Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu bilioni 6.3 duniani wanatumia intaneti, lakini bilioni 2 bado hawajaunganishwa: ITU

Wanafunzi wakiandika kwenye kompyuta mpakato darasani.
ITU/G. Anderson Watu wanaumia Intaneti mjini Nairobi.

Watu bilioni 6.3 duniani wanatumia intaneti, lakini bilioni 2 bado hawajaunganishwa: ITU

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Watu bilioni 6.3 duniani, sawa na asilimia 76 ya idadi ya watu wote, wanatumia intaneti mwaka 2026, lakini wengine bilioni mbili bado hawana huduma hiyo, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Kimataifa la Mawasiliano, ITU, iliyotolewa leo Novemba 3 mjini Geneva, Uswisi.

Ripoti hiyo, Facts and Figures 2026, inaonesha ongezeko la watumiaji wa intaneti kutoka bilioni 6.1, sawa na asilimia 74 mwaka 2025, huku pengo la upatikanaji na matumizi ya teknolojia ya kidijitali likiendelea kuwepo, hususan kati ya nchi tajiri na maskini.

Katika nchi zenye kipato cha juu, asilimia 93 ya watu wanatumia intaneti, ikilinganishwa na asilimia 32 pekee katika nchi zenye kipato cha chini.

Katibu Mkuu wa ITU, Doreen Bogdan-Martin, amesema katika zama hizi za akili mnemba ( AI), kutokuwa na intaneti kunamaanisha kukosa fursa nyingi, kuanzia elimu hadi ajira.

Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kila mtu, popote alipo, anaweza kupata na kutumia intaneti kwa manufaa yake.

Pengo la kidijitali linapungua, lakini bado ni kubwa

Ripoti hiyo imeainisha tofauti mbalimbali katika upatikanaji na matumizi ya intaneti duniani:

  • Jinsia: Asilimia 79 ya wanaume wanatumia intaneti, ikilinganishwa na asilimia 74 ya wanawake.
  • Umri: Vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wanaongoza kwa matumizi ya intaneti kwa asilimia 86, ikilinganishwa na asilimia 74 ya watu wa umri mwingine.
  • Maeneo: Asilimia 82 ya wakazi wa mijini wanatumia intaneti, ikilinganishwa na asilimia 63 vijijini.
  • Umiliki wa simu: Asilimia 84 ya watu wenye umri wa miaka 10 na kuendelea wanamiliki simu za mkononi. Katika nchi tajiri ni zaidi ya asilimia 95, lakini nchi maskini ni asilimia 57.
  • Mitandao ya simu: Asilimia 97 ya watu duniani wanaishi maeneo yenye angalau mtandao wa 3G. Hata hivyo, mtandao wa 5G unawafikia asilimia 59 pekee, huku nchi tajiri zikiwa na asilimia 86 na maskini asilimia 4.
  • Matumizi ya data: Watumiaji wa intaneti kupitia simu katika nchi tajiri hutumia wastani wa GB 20 kwa mwezi, mara sita zaidi ya GB 3.4 katika nchi maskini.
  • Gharama: Bei ya huduma za intaneti kupitia simu imepungua hadi wastani wa asilimia 1.2 ya pato la taifa kwa kila mtu, ikilinganishwa na asilimia 2.3 kwa intaneti ya kudumu.

Kuhakikisha intaneti inamnufaisha kila mtu katika zama za AI

Ripoti inaonesha kuwa kwa mara ya kwanza, nchi zinazoendelea zisizo na bahari na nchi ndogo za visiwani zimefikia lengo la gharama nafuu za intaneti kupitia simu.

Hata hivyo, katika nchi zenye maendeleo duni zaidi, gharama hizo bado zinafikia asilimia 6.1 ya pato la taifa kwa kila mtu.

Mkurugenzi wa Ofisi ya Maendeleo ya Mawasiliano ya ITU, Cosmas Luckyson Zavazava, amesisitiza kuwa “upatikanaji wa intaneti pekee hautoshi bila ujuzi wa kidijitali.” Ameonya kuwa bila ujuzi huo na huduma bora za intaneti, manufaa ya teknolojia mpya, ikiwemo AI, yataendelea kuwa nje ya uwezo wa watu wengi.