Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

New York yapandisha bustani kuzuia mafuriko huku kina cha bahari kikiendelea kuongezeka

Mwonekano wa angani wa Upande wa Mashariki wa Manhattan ukionyesha mradi wa Ustahimilivu wa Pwani wa Upande wa Mashariki ukiwa na uwanja wa michezo, barabara kuu, Daraja la Queensboro, na anga ya juu ya Mto East.
© NYCDDC Maegesho dhidi ya mafuriko imejengwa upande wa mashariki wa Kisiwa cha Manhattan kando ya East River katika Jiji la New York.

New York yapandisha bustani kuzuia mafuriko huku kina cha bahari kikiendelea kuongezeka

Tabianchi na mazingira

Kimbunga Sandy kilipiga Jiji la New York, na kusababisha mawimbi makubwa ya dhoruba yaliyofurika nyumba, mifumo ya treni za chini ya ardhi na vichuguu, kukatiza umeme na kuzua moto uliosababisha vifo. Katika muda wa saa 48 pekee, watu 44 walipoteza maisha, karibu wakazi milioni mbili wa New York walikosa umeme, na wagonjwa 6,500 walihamishwa kutoka hospitalini na makao ya wazee.

New York iliapa kwamba maafa kama hayo hayatatokea tena.

Hata hivyo, mabadiliko ya tabianchi yalipoanza kutishia kuleta hali mbaya zaidi za hewa na kuongeza kwa hatari kina cha bahari katika jiji hilo la pwani, ahadi ya kuzuia maafa kama hayo ilimaanisha kujenga miundombinu mikubwa ya kuimarisha ustahimilivu katika ukanda mzima wa pwani ya jiji.

Miaka 14 baada ya Kimbunga Sandy, UN News ilitembelea sehemu moja ya mradi huo wa mabilioni ya dola: Mradi wa Ustahimilivu wa Pwani ya Upande wa Mashariki (East Side Coastal Resiliency – ESCR).

Vifaa vizito vya ujenzi ikijumuisha kipakiaji cha mbele cha manjano na kreni ya mnara hufanya kazi kwenye eneo la udongo lenye marundo ya changarawe mbele,
© NYCDDC NYC, Mto Mashariki.

Kilichojengwa chini ya ardhi

Kaskazini mwa Daraja la Williamsburg, kreni nyeupe huinua ndoo zilizojaa udongo kutoka kwenye jahazi na kumwaga udongo huo kwenye mashine za kusogeza ardhi. Hatua kwa hatua, Bustani ya East River inainuliwa kwa hadi futi 10, sawa na takriban mita tatu.

Bustani hiyo ni sehemu moja ya mfululizo wa vizuizi vya kuzuia mafuriko vinavyojengwa kando ya ufukwe wa Manhattan kwa umbali wa zaidi ya maili tatu, sawa na kilomita 5. Mradi wa Ustahimilivu wa Pwani ya Upande wa Mashariki, ulioanzishwa baada ya Kimbunga Sandy kufurika eneo hilo mwaka 2012, pamoja na mradi mwingine mdogo ulio kusini, ni uwekezaji wa takriban dola bilioni 2 unaolenga kuwalinda zaidi ya wakazi 110,000.

“Eneo hili lote lilikuwa limefurika,” amesema Bobby Issac, Kamishna Msaidizi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Ustahimilivu wa Pwani katika Idara ya Usanifu na Ujenzi ya Jiji la New York.

Amesema wakati wa Kimbunga Sandy, maji yalifunika angalau ghorofa moja ya majengo ya makazi ya umma yaliyokuwa nyuma yake, na wakazi hawakuweza kuingia wala kutoka.

Sehemu kubwa ya miundombinu ya ulinzi katika eneo hili haionekani kwa urahisi. Ukuta wa kuzuia mafuriko unapita katikati ya bustani hiyo iliyojengwa upya. Kando ya maji, nguzo zilizojaa zege zimezama takriban futi 100, sawa na mita 30, ndani ya ardhi iliyorejeshwa, ambayo inaweza kuwa na mabaki ya vitu mbalimbali, kuanzia gati za zamani hadi mabaki ya meli.

“Kile unachokiona juu ya ardhi ni theluthi moja tu ya kilichojengwa,” amesema Issac.

Dhoruba inapokaribia, hakuna kitu katika bustani kinachohitaji kuhamishwa. Katika maeneo mengine ya ufukwe, wafanyakazi watafunga milango 18 ya kuzuia mafuriko kwa kuizungusha au kuisogeza, huku kusini zaidi wakinyanyua vizuizi karibu 100 vinavyoinuka kutoka ardhini.

Kwa mujibu wa Issac, usanifu wa mfumo huo pia umezingatia uwezekano wa kina cha bahari kuongezeka kwa takriban inchi 30, sawa na sentimita 76.

Amesema takriban asilimia 90 ya mfumo huo tayari umewekwa, na vizuizi vya muda vinaweza kuziba sehemu zilizo wazi kwa taarifa ya siku chache hadi kazi itakapokamilika mwaka 2027.

Zaidi ya maafa ya Kimbunga Sandy

Mbali na vifo vilivyotokea, Kimbunga Sandy kilisababisha uharibifu wa mali wenye thamani ya dola bilioni 19, amesema Kathryn Prybylski, Kamishna Msaidizi wa Ofisi ya Ustahimilivu wa Pwani ya Jiji la New York, ambaye atakuwa na jukumu la kuendesha kuta na milango mipya ya kuzuia mafuriko.

“Miradi hii inayojengwa sasa katika maeneo mbalimbali ya jiji ni matokeo ya Kimbunga Sandy. Kwa kweli, sasa ni wakati wetu wa kuangalia siku zijazo,” amesema.

Hali ya kimataifa inaongeza uharaka wa kuchukua hatua. Kwa mujibu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), kasi ya kupanda kwa kina cha bahari duniani imekaribia kuongezeka mara mbili tangu vipimo vya setilaiti vilipoanza mwaka 1993. Wakati huohuo, ongezeko la joto baharini linachochea dhoruba kali zaidi za kitropiki.

Kwa jiji lenye ukanda wa pwani wa maili 520, sawa na kilomita 840, tishio si dhoruba kubwa inayoweza kutokea baadaye pekee, bali pia mawimbi ya kawaida ya bahari. Prybylski ameonya kuwa bila hatua za ulinzi, wakazi wengi wa New York watakabiliwa na mafuriko ya mara kwa mara yanayosababishwa na mawimbi ya bahari katika miongo ijayo.

Katika baadhi ya maeneo, amesema, mafuriko hayo yanaweza kutokea mara moja au mbili kwa mwezi, au hata mara 10 kwa mwezi. Hatimaye, baadhi ya barabara zinaweza kufurika kila siku wakati wa kupanda kwa maji ya bahari, jambo litakalobadilisha jinsi watu wanavyosafiri kwenda kazini na kuwapeleka watoto wao shuleni.

Mtazamo wa angani wa barabara ya makazi iliyofurika maji jijini New York huku maji yakizama magari yaliyoegeshwa kati ya majengo ya ghorofa ya matofali baada ya mvua kubwa ya mawe ya Sandy.
© Adobe Stock/Solepsizm Vitongoji vingi kusini mwa Manhattan vilifurika maji wakati Kimbunga Sandy kilipopiga New York. (Maktaba)

Tishio kubwa zaidi duniani

Tweet URL

New York ni mojawapo tu ya miji inayokabiliwa na vitisho hivi. Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa imebaini kuwa karibu asilimia 10 ya watu duniani, sawa na takriban watu milioni 770, wanaishi katika maeneo ya pwani yaliyo chini ya mita tano kutoka usawa wa maji wakati wa mawimbi makubwa. Hali hiyo inawaweka katika hatari kubwa ya athari za kupanda kwa kina cha bahari.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres,  ameonya  kuwa “miji mikubwa katika kila bara itakabiliwa na athari kubwa” kutokana na kupanda kwa kina cha bahari, akiitaja New York miongoni mwa miji iliyo hatarini.

“Mradi wa New York wa kuzuia mafuriko ni hatua inayostahili kupongezwa. Pia ni ujumbe kwa miji yote mikubwa,” amesema Navid Hanif kutoka Idara ya Uchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa (DESA), katika mahojiano na habari ya UN.

Amesema hatua zinazochukuliwa na New York zinapaswa kutambuliwa, kuthaminiwa na kuigwa katika maeneo mengine duniani.

Ingawa kupanda kwa kina cha bahari kunatishia zaidi miundombinu katika miji ya nchi zenye kipato cha juu kama New York, Miami na Guangzhou nchini China, hali hiyo ni tishio kwa uwepo wa jamii katika miji ya Asia Kusini iliyo katika maeneo ya chini, ikiwemo Kolkata, Mumbai na Dhaka.

Zaidi ya watu milioni 14 katika Asia Kusini wako katika hatari ya kupoteza makazi yao kutokana na maeneo yao kufunikwa kabisa na maji. Wakati huohuo, jamii katika Fiji, Vanuatu, Visiwa vya Solomon na visiwa vingine vya Pasifiki vilivyo katika maeneo ya chini tayari zimelazimika kuhama.

Kukabiliana na athari na kuimarisha ustahimilivu

Umoja wa Mataifa, ambao makao yake makuu yako umbali wa chini ya maili mbili kaskazini mwa mradi wa Ustahimilivu wa Pwani ya Upande wa Mashariki (ESCR), ni mshirika hai katika kuunga mkono juhudi za kupunguza mabadiliko ya tabianchi na kukabiliana na athari zake duniani.

Katika mkutano wa hivi karibuni kuhusu kupanda kwa kina cha bahari, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zilipitisha Tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu Kupanda kwa Kina cha Bahari. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa nchi zote wanachama kukubaliana kuhusu waraka mmoja wa pamoja unaohusu suala hilo.

Tamko hilo lilitoa wito wa kuwepo kwa ufadhili unaotabirika zaidi na unaopatikana kwa urahisi kwa ajili ya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ustahimilivu, hasa katika nchi za visiwa vidogo na nchi zilizoendelea kwa kiwango cha chini zaidi.

Mradi wa Ustahimilivu wa Pwani ya Upande wa Mashariki wa New York unaonyesha namna uwekezaji wa aina hiyo unavyoweza kuwanufaisha wakazi wa eneo husika.

Kathryn Prybylski amesimama kwenye sehemu ya matembezi ya ufukweni iliyotengenezwa kwa lami katika mradi wa East Side Coastal Resiliency huko Manhattan, huku Daraja la Manhattan na Mto East zikiwa nyuma yake.
Habari za UN/Daniel Dickinson Kathryn Prybylski, Kamishna Msaidizi wa Uhandisi wa Ustahimilivu wa Pwani wa Jiji la New York.

Katika Bustani ya East River ambayo sasa imeinuliwa, watu wanaotembea kwa miguu wanafurahia njia za kutembea kando ya mto huku wakitazama mandhari ya Brooklyn. Bustani hiyo pia ina maeneo ya kijani yaliyotunzwa vizuri na nafasi za shughuli za jamii, zikiwemo viwanja vya michezo, maeneo ya watoto kuchezea na sehemu za kuchomea nyama.

“Tuko katika bustani hii mara mbili kila siku, kila siku. Tunaipenda! Ni mfano mzuri wa jinsi ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi unavyoweza kuwasaidia watu kufurahia maisha yao,” amesema Liz, mkazi wa eneo hilo aliyekuwa akipita na kumtembeza mbwa wake.