Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres: Mauaji ya wanahabari yasiyo na adhabu kwa wahusika lazima yakomeshwe

Mwandishi wa habari wa kike wa Kizungu aliyevaa kofia ya bluu ya PRESS na fulana isiyopitisha risasi akiwa ameshika kipaza sauti huku akirekodiwa na kamera ya video karibu na jengo la matofali lililoharibiwa huku wanajeshi wakiwa nyuma.
© Adobe Stock/Supamotion Mwandishi wa habari za vita akiwa amevaa vifaa vya kujikinga akiripoti akiwa hai karibu na jengo lililoharibiwa.

Guterres: Mauaji ya wanahabari yasiyo na adhabu kwa wahusika lazima yakomeshwe

Haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito wa kukomeshwa kwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanahabari na kuhakikisha wanaohusika na mauaji yao wanafikishwa mbele ya sheria, akieleza kuwa mauaji sita kati ya kila saba ya wanahabari duniani hayapati haki.

Katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Kutoadhibiwa kwa Uhalifu dhidi ya Wanahabari, inayoadhimishwa kila mwaka Novemba 2, Guterres amesema wanahabari kote duniani wanaendelea kulipa gharama kubwa kwa kusema ukweli na kutekeleza wajibu wao wa kuhabarisha umma.

Amesema licha ya mchango muhimu wa wanahabari katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa na kuwawajibisha walio madarakani, wengi wao wanakabiliwa na vitisho, ufuatiliaji wa mawasiliano yao, mashitaka mahakamani, mashambulizi ya kimwili na vifungo gerezani. Baadhi yao wanateswa na hata kuuawa kwa sababu tu ya kutekeleza majukumu yao.

“Katika mwaka uliopita, angalau wanahabari 34 walipoteza maisha yao. Mauaji sita kati ya kila saba ya aina hiyo hayajaadhibiwa. Katika maeneo yenye migogoro, kiwango cha kutoadhibiwa kwa wahusika kinakaribia asilimia 100,” amesema Guterres.

Amesisitiza kuwa hali hiyo ni ukiukwaji mkubwa wa haki kwa waathirika na familia zao, pamoja na jamii nzima inayotegemea wanahabari kupata taarifa na kushiriki katika masuala yanayoihusu.

“Hali hii ya aibu lazima ikomeshwe,” amesema.

Haki kwa wanahabari ni msingi wa demokrasia

Katibu Mkuu amesema hakuna jambo lolote linalopaswa kuwazuia wanahabari kutekeleza majukumu yao, kwa kuwa kazi yao ni muhimu katika kulinda haki za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria.

Ametaka kila tukio la uhalifu dhidi ya wanahabari lichunguzwe, wahusika wote wafikishwe mbele ya sheria na mashambulizi dhidi ya wanahabari yanayofanyika kupitia mtandao yakomeshwe.

Hatua zimepigwa, lakini bado haitoshi

Pamoja na changamoto hizo, Guterres amesema kuna ushahidi kwamba hatua za kukomesha kutoadhibiwa kwa wahusika wa uhalifu dhidi ya wanahabari zinaweza kuleta matokeo chanya.

Ameeleza kuwa tangu kuzinduliwa kwa Mpango Kazi wa Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama wa Wanahabari na Suala la Kutoadhibiwa kwa Wahusika mwaka 2012, kiwango cha kutoadhibiwa kwa uhalifu huo katika nchi zisizokumbwa na migogoro ya silaha kimepungua kutoka asilimia 94 hadi asilimia 77.

Hata hivyo, amesema juhudi zaidi zinahitajika ili kuhakikisha wanahabari wanafanya kazi zao kwa usalama na bila hofu.

Katika kuhitimisha ujumbe wake, Guterres amesisitiza umuhimu wa haki kwa wanahabari wote wanaolengwa kutokana na kazi zao.

“Katika Siku hii ya Kimataifa ya Kutokomeza Kutoadhibiwa kwa Uhalifu dhidi ya Wanahabari, tunadai haki. Wanahabari wanapolengwa na taarifa zao kuzimwa, sote tunakuwa waathirika,” amesema.

Soma zaidi kuhusu siku hiyo kwa kubofya hapa