Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana sita wakimbizi kuandika historia katika Olimpiki ya Vijana Dakar 2026

Wanariadha sita vijana wakimbizi waliovaa shati nyeupe za polo zinazolingana na suruali nyeusi wakishikilia mabango ya "Tutaonana Dakar" huku wakipiga picha nje.
© UNHCR/Charity Nzomo Timu ya Olimpiki ya Wakimbizi yenye washiriki sita ikipigwa picha katika kambi ya mazoezi huko Eldoret, Kenya, kabla ya Michezo ya Olimpiki ya Vijana huko Dakar, Senegal inayoanza 31 Oktoba 2026

Vijana sita wakimbizi kuandika historia katika Olimpiki ya Vijana Dakar 2026

Wahamiaji na Wakimbizi

Vijana sita wakimbizi, wasichana watatu na wavulana watatu, wanatarajiwa kuandika historia kwa kuwa timu ya kwanza ya wakimbizi kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Vijana itakayoanza kesho tarehe 31 Oktoba mjini Dakar, Senegal.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, vijana hao waliochaguliwa, wanaoishi Kenya na Uganda, watashindana katika michezo ya riadha, judo na taekwondo pamoja na wanamichezo wengine wapatao 2,700 kutoka duniani kote. Mashindano hayo yatakayokamilika tarehe 13 Novemba yatakuwa ya kwanza ya Olimpiki kufanyika barani Afrika.

“Vijana hawa sita wanauonesha ulimwengu kile ambacho wakimbizi wanaweza kufanikisha wanapopewa nafasi. Michezo hutengeneza fursa, hujenga hisia ya kuwa sehemu ya jamii na huwasaidia vijana wakimbizi kujenga upya maisha yao,” amesema Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR anayeshughulikia Ulinzi, Edem Wosornu.

Sanamu ya pete za Olimpiki katika bustani katika Makao Makuu UN , New York.
UN News/Jing Zhang Nembo ya Olimpiki katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa

Vinaja hawashindanii medali pekee bali matumaini

Timu hiyo inaongozwa na Yiech Pur Biel, mkimbizi kutoka Sudan Kusini na Balozi Mwema wa UNHCR, aliyeshiriki katika timu ya kwanza ya wakimbizi kwenye Michezo ya Olimpiki ya Rio mwaka 2016.

“Miaka kumi iliyopita nilisimama kwenye jukwaa la Olimpiki nikiwa mwanamichezo mkimbizi. Leo, kuona kizazi kipya cha wakimbizi kikifuata njia hiyo ni jambo la kipekee sana,” amesema Biel, akisisitiza kuwa vijana hao hawashindanii medali pekee bali pia wanawapa matumaini wakimbizi wengine.

Timu hiyo imeundwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, IOC, na kusimamiwa na wakfu wa Olimpiki wa wakimbizi au Olympic Refuge Foundation kwa ushirikiano na UNHCR na wadau wengine.

UNHCR imesema ushiriki wao unakuja wakati zaidi ya watu milioni 117 wakiwa wamelazimika kuhama makazi yao duniani, wakiwemo milioni 39 katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Shirika hilo limetoa wito wa kupanuliwa kwa fursa za michezo na elimu kwa vijana wakimbizi hata baada ya mashindano kumalizika.

Pete tano zilizounganishwa kwa rangi ya bluu, njano, nyeusi, kijani, na nyekundu kwenye mandhari ya bluu nyepesi.
UN /Eskinder Debebe Nembo ya olimpiki ikiwa na miduara mitano ikimaanisha idadi ya mabara ambayo yanashikiri michuano hiyo.

Wakimbizi wanaounda timu hiyo

Washiriki wa Timu ya Wakimbizi ya Olimpiki ya Dakar 2026 watakuwa:

  • Arno (anaishi Kenya, mchezo: Judo, wanaume, uzito wa kilo chini ya 55)

  • Clement (anaishi Kenya, mchezo: Riadha, mbio za mita 800 kwa wanaume)

  • Florence (anaishi Uganda, mchezo: Riadha, mbio za mita 200 kwa wanawake)

  • Lourance (anaishi Kenya, mchezo: Taekwondo, wanawake, uzito wa kilo chini ya 49)

  • Nyataba (anaishi Kenya, mchezo: Riadha, mbio za mita 800 kwa wanawake)

  • Rachid (anaishi Uganda, mchezo: Riadha, mbio za mita 200 kwa wanaume)