Siku ya Kimataifa ya Hifadhi za Biosfia, kwa nini ni muhimu?
Hifadhi 797 za Biosfia katika nchi 145 duniani zinaonesha kuwa inawezekana kulinda bioanuwai huku jamii zikiendelea kujenga uchumi na maisha endelevu.
Kadiri miaka inavyosonga, umuhimu wa kukabiliana na changamoto za mazingira unazidi kudhihirika, huku sayari ya dunia ikikabiliwa na vitisho vinavyotokana na mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na upotevu wa bioanuwai.
Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi za Biosfia, inayofanyika kila mwaka Novemba 3, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) linatoa wito wa kubadili kwa kiasi kikubwa uhusiano wa binadamu na mazingira, likisisitiza kuwa maendeleo endelevu yanawezekana pale jamii zinapoheshimu na kuishi kwa uwiano na maumbile.
Biosfia ni nini?
Biosfia ni eneo la kiikolojia la dunia ambamo viumbe hai vyote vinapatikana na kuingiliana na mazingira yao. Eneo hili linajumuisha sehemu mbalimbali za sayari, kuanzia vilindi vya bahari hadi vilele vya milima na sehemu za chini za angahewa.
Biosfia inaunganisha mifumo mikuu ya Dunia, ambayo ni angahewa inayohusiana na hewa, haidrosfia inayohusiana na maji na litosfia inayohusiana na ardhi na miamba.
Ndani ya mifumo hiyo, mimea, wanyama na viumbe vidogo hushirikiana katika mifumo ya ikolojia, huku michakato ya asili ikisaidia kurejesha na kuzungusha virutubisho na rasilimali muhimu kwa uhai.
Hifadhi za Biosfia ni nini na zina umuhimu gani?
Hifadhi za Biosfia ni maeneo yanayotambuliwa na UNESCO chini ya Mpango wa Binadamu na Biosfia (MAB).
Ni maeneo yanayotumika kama maabara hai za kuonesha namna uhifadhi wa bioanuwai na maendeleo endelevu vinavyoweza kwenda pamoja.
Badala ya kuwatenga binadamu na mazingira, hifadhi hizi zinazingatia kuwa jamii na mifumo ya ikolojia vinaweza kustawi kwa pamoja.
Jamii za wenyeji, wakiwemo watu wa asili, mashirika ya kiraia na sekta binafsi, hushirikishwa katika kulinda na kurejesha mifumo ya ikolojia huku wakijenga vyanzo vya mapato na maisha endelevu.
Nguzo tatu za hifadhi za Biosfia
UNESCO inaeleza kuwa hifadhi za Biosfia zinatoa suluhisho la changamoto za kimataifa kupitia nguzo tatu zinazokamilishana.
- Nguzo ya kwanza ni uhifadhi wa mazingira, unaolenga kulinda bioanuwai pamoja na urithi wa kitamaduni.
- Nguzo ya pili ni utafiti wa kisayansi, unaowezesha ukusanyaji wa takwimu, ufuatiliaji wa mazingira, elimu na mafunzo ili kusaidia kufanya maamuzi sahihi.
- Nguzo ya tatu ni maendeleo endelevu, yanayohakikisha shughuli za kiuchumi zinafanyika kwa kuzingatia mahitaji ya kijamii, utamaduni na mazingira.
Kwa kuunganisha nguzo hizo, UNESCO inasema hifadhi za Biosfia zinatoa mifano ya vitendo ya namna jamii zinavyoweza kunufaika na rasilimali za mazingira bila kuziharibu.
Hifadhi 797 katika nchi 145 duniani
Kwa mujibu wa takwimu za UNESCO, dunia ina hifadhi 797 za Biosfia katika nchi 145, zinazochukua eneo la kilomita za mraba milioni 7.5, sawa na zaidi ya asilimia tano ya ardhi yote ya nchi kavu duniani.
Takribani asilimia 90 ya hifadhi hizo zinaingiliana na maeneo muhimu ya bioanuwai, yanayojulikana kama Key Biodiversity Areas.
Hifadhi za kwanza zilitambuliwa mwaka 1976 na tangu wakati huo, maeneo mapya yameendelea kuongezwa katika mtandao huo wa kimataifa.
Hifadhi hizo zinapatikana katika mabara yote isipokuwa Antaktika. Hifadhi ya Mata Atlântica nchini Brazil ndiyo kubwa zaidi duniani, ikiwa na eneo linalozidi kilomita za mraba 88,000.
Aidha, asilimia 50 ya hifadhi zote za Biosfia zinaingiliana na maeneo mengine yanayotambuliwa na UNESCO, yakiwemo maeneo ya Urithi wa Dunia na Mbuga za Jiolojia za Kimataifa.
Wito wa kujenga mustakabali endelevu
Siku ya Kimataifa ya Hifadhi za Biosfia ilitangazwa na Mkutano Mkuu wa UNESCO katika kikao chake cha 41 mwaka 2021. Siku hii ni fursa ya kujifunza kutokana na suluhisho zinazotekelezwa katika hifadhi hizo na kuzitumia kuendeleza mifumo endelevu ya maisha katika maeneo mengine duniani.
UNESCO inasisitiza kuwa hakuna taifa au jamii inayoweza kujitenga na mazingira, na kwamba kulinda asili si jukumu la serikali pekee, bali kunahitaji ushiriki wa jamii, wanasayansi, sekta binafsi na wadau wengine.
Hifadhi za Biosfia zinaonesha kuwa binadamu wanaweza kuendeleza shughuli zao za kiuchumi na kijamii huku wakihifadhi mazingira na kuhakikisha rasilimali za asili zinaendelea kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.