Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM: Zaidi ya watu 7,000 wakimbia makazi yao kutokana na machafuko Cabo Delgado Msumbiji

Mwanamke akiwa amebeba mtoto na begi kubwa ya rangi ya bluu ya misaada ya IOM huku akitembea katika eneo lililoathiriwa na mafuriko nchini Msumbiji.
© IOM/Burak Cerci Mwanamke amebeba mtoto na kifurushi cha misaada akipita katika eneo lililoathiriwa na mafuriko nchini Msumbiji.

IOM: Zaidi ya watu 7,000 wakimbia makazi yao kutokana na machafuko Cabo Delgado Msumbiji

Amani na Usalama

Zaidi ya watu 7,000 wamelazimika kukimbia makazi yao katika jimbo la Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji, tangu mwishoni mwa Septemba mwaka huu, wakikimbia machafuko mapya na hofu ya mashambulizi ya makundi yenye silaha yasiyo ya kiserikali.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM, linasema karibu asilimia 80 ya waliokimbia makazi yao hivi karibuni ni wanawake na watoto, hali inayoongeza shinikizo kwa jamii zinazowahifadhi.

Jamii zinazowahifadhi nazo zakabiliwa na changamoto

Kwa mujibu wa takwimu za IOM, watu 5,794 walikimbia makazi yao kati ya Septemba 21 na Oktoba 13, huku wengine 1,235 wakihama kati ya Oktoba 14 na 27, na kufanya jumla kufikia watu 7,029 ndani ya kipindi cha zaidi ya wiki tano. Baadhi ya familia zimelazimika kuhama zaidi ya mara moja, hali inayozidisha mazingira yao ya hatari.

Mkuu wa Ujumbe wa IOM nchini Msumbiji, Dana Graber Ladek, amesema hali hiyo inazidi kuwaweka katika mazingira magumu wakimbizi wapya na jamii zinazowapokea.

“Familia nyingi zaidi zinatafuta usalama katika jamii ambazo tayari zinawahifadhi watu waliokimbia makazi yao kutokana na machafuko. Karibu watu wanane kati ya kumi ni wanawake na watoto,” amesema Graber Ladek.

Chakula, makazi na afya ni mahitaji ya dharura

IOM inaeleza kuwa katika kipindi cha hivi karibuni cha wiki mbili, watoto 584 na wanawake 386 walikimbia makazi yao, wakiwemo wanawake wajawazito 87, wazee 58, watu wenye ulemavu 18 na watoto wanne waliotengana na familia zao au wasio na walezi.

Baadhi ya wanaume katika familia hizo wamebaki katika maeneo yao ya asili, licha ya hatari ya mashambulizi, ili kuendeleza shughuli za kujipatia kipato. Tathmini ya IOM inaonesha kuwa asilimia 88 ya waliohojiwa wanahitaji chakula, asilimia 71 wanahitaji makazi na asilimia 44 wanahitaji huduma za afya.

Zaidi ya watu 205,000 tayari wamehama Cabo Delgado

Hadi Oktoba 2026, jimbo la Cabo Delgado lilikuwa na zaidi ya watu 205,000 waliokimbia makazi yao katika maeneo 84, huku zaidi ya nusu yao wakiwa watoto.

Wengi wa waliohama hivi karibuni wanategemea familia na jamii zinazowahifadhi, hali inayoongeza mzigo kwa kaya na huduma za kijamii ambazo tayari zinakabiliwa na changamoto.

IOM yaendelea kutoa msaada licha ya ukata wa fedha

Graber Ladek ameonya kuwa jamii zinazowahifadhi zinahitaji msaada wa chakula, makazi na huduma za afya, akisema bila msaada wa wakati, maisha ya familia zilizokimbia makazi yao na wale wanaozipokea yanaweza kuwa magumu zaidi. IOM inaendelea kutoa msaada wa makazi ya dharura, vifaa muhimu vya nyumbani, maji safi, usafi na huduma za ulinzi, pamoja na msaada wa afya ya akili na kisaikolojia.

Hata hivyo, shirika hilo linasema kuendelea kwa watu kuhama makazi yao na kupungua kwa ufadhili kunazidi kudhoofisha juhudi za kibinadamu wakati mahitaji ya msaada wa dharura yanaongezeka kila uchao.