Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Akili Mnemba (AI) inabadilisha namna tunavyofikiri: Je, tutatambua mabadiliko hayo kwa wakati?

Wanafunzi mbalimbali wa shule ya upili huketi kuzunguka meza ya darasa ya mbao, wakiandika na kupitia karatasi pamoja huku wakijiandaa kwa mtihani.
© Adobe Stock/PP Kundi la wanafunzi wa shule ya upili wanajadili mradi wa ushirikiano.

Akili Mnemba (AI) inabadilisha namna tunavyofikiri: Je, tutatambua mabadiliko hayo kwa wakati?

Na Na Sachin Gur
Utamaduni na Elimu

Akili mnemba (AI) inaahidi kurahisisha maisha. Kwa kubonyeza vitufe vichache tu, inaweza kuandika barua pepe, kufupisha ripoti, kutoa mawazo na kujibu maswali magumu ndani ya sekunde chache. Kwa watu wengi, hali hii inaonekana kama hatua kubwa ya kiteknolojia inayolingana na kuwasili kwa intaneti.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mwanasayansi wa ubongo David Rock, swali kubwa zaidi si kile ambacho Akili Mnemba inatufanyia, bali ni kile ambacho huenda akili mnemba itatufanyia.

“Kwa namna fulani, teknolojia haitubadilishi kabisa,” amesema Rock.

Ubongo wa binadamu bado hufanya maamuzi, hutatua matatizo na kukabiliana na changamoto kwa namna ileile ambayo umekuwa ukifanya kwa maelfu ya miaka. Hata hivyo, historia inaonesha kuwa matukio makubwa na shinikizo la muda mrefu vinaweza kuacha athari za kudumu kwenye ubongo, na hivyo kuathiri tabia kwa miaka mingi au hata vizazi.

Kitendawili kikubwa cha Akili Mnemba

Mapinduzi ya sasa ya kiteknolojia yanaweza kuwa moja ya nyakati hizo.

Rock anasema tofauti iliyopo ni kwamba teknolojia inazidi kutufanya tuhisi kuwa tuna uwezo wa kudhibiti karibu kila kitu. Unahitaji usafiri? Bonyeza kitufe. Unataka chakula kiletwe nyumbani? Bonyeza kingine. Unatafuta taarifa? Zinapatikana papo hapo.

Hisia hiyo inayoongezeka ya kujitegemea inaweza kuwa yenye kuwezesha. Lakini pia inaleta mtego usioonekana kwa urahisi, hasa mifumo ya AI inapozidi kuwa na uwezo wa kufanya kazi ambazo hapo awali zilihitaji juhudi kubwa za kiakili.

“Usiache ubongo wako nje ya mchakato”

Wasiwasi mkubwa si kwamba akili mnemba inazidi kuwa na nguvu, bali ni kwamba watu wanazidi kuwa tayari kukabidhi uwezo wao wa kufikiri kwa teknolojia hiyo.

Hivi karibuni, Rock ameelezea hali ya sasa kuwa ni kipindi cha mpito kutoka hofu ya kukosa fursa za kupitwa kwa utumizi wa akili mnemba, hadi hali ya kuchoshwa au kukerwa na matumizi yake.

Mashirika yalikimbilia kutumia zana za akili mnemba zalishi, mara nyingi kabla ya kuelewa kikamilifu athari zake za muda mrefu. Sasa, matokeo ya hatua hizo yanazidi kuwa wazi.

Anachokiona kinamtia wasiwasi.

Anasema ni idadi ndogo tu ya wafanyakazi, huenda kati ya asilimia tano hadi 10, wanaotumia akili mnemba kwa namna iliyokusudiwa: kuikabidhi kazi za kawaida ili kuachia uwezo wao wa kiakili kwa ajili ya kazi zinazohitaji juhudi kubwa zaidi. Hata hivyo, wengi wanafanya kinyume chake.

“Ubongo unapenda kuhifadhi nishati,” amesema. “Inavutia sana kuuokoa ubongo wako usifikirie kabisa.”

Anasema matokeo yake ni kudhoofika taratibu kwa uwezo wa kufanya maamuzi sahihi. Watu wanapokabidhi si kazi za kawaida pekee bali pia uchambuzi, tathmini na ufanyaji maamuzi kwa teknolojia, wanahatarisha kupoteza uwezo wa kutofautisha mawazo mazuri na mabaya.

Akili mnemba inaweza kutoa majibu kwa haraka, lakini kasi si sawa na hekima.“Usiache ubongo wako nje ya mchakato. Ubongo wako usiposhiriki, unapoteza ujuzi huo haraka sana,” amesema.

Mgogoro wa umakini

Kuongezeka kwa matumizi ya akili mnemba kunatokea wakati ambapo watu wengi tayari wanapata changamoto ya kuzingatia mambo.

Kwa mujibu wa Rock, changamoto kubwa inayowakabili wafanyakazi leo si ukosefu wa taarifa, bali wingi wa taarifa unaozidi uwezo wao wa kuzichakata.

Analinganisha hali ya sasa na kuwasili kwa barua pepe, ambayo iliongeza kwa kiasi kikubwa wingi wa taarifa ambazo watu walipaswa kuzichakata.

Hata hivyo, kwa sasa kiwango hicho ni kikubwa zaidi. Wafanyakazi wanakumbwa na ujumbe, taarifa mpya, taarifa na muhtasari unaotengenezwa na akili mnemba, mara nyingi kwa kiwango kinachozidi uwezo halisi wa ubongo wa binadamu kukimudu.

“Kwa kweli, ubongo wetu una mipaka halisi,” amesema.

Dkt. David Rock akizungumza na hadhira iliyoketi katika kikao cha Tamasha la Ujuzi UN , akiwa amesimama nyuma ya jukwaa lenye nembo UN na akiashiria kwa mkono mmoja.
Habari za UN/Mashael Shah. David Rock ndiye mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi wa Mishipa.

David Rock ni mwanzilishi mwenza na Afisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi ya NeuroLeadership.

Kompyuta zinaweza kuchakata maelfu ya maamuzi ndani ya muda mfupi. Binadamu hawawezi kufanya hivyo. Hata hivyo, mashirika mengi yanaendelea kufanya kazi kana kwamba watu wana uwezo usio na kikomo wa kuzingatia mambo na kufanya maamuzi.

Rock anaamini kuwa jamii bado iko katika kipindi cha kuzoea AI, kama ilivyokuwa katika siku za mwanzo za magari kabla ya kuwepo kwa sheria za barabarani na mipaka ya mwendo kasi. Teknolojia imewasili kwa kasi zaidi kuliko kanuni za kijamii na mifumo ya ulinzi inayohitajika ili kuitumia kwa uwajibikaji.

Teknolojia inayotaka kuwa rafiki yako

Tofauti na mafanikio mengine ya kiteknolojia yaliyotangulia, akili mnemba huenda inabadilisha jambo la msingi zaidi kuliko kazi.

“Inadukua uhusiano wa kihisia,” amesema Rock.

Ingawa televisheni, vitabu na simu janja zilishindania umakini wetu, akili mnemba inazidi kushindania mahusiano yetu. Watu wengi zaidi wanageukia programu za mazungumzo za akili mnemba, si kwa ajili ya kupata taarifa pekee, bali pia kwa mazungumzo, urafiki na ushauri.

Mwelekeo huo unamtia wasiwasi.

Amesema tafiti zinaonesha kuwa watu wanaotumia muda mwingi kuwasiliana na akili mnemba zinazotoa urafiki wanaweza kujihisi wapweke zaidi badala ya kupunguza upweke. Tafiti nyingine zinaonesha uhusiano kati ya utegemezi mkubwa wa programu za mazungumzo na kuongezeka kwa kujitenga na mwingiliano wa kijamii katika maisha halisi.

Ubongo wa binadamu uliendelezwa katika mazingira ya mahusiano na watu wengine. Kubadilisha mwingiliano huo kwa kiwango kikubwa na mashine kunaweza kuleta gharama za kisaikolojia ambazo jamii ndiyo inaanza kuzielewa.

Akili mnemba inavyozidi kuwa na uwezo mkubwa zaidi, na teknolojia za roboti, kompyuta zenye kasi zaidi na intaneti ya kizazi kijacho zinapounganishwa, maswali hayo huenda yakazidi kuwa muhimu.

Kwa nini uhusiano wa kibinadamu unaweza kuwa na thamani zaidi

Kwa namna ya kushangaza, kadiri mashine zinavyozidi kuwa na uwezo mkubwa, ndivyo mahusiano ya kibinadamu yanavyoweza kuwa na thamani zaidi.

Rock anaamini kuwa siku zijazo zitatoa kipaumbele kikubwa kwa uaminifu, uhalisia na uhusiano wa kweli kati ya binadamu. Katika ulimwengu ambamo mashine zinaweza kutengeneza maudhui, kuchambua data na kuiga mazungumzo, kile kinachobaki kuwa cha kipekee kwa binadamu kinaweza kuwa na thamani zaidi.

“Uzoefu wa kibinadamu utakuwa na thamani kubwa zaidi,” amesema.

Badala ya kuchukua nafasi ya watu, akili mnemba   huenda hatimaye ikaongeza umuhimu wa mitandao ya kibinadamu, mahusiano ya kina na ushirikiano wenye maana.

Hata hivyo, mustakabali huo haujahakikishwa. Ni moja tu ya njia zinazowezekana za kukabiliana na ulimwengu unaobadilika kwa kasi ya teknolojia.

Na kasi hiyo ndiyo hasa ambayo Rock anatarajia kuongezeka.

“Mabadiliko hayajawahi kuwa ya kasi hivi, lakini hayatakuwa ya polepole hivi tena,” amesema.

Ujuzi ambao huenda ukawa muhimu zaidi

Kwa hiyo, watu wanawezaje kuendana na mabadiliko hayo? jibu la Rock linategemea dhana moja: kufikiri kuhusu namna tunavyofikiri.

Badala ya kuruhusu akili mnemba  ichukue udhibiti, anasema watu wanapaswa kubaki na mamlaka kamili ya kufanya maamuzi, huku wakitumia mifumo hiyo kupinga na kupanua mitazamo yao badala ya kuichukua nafasi.

Akili mnemba inaweza kuwasaidia watu kuzingatia mitazamo ambayo huenda wasingeitambua vinginevyo, kupima mawazo yao ya awali na kuchunguza tafsiri mbadala. Hata hivyo, jukumu la kufanya maamuzi sahihi lazima libaki kwa binadamu.

Anaita mbinu hiyo “binadamu kuwa mstari wa mbele”. Anasema teknolojia hiyo hufanya kazi vizuri zaidi inapokuza uwezo wa kufikiri badala ya kuuchukua nafasi.

Akili mnemba inavyozidi kuwa sehemu ya maisha ya kila siku, tofauti hiyo inaweza kuwa muhimu sana. Mashine zinaweza kuwa na akili zaidi na kufanya kazi kwa kasi zaidi, lakini changamoto kwa binadamu itakuwa kuhakikisha kuwa akili zetu zinaendelea kushiriki kikamilifu.

Kwa sababu huenda mustakabali usitegemee kiwango cha akili ambacho akili mnemba itafikia, bali kama tutaendelea kutumia akili tuliyo nayo tayari.

Dkt. David Rock, aliyeanzisha istilahi neuroleadership, ni mwanzilishi mwenza na Afisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi ya NeuroLeadership, kampuni ya kimataifa ya ushauri inayotumia sayansi ya ubongo kuboresha uongozi na utendaji wa mashirika.

Ni mwandishi wa vitabu kadhaa, vikiwemo kitabu kilichouzwa sana Your Brain at Work na kitabu chake cha hivi karibuni Your Story Has a Villain. Yeye ni mmoja wa wazungumzaji wakuu katika Tamasha la Ujuzi la Umoja wa Mataifa 2026, lenye kaulimbiu isemayo “Watu katika Kitovu”.