Ufuatiliaji wa manusura wa Ebola nchini DRC waendelea
- Kliniki mbili za manusura zimeanzishwa
- Moja Beni na nyingine Bunia
- Ufuatiliaji ni muhimu kwani virusi husalia muda mrefu mwilini
- WHO yataja kwenye majimaji kama vile manii
Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC) ambako mlipuko wa Ebola ya virusi vya Bundibugyo bado unaendelea, ufuatiliaji wa wagonjwa waliopona ni muhimu kama moja ya sehemu za mwitikio dhidi ya mlipuko wa ugonjwa huo uliothibitishwa mwezi Mei mwaka huu, ukiwa ni mlipuko wa 17.
Wagonjwa waliopona, mara baada ya kuruhusiwa kwenye vituo vya matibabu, (ETC), huendelea kupatiwa misaada ikiwemo ya kisaikolojia na uchunguzi kupitia kliniki mahsusi.
Kwa msaada wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la afya, (WHO), Misaada ya dharura, (OCHA) na serikali ya Uingereza, kliniki mbili za aina hiyo zimeanzishwa, moja huko Beni jimboni Kivu Kaskazini, na Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri, ambako ni kitovu cha mlipuko wa sasa.
Miongoni mwa wanaopata huduma hizo ni Christian Buna, ambaye kupitia video ya WHO kanda ya Afrikav iliyochapishwa kwenye ukurasa wake wa X, anaonekana akiingia kwenye kliniki iliyoko Bunia.
Anasema, “niliambukizwa Ebola, nilithibitishwa kupona miezi kadhaa iliyopita. Nimefika hapa kwenye kliniki ya waliopona kwa ufuatiliaji zaidi.”
Tangu kuanza kwa mlipuko mwezi Mei mwaka huu nchini DRC, zaidi ya wagonjwa 2,500 wamepona. Lakini baada ya kupona baadhi ya athari za ugonjwa huo zinaweza kusalia mwilini.
Dokta Roland Kasagama, ni Mratibu wa Tiba katika kituo cha waliopona Ebola mjini Bunia ambapo anasema, “Mgonjwa anaporuhusiwa kutoka kituo cha matibabu, huwa wanapata changamoto mbali mbali. Kwa hivyo, tuko hapa kuwapatia huduma za kina.”
Kwa msaada wa fedha kutoka OCHA na serikali ya Uingereza, WHO iliweza kujenga kliniki ya kwanza ya manusura wa Ebola mjini Bunia. Manusura wanatakiwa kuhudhuria kliniki mara moja kwa mwezi ili wafanyiwe uchunguzi.
Tayari Christian ameketi na anafanyiwa uchunguzi wa vipimo mbali mbali.
Dkt. Huguette Mbuyi Musadi, anatoka kitengo cha Wizara ya Afya ya DRC kinachohusika na Huduma kwa Manusura wa Ebola. Yeye anasema kwamba, “Manusura anapofika, tunamfanyia uchunguzi wa kina kuona iwapo kuna hali yoyote ya kiafya inayohusiana na ugonjwa aliopona. Na pia majimaji ya mwilini mwake kuona iwapo kuna masalia ya virusi vya Ebola.”
Kliniki ni ya kisasa, ambapo kamera inatupeleka ndani na kuoneshwa vifaa vya uchunguzi. WHO inasema huduma zinazotolewa hapa ni pamoja na uchunguzi wa afya kwa ujumla, vipimo vya maabara, usaidizi wa lishe, huduma ya kisaikolojia na dawa.
Kabla ya kupatiwa dawa, manusura wanaelimishwa juu ya umuhimu wa kutumia kondomu au mipira ya kiume wakati wa kujamiiana.
Elisee Mbusi, mfamasia kwenye kituo hiki cha manusura wa Ebola anasema hilo ni muhimu kwa kuwa; “Virusi vinaweza kusalia kwenye manii au shahawa kwa muda mrefu sana. Iwapo manusura ataendelea kujamiiana bila kutumia kondomu, anahatarisha kumuambukiza mwenza wake virusi vya Ebola.”
Kwa WHO, kuanzishwa kwa vituo hivi vya manusura wa Ebola, kuna malengo makuu mawili kama asemavyo Dkt. Brys Busanga, Kiongozi wa Kitengo cha Ufuatiliaji wa Manusura, WHO; “mosi ni kuepusha ugonjwa huo kujirudia tena kwenye jamii kupitia wagonjwa waliopona. Sababu ya pili ni kuwapatia huduma za matibabu dhidi ya changamoto yoyote ya kiafya kwa manusura wa Ebola baada ya kuruhusiwa kutoka vituo vya matibabu.”
Tangu mwezi uliopita wa Septemba zaidi ya manusura 400 wa Ebola wamepatiwa huduma kwenye kliniki ya Bunia, jimboni Ituri.
Video inatamatika, Christian akionekana akiondoka kituoni hapo akiwa na tabasamu usoni, akisema, “Nilipokelewa vizuri. Na ninamasisha “manusura wengine nao waje pia kwa huduma za uchunguzi, kwa kuwa ni vema kufahamu hali yako ya kiafya.”