Wiki ya UN ya upokonyaji silaha ni nini? na kwa nini ni muhimu?
Wiki ya Umoja wa Mataifa ya upokonyaji silaha, inayoadhimishwa kila mwaka kuanzia tarehe 24 Oktoba, inaangazia umuhimu wa kupunguza silaha, kuzuia migogoro ya kivita na kujenga dunia salama na yenye amani zaidi.
Kwa nini Wiki ya Upokonyaji Silaha huadhimishwa?
Wiki ya Upokonyaji Silaha ni maadhimisho ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa yanayolenga kuongeza uelewa wa umma na kuboresha uelewa kuhusu masuala ya upokonyaji silaha na umuhimu wake katika kudumisha amani na usalama wa kimataifa pamoja na maendeleo endelevu.
Maadhimisho hayo huanza tarehe 24 Oktoba, Siku ya Umoja wa Mataifa, ambayo huadhimisha kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa mwaka 1945.
Wiki hiyo ilipendekezwa kwa mara ya kwanza katika Hati ya Mwisho ya kikao maalumu cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu upokonyaji silaha kilichofanyika mwaka 1978, kupitia azimio S-10/2.
Mwezi Desemba 1995, Baraza Kuu lilipitisha azimio 50/72 B, likizialika serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kuendelea kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo ili kuimarisha uelewa wa umma kuhusu upokonyaji silaha.
Kwa nini upokonyaji silaha ni muhimu?
Upokonyaji silaha na udhibiti wa silaha vimekuwa sehemu muhimu ya juhudi za Umoja wa Mataifa za kuzuia na kumaliza migogoro na mapigano ya kivita tangu kuanzishwa kwa Shirika hilo.
Kupunguza silaha na kuimarisha udhibiti wa uzalishaji, umiliki na uhamishaji wake kunaweza kusaidia kudumisha amani na usalama wa kimataifa, kuwalinda raia, kujenga uaminifu miongoni mwa Mataifa na kuunga mkono maendeleo endelevu.
Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa mivutano inayoongezeka na vitisho vya kiusalama vinapaswa kushughulikiwa kupitia mazungumzo ya kisiasa na majadiliano ya kutafuta suluhu, badala ya kuongeza mrundikano wa silaha.
Upokonyaji silaha pia una umuhimu wa kibinadamu. Kupunguza upatikanaji na matumizi ya silaha kunaweza kusaidia kupunguza vifo na majeruhi miongoni mwa raia, watu kulazimika kuyahama makazi yao na uharibifu wa miundombinu muhimu wakati wa migogoro.
Ni changamoto zipi kuu zinazotia wasiwasi?
Umoja wa Mataifa unaangazia changamoto kadhaa kuu zinazofanya upokonyaji silaha kuwa muhimu zaidi.
Silaha za nyuklia na silaha za maangamizi makubwa: Uwezo wake mkubwa wa kusababisha uharibifu unaendelea kuwa tishio kwa binadamu. Kuzuia kuenea kwa silaha hizo na kuendeleza juhudi za kuondoa silaha za nyuklia ni vipaumbele muhimu vya kimataifa.
Silaha za kawaida: Mrundikano mkubwa wa silaha za kawaida na biashara haramu ya silaha hizo vinatishia amani na usalama wa kimataifa. Matumizi ya silaha nzito za kawaida katika maeneo yenye wakazi pia yanawaweka raia katika hatari kubwa.
Teknolojia mpya za silaha: Maendeleo katika teknolojia kama vile silaha zinazojiendesha zenyewe na vita vya mtandaoni (cyberwarfare) yanaibua maswali mapya kuhusu usalama wa dunia, ulinzi wa raia na mustakabali wa mapigano ya kivita.
Changamoto hizi zimeendelea kupata umakini mkubwa kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.
Umoja wa Mataifa unafanya nini?
Umoja wa Mataifa unaendelea kuunga mkono juhudi za kimataifa za kuendeleza upokonyaji silaha, udhibiti wa silaha na kuzuia kuenea kwa silaha.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa wito wa kurejesha upokonyaji silaha katika kitovu cha juhudi za dunia za kufikia amani na usalama. Ajenda yake ya upokonyaji silaha, “Kulinda Mustakabali Wetu wa Pamoja”, inaeleza hatua zinazoweza kuchukuliwa kupunguza vitisho vinavyotokana na silaha za maangamizi makubwa, silaha za kawaida na teknolojia mpya.
“Upokonyaji silaha lazima urejeshwe katika kitovu cha juhudi zetu za pamoja za kuleta amani na usalama,” amesema Guterres.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Upokonyaji Silaha (UNODA) inaunga mkono juhudi za kimataifa zinazolenga kufikia lengo la muda mrefu la upokonyaji silaha wa jumla na kamili, chini ya udhibiti madhubuti na wenye ufanisi wa kimataifa.
Ofisi hiyo pia inashughulikia athari za kibinadamu zinazotokana na silaha za kawaida na changamoto za kiusalama zinazoibuliwa na teknolojia mpya, zikiwemo silaha zinazojiendesha zenyewe.
Nani anaweza kushiriki katika Wiki ya Upokonyaji Silaha?
Serikali, mashirika ya kimataifa, makundi ya asasi za kiraia, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za elimu na wananchi wanaweza kuchangia katika maadhimisho hayo.
Shughuli zinaweza kujumuisha mijadala ya umma, kampeni za elimu, utetezi, utafiti na mipango inayolenga kuongeza uelewa kuhusu udhibiti wa silaha na madhara yake ya kibinadamu.
Wiki hiyo pia hutoa fursa ya kutambua juhudi za watu na mashirika yanayochangia kujenga mustakabali salama zaidi kupitia upokonyaji silaha, udhibiti wa silaha na kuzuia kuenea kwa silaha.
Umuhimu wake kwa dunia
Upokonyaji silaha hauhusu tu kupunguza idadi ya silaha. Pia unahusu kuzuia migogoro, kulinda maisha ya binadamu, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuweka mazingira yanayowezesha maendeleo endelevu.
Wakati dunia ikiendelea kukabiliwa na vitisho vya silaha za nyuklia, kuenea kwa silaha za kawaida na maendeleo ya haraka ya teknolojia za kijeshi, Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa mazungumzo, majadiliano na hatua za pamoja ni muhimu katika kupunguza hatari na kuhakikisha mustakabali wenye amani zaidi.