Heko Misri kwa kuwa nguzo ya ushirikiano wa kimataifa - Guterres
Katika ziara yake ya tisa nchini Misri tangu ashike wadhifa wa Ukatibu Mkuu Januari 2017, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amepongeza nafasi muhimu ya Misri katika kipindi hiki cha “changamoto kubwa zaidi zinazoikabili ukanda wa Masharikiya Kati kwa ujumla,” pamoja na juhudi zake za kutoa nafasi kwa diplomasia na kuzikutanisha pande zinazohusika katika meza ya mazungumzo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Cairo, Misiri leo kwenye mkutano uliohudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa taifa hilo la kaskazini mwa Afrika, Guterres ameitaja Misri kama nguzo muhimu ya hatua za kimataifa zinazochukuliwa kwa ushirikiano wa nchi mbalimbali.
Vikwazo vya Israeli dhidi ya misaada ya kiutu Gaza viondolewe
Guterres ameelezea shukrani zake kwa nafasi ya Misri katika juhudi za upatanishi na utoaji wa misaada ya kibinadamu kuhusiana na Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli.
Amesisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo vilivyowekwa na Israeli dhidi ya misaada ya kibinadamu na kuondoa vizingiti vinavyozuia utekelezaji wa mpango wa kina wa kumaliza mzozo wa Gaza, ulioidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Amezungumzia pia umuhimu wa kuwalinda raia na kuheshimu sheria za kimataifa.
Njarama za kutokomeza kabila fulani
Guterres ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu vitendo vya Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu. Amelitaja upanuzi wa makazi ya walowezi, kuendelea kwa ubomoaji na ufukuzaji wa watu kutoka makwao bila kukoma, kufukuzwa kwa Wapalestina kutoka katika ardhi zao, kuongezeka kwa ghasia zinazofanywa na walowezi, na familia za Wapalestina kukabiliwa na mashambulizi. Amesema mashambulizi hayo pia yamewalenga waandishi wa habari na wanadiplomasia.
“Tunashuhudia hali ambayo matumizi ya shuruti yanaongezeka, huku tishio la kumaliza kabila fulani likizidi kudhihirika kwa kiwango kikubwa zaidi. Hili lazima likomeshwe,” amesema Katibu Mkuu.
Kikao na Rais al-Sisi wa Misri
Katibu Mkuu Guterres amezungumza pia na Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi, ambapo amewaeleza waandishi wa habari anasifu nafasi ya Misri katika juhudi za upatanishi zinazolenga kusaidia kuweka mazingira mwafaka kwa mazungumzo kati ya Marekani na Iran.
Ametoa ujumbe thabiti na ulio wazi kwa pande zote, akisisitiza umuhimu wa kupunguza mvutano na kutafuta suluhisho za kidiplomasia kabla hali haijafikia hatua ya kushindwa kudhibitiwa. Pia amesisitiza umuhimu wa kurejesha kikamilifu haki na uhuru wa usafiri wa majini ndani na karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz na Bab al-Mandeb, kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Mapigano Sudan yasitishwe; Libya nako kipindi cha mpito wa kisiasa kimalizike
Katibu Mkuu amesema kuwa wakati wa ziara hiyo, alijadiliana pia na maafisa wa Misri kuhusu hali nchini Sudan. “Nimesisitiza umuhimu wa kusitishwa kwa mapigano nchini humo na kuhakikisha kwamba mustakabali wa Sudan unaamuliwa na wananchi wake kupitia mchakato wa kisiasa jumuishi unaolinda umoja, mamlaka ya kujitawala na ukamilifu wa mipaka ya nchi hiyo.”
Kuhusu Libya, Guterres amesema umefika wakati wa kujenga juu ya kasi iliyopatikana katika mchakato wa kisiasa, kuunganisha taasisi na kuweka mazingira ya kufanyika kwa uchaguzi wa kitaifa, ili hatimaye kumaliza kipindi kirefu cha mpito wa kisiasa. amegusia pia juhudi zinazoendelea kufanywa na mwakilishi wake nchini Libya kwa lengo hilo.
Guterres amesifu Misri kwa mshikamano wake katika kuwahifadhi wakimbizi na kusisitiza kwamba nchi zinazowapa usalama watu wanaokimbia vita na machafuko zinahitaji na zinastahili kupata msaada mkubwa kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.
Soma hotuba nzima hapa.