Kutoka kuhofia kuhukumiwa hadi kuwa mhamasishaji wa afya ya uzazi nchini Kenya
Zipporah Achieng, mama kijana nchini Kenya, ambaye aliwahi kuhofia kuhukumiwa alipokwenda kliniki kupata huduma za afya baada ya kujifungua, sasa amegeuka kuwa mhamasishaji wa afya ya uzazi kwa vijana. Kupitia mpango wa Together for SRHR, unaotekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika manne ya Umoja wa Mataifa kwa lengo hilo la kuelimisha vijana na vijana balehe kuhusu afya ya uzazi, Zipporah anawasaidia vijana kupata taarifa sahihi na huduma za afya ya uzazi bila unyanyapaa
Alipofika kliniki baada ya kujifungua binti yake mdogo, Zipporah Achieng alijikuta ndiye kijana pekee miongoni mwa watu waliokuwa wakisubiri huduma.
Hali hiyo ilimfanya ahofie kuhukumiwa, huku akihisi kuwa mhudumu wa afya hakumpa nafasi ya kutosha kujieleza.
Hapa Zipporah anakumbuka alivyopokelewa, anasema "Nilipojifungua binti yangu mdogo na kufika hapa kliniki, nilikuwa kijana pekee. Mwanzoni nilihisi kuhukumiwa. Nilijiuliza, nikikaa hapa watu hawa wataniona. Nilihisi muuguzi hakunipa muda wa kutosha kujieleza, jambo lililonifanya nijisikie vibaya."
Lakini uzoefu huo ulimpa msukumo wa kuwasaidia vijana wengine kupata huduma bila kupitia changamoto kama zake.
Sasa Zipporah ni mhamasishaji wa afya ya uzazi, akiwapatia vijana matumaini na taarifa sahihi kupitia mradi huo unaotekelezwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la kuhudumia watoto, UNICEF, la afya ya uzazi na idadi ya watu, UNFPA, la kupambana na Ukimwi, UNAIDS na la Afya Duniani, WHO. Anasema "Hatimaye nikawa mhamasishaji wa afya ya uzazi. Kazi yangu ni kurahisisha upatikanaji wa huduma rafiki kwa vijana, kuwapa matumaini, taarifa sahihi na kuwaelewa."
Mpango huo unatekelezwa katika kaunti tatu nchini Kenya. Kigen Korir, mtaalamu wa afya ya uzazi kwa vijana kutoka UNFPA, anazitaja akisema 'ni Nairobi, Samburu na Bungoma."
Katika Kaunti ya Bungoma, UNICEF pia imewajengea uwezo wanahabari kuripoti masuala ya afya ya uzazi na kupambana na taarifa potofu.
Kavutha Mutuvi, mtaalamu wa afya kutoka UNICEF Kenya, anaeleza mabadiliko yaliyojitokeza baada ya mafunzo hayo.
"Kwa mfano, Bungoma tuna kituo kinachotoa huduma rafiki kwa vijana. Tangu tulipowapatia wanahabari mafunzo na kuanza kuzungumzia huduma hizo, kituo kimeripoti ongezeko la matumizi ya huduma zake."
Kwa Zipporah, dhamira yake ni kuhakikisha vijana hawahofii kutafuta huduma za afya ya uzazi, huku wakipata taarifa sahihi zinazowawezesha kufanya uamuzi kuhusu maisha yao.