Türk aonya kuhusu ukatili dhidi ya raia katika migogoro duniani
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, ameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa ukatili dhidi ya raia katika maeneo yenye migogoro duniani, hususan Sudan, ambako mauaji, ubakaji na mashambulizi yanayotumia ndege zisizo na rubani yanaendelea kugharimu maisha ya watu. Aidha amepongeza vijana kwa kusimama kidete kudai haki na uwajibikaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York Marekani katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Türk ameeleza imani yake na ubinadamu.
“Ninaamini ya dhati kwamba idadi kubwa ya watu duniani kote wanajali haki za binadamu. Wanakataa ukatili. Wanakataa ajenda inayopinga haki, ajenda ambayo, kwa bahati mbaya, siku hizi tunaiona ikiendeshwa kwa namna iliyoratibiwa sana. Na wanatamani ulimwengu bora zaidi, lakini wanajihisi wako peke yao kabisa.”
Imani yake inazidi kwa kuona namna kizazi cha sasa cha vijana maarufu kama Gen Z wanafuatilia na kudai haki, na uwajibikaji “Hebu tuangalie Serbia, kwa mfano, lakini pia kile kilichotokea Bangladesh, Nepal, Madagaska, maandamano mengi ya Gen Z kote ulimwenguni ambapo unaona watu wakijitoa kudai haki zao na kupambana na ufisadi na ukosefu wa usawa na kuuliza kinaga ubaga haki za binadamu zinawakilisha nini haswa.”
Mizozo inagharibu maisha ya wengi
Kamishna Türkpia amezungumzia migogoro inayoendelea katika maeneo mbalimbali duniani kuanzia Ukraine, Gaza, Somalia, Sudan mpaka Sudan Kusini.
“Mimi mwenyewe nimefika Sudan Kusini mara mbili. Nina wasiwasi mkubwa sana kuhusu kinachoendelea. Huu ni mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu. Ni vita vinavyoendelea kupiganwa kwa kutumia ndege zisizo na rubani. Kwa hakika, vifo vingi vya raia leo vinatokana na matumizi ya ndege zisizo na rubani."
Mkuu huyo wa haki za binadamu alielezea kuhusu vitendo vilivyofanywa na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) hasa yale waliyoyafanya mwezi Aprili mwaka 2025 katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Zamzam, na baadaye huko El Fasher nakuvitaja kuwa ni vitendo vya ukatili wa kutisha zaidi kuliko unavyoweza kufikiria.
"Nilizungumza na baadhi ya waathirika waliokimbia El Fasher: wamenieleza kuhusu ubakaji wa halaiki, mauaji ya haraka bila utaratibu wa kisheria, na mauaji ya watu wengi. Yaani, ni mambo ya kutisha kweli. Tunachotumaini sote ni kwamba, kuwe na uelewa mpana zaidi kuhusu hali ilivyo nchini Sudan, na kwamba wale wenye ushawishi kwa upande wowote kati ya pande zinazopigana watumie ushawishi huo ipasavyo ili kukomesha hali hii.”
Kamishna huyo Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa pia amesisitiza umuhimu wa uandishi wa habari kwa uhuru. Ameeleza mshikamano wake na waandishi wa habari na wafanyakazi wengine wa vyombo vya habari wanaoshambuliwa, ikiwa ni pamoja na katika maeneo yenye migogoro, na kutoa wito wa kuendelea kuzungumzia masuala ya haki za binadamu katika mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa.