ILO: Usawa wa kijinsia waongeza faida kwa kampuni, lakini wanawake bado wako nyuma katika uongozi
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi Duniani, ILO, limesema kampuni zinazotekeleza sera za usawa wa kijinsia na utofauti mahali pa kazi zinapata manufaa makubwa zaidi kibiashara, ikiwemo ongezeko la faida. Hata hivyo, shirika hilo limeonya kuwa kupungua kwa utekelezaji wa sera hizo kunatishia maendeleo yaliyopatikana katika kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi.
Katika ripoti yake mpya iliyotolewa leo Novemba 3 mjini Geneva, Uswisi, yenye jina Women in Business and Management: Scaling Success, ILO imesema idadi ya kampuni zinazoongozwa na wanawake imeongezeka katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
Kampuni zenye wanawake wenyeviti wa bodi zimeongezeka kutoka asilimia 13.1 mwaka 2013 hadi asilimia 30.9 mwaka 2025, huku zile zenye wanawake wakurugenzi watendaji zikiongezeka kutoka asilimia 23.4 hadi asilimia 28.2.
“Usawa wa kijinsia ni haki ya msingi, na ushahidi unaonesha wazi kuwa pia ni kichocheo kikubwa cha biashara endelevu na ukuaji wa uchumi,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Gilbert F. Houngbo, akisisitiza kuwa, “Kipaumbele sasa ni kuzigeuza sera na ahadi kuwa maendeleo halisi yanayoweza kupimwa.”
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, karibu kampuni saba kati ya kumi zilizoshiriki utafiti mwaka 2025 zimesema juhudi za kuimarisha usawa wa kijinsia na utofauti zimeboresha matokeo ya biashara zao. Aidha, kati ya kampuni zilizoripoti ongezeko la faida kutokana na juhudi za kuwawezesha wanawake katika uongozi, asilimia 87.4 zilisema faida zao ziliongezeka kwa angalau asilimia tano.
Juhudi bado zinahitajika
Hata hivyo, ILO imesema wanawake bado wanashikilia chini ya theluthi moja ya nafasi za usimamizi duniani, sawa na asilimia 30 pekee. Wakati huo huo, ingawa asilimia 74.8 ya kampuni zina sera za usawa wa kijinsia, kampuni zinazotekeleza hatua za kuimarisha usawa huo zimepungua kutoka asilimia 37.4 mwaka 2018 hadi asilimia 26.5 mwaka 2025.
Hatua zilizoathirika ni pamoja na likizo ya uzazi, programu za kusaidia wanawake na juhudi za kuhakikisha malipo sawa kwa kazi zenye thamani sawa.
Mkurugenzi wa Ofisi ya ILO inayoshughulikia shughuli za waajiri, Maria Paz Anzorreguy, amesema, “Katika wakati huu ambapo kampuni zinashindana kupata wafanyakazi wenye ujuzi na vipaji, kuacha uwezo wa wanawake bila kutumiwa kikamilifu hakuna mantiki kubwa kibiashara.” Ameongeza kuwa ushahidi unaonesha hatua zinazofanya kazi, na sasa kinachohitajika ni kuzitekeleza na kuzipanua.
Ripoti hiyo, iliyotokana na utafiti uliohusisha kampuni 11,957 katika nchi 99, imetoa wito kwa waajiri kuimarisha fursa za wanawake kufikia nafasi za uongozi, kuweka malengo yanayopimika na kushughulikia vikwazo vinavyowakabili, ikiwemo mgawanyo usio sawa wa majukumu ya malezi na mitazamo ya kijamii inayozuia maendeleo yao kazini.
Unaweza kutazama video ya kueleza kw kifupi kuhusu ripoti hiyo kwa kubofya hapa