UNICEF: Mashambulizi ya anga ya Urusi nchini Ukraine yamezidi kuigharimu elimu
Ukraine imekumbwa na takribani mashambulizi 2,000 dhidi ya sekta ya elimu tangu uvamizi kamili wa Urusi mwaka 2022, huku mashambulizi 270 yakiripotiwa mwaka huu pekee, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).
Kupitia taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi msemaji wa UNICEF Ricardo Pires amesema tangu kuanza kwa mwaka wa masomo, “watoto wamekumbwa na wastani wa saa 34 za tahadhari za mashambulizi ya anga wakati wa masomo shuleni, sawa na zaidi ya asilimia 13 ya muda uliopangwa kwa ajili ya kujifunza.”
Hadi kufikia Oktoba 20, amesema baadhi ya maeneo yameathiriwa zaidi, huku tahadhari hizo zikichukua zaidi ya saa 60.
Katika mji mkuu Kyiv, idadi ya tahadhari za mashambulizi ya anga iliongezeka kutoka mara 12 mwezi Septemba 2025 hadi mara 71 mwezi Septemba 2026.
Katika maeneo ya Dnipropetrovsk, Kirovohrad na Kharkiv, watoto wamekumbwa na tahadhari za mashambulizi ya anga kwa zaidi ya saa 60 wakati wa masomo. Hii ni sawa na takribani robo ya muda wote uliopangwa kwa ajili ya kujifunza, na kuwaathiri zaidi ya watoto 560,000.
Elimu Katikati ya ving'ora vya mashambulizi
“Nimerejea hivi karibuni shuleni na kuhudhuria masomo ana kwa ana, hata hivyo, bado tunatumia sehemu kubwa ya siku yetu ya masomo kwenye makazi ya kujikinga kutokana na mashambulizi ya anga,” amesema Katia, mwenye umri wa miaka 15, kutoka eneo la Mykolaiv, ambaye ushuhuda wake umeshirikishwa na Bwana Pires.
Msemaji huyo amesisitiza athari zinazoonekana za vita kwa afya ya akili ya watoto wote nchini Ukraine. Amekumbuka ziara yake ya mwezi mmoja uliopita, ambapo alizungumza na watoto wanaolazimika kusomea chini ya ardhi, “kwa sababu si salama kwao kuwa juu ya ardhi”.
Licha ya usalama wa kiasi unaotolewa na madarasa yaliyojengwa chini ya ardhi kwa ajili ya kujikinga, “hata huko, bado wanakabiliwa na tahadhari za mashambulizi ya anga wakati wote. Unaweza kuhisi kuwa baadhi yao, hasa wale wenye umri mkubwa, wana wasiwasi mkubwa na walitueleza kuwa wanashindwa kuzingatia masomo kikamilifu na kujitenga kwa muda na yanayoendelea juu ya ardhi.”
Athari kwa watoto kila mahali
Akizungumzia wasiwasi huo, mkuu wa mfuko wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa Elimu Haiwezi Kusubiri (Education Cannot Wait) ECW, Maysa Jabout, amesema vita vina athari kubwa kwa watoto kila mahali.
Amesema hali hiyo imelazimu mfuko huo kuweka kipaumbele katika ufadhili wa huduma za ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia na kijamii kwa watoto.
Ameeleza kuwa hatua hiyo inamaanisha kupunguza sehemu ya fedha muhimu zinazohitajika kwa ajili ya ufundishaji na ujifunzaji, ili kusaidia watoto kukabiliana na changamoto za kujifunza katika mazingira magumu sana.