarehe 3 Novemba.

Majaji waliochaguliwa ni Dapo Akande kutoka Uingereza, François Alabrune kutoka Ufaransa, Mahmoud Daifallah Hmoud kutoka Jordan, Rena Lee kutoka Singapore na Phoebe Okowa kutoka Kenya.

Majaji hao wataanza kutumikia mihula yao ya miaka tisa tarehe 6 Februari 2027.

Nafasi tano za majaji kuwania uchaguzi

Mahakama ya Kimataifa ya Haki, yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi, ndiyo chombo kikuu cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na masuala ya utoaji haki.

Mahakama hiyo ina majaji 15 wanaohudumu kwa mihula ya miaka tisa. Kila baada ya miaka mitatu, uchaguzi hufanyika kujaza nafasi tano za majaji, ili kuhakikisha mwendelezo wa shughuli za mahakama hiyo.

Kwa mujibu wa kanuni za mahakama hiyo, hairuhusiwi kuwa na majaji wawili wenye uraia wa nchi moja.

Kura za Baraza la Usalama na Baraza Kuu

Ili kuchaguliwa, kila mgombea anapaswa kupata kura nyingi za walio wengi katika Baraza Kuu lenye wanachama 193 na Baraza la Usalama lenye wanachama 15.

Vyombo hivyo viwili hupiga kura kwa kujitegemea, kwa njia ya siri, na wagombea wanapaswa kupata wingi wa kura unaohitajika katika kila chombo.

Tofauti na maamuzi mengine ya Baraza la Usalama, haki ya kura ya turufu au veto haitumiki katika uchaguzi huu.

Hivyo, huenda zikahitajika duru kadhaa za upigaji kura kabla ya nafasi zote tano kujazwa.