Mafunzo kazini yatajwa kama daraja la kuunganisha vijana na ajira Afrika
Mafunzo kazini yatajwa kama daraja la kuunganisha vijana na ajira Afrika
- Swali la msingi ni je nani agharamie?
- Waajiri, vyama vya wafanyakazi na serikali washirikiane
- Hatua hii itaimarisha ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira
Mafunzo yanayofanyika katika maeneo halisi ya kazi yanaweza kuwa suluhisho muhimu la kupunguza pengo kati ya ujuzi unaopatikana katika taasisi za mafunzo na mahitaji ya waajiri, kwa mujibu wa wataalamu waliozungumza katika podikasti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi Duniani (ILO), kuelekea ya Wiki ya Ujuzi Afrika 2026, inayoendelea mjini Harare, Zimbabwe.
Katika mahojiano yaliyoongozwa na Anders Johnsson wa ILO, Albert Rukeisa wa Chama cha Waajiri Tanzania, (ATE) na Priyadarshini Gupta wa Baraza la Vyama vya Wafanyakazi Mauritius (MTUC) wamesisitiza umuhimu wa kuunganisha mafunzo na uzoefu wa vitendo kazini ili kuwawezesha vijana kupata ajira zenye staha.
Rukeisa amesema, “changamoto kubwa ni kutoshirikishwa kikamilifu kwa waajiri katika kuandaa mitaala, viwango vya mafunzo na matokeo yanayotarajiwa. Hali hiyo husababisha wahitimu kuwa na sifa za kitaaluma, lakini kukosa ujuzi unaohitajika katika maeneo ya kazi.”
Mfano wa Tanzania na programu ya uanagenzi kwa vijana
Ameeleza kuwa mafunzo kazini, ikiwemo mafunzo ya vitendo na uanagenzi, yanapaswa kuwapa vijana uzoefu wa kiufundi na stadi laini, huku yakisaidia biashara kuongeza tija na ushindani.
Ametolea mfano nchini Tanzania ambako amesema 2016 au 2017, serikali ilizindua miongozo ya kitaifa kuhusu mafunzo kwa vitendo na uanagenzi, iliyozielekeza kampuni pamoja na wahitimu kuhusu namna ya kuendesha mafunzo katika maeneo yao ya kazi.
“Kwa hiyo, tunasisitiza kuwa suala hili si kuwaweka tu wahitimu katika maeneo ya kazi, bali ni kuwasaidia katika safari yao ya kujifunza, kwa kuwapatia mafunzo na ukuzaji wa vipaji ulioandaliwa vizuri, ili wanapomaliza wawe na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira. Hii inajumuisha ujuzi wa kitaalamu pamoja na stadi nyingine laini, kama vile mawasiliano, ushirikiano na uwezo wa kutatua matatizo,” amesema Afisa huyo wa ATE,
Mafunzo ya uanagenzi yaendane na malipo stahiki
Kwa upande wake, Gupta amesisitiza kuwa kupata cheti hakumaanishi moja kwa moja kupata ajira, hasa pale waajiri wanapodai uzoefu ambao vijana hawajapata nafasi ya kuujenga.
“Uanagenzi bora unahitaji washauri wenye ujuzi, mrejesho wa mara kwa mara, makubaliano yaliyoandikwa, malipo stahiki, usalama kazini na ulinzi wa kijamii. Wanafunzi hawapaswi kutumiwa kuchukua nafasi za wafanyakazi wa kawaida,” amesema Bi. Gupta kwenye podikasti hiyo iitwayo Mustakabali wa ajira au kwa kiingereza, Future of Work.
Ushirikiano na ufadhili ni muhimu
Wazungumzaji ambao wote ni wajumbe wa Mtandao wa Afrika wa wakufunzi mahiri wa mafunzo yanayotolewa mahali pa kazi, unaoungwa mkono na ILO kwa ufadhili wa Ujerumani wametaka serikali, waajiri, vyama vya wafanyakazi na taasisi za mafunzo kushirikiana kupanga programu zinazozingatia mahitaji halisi ya sekta mbalimbali. “Serikali zinapaswa kusaidia ufadhili, vifaa vya mafunzo na posho kwa wanafunzi, huku waajiri wakitoa mafunzo yenye ubora na mazingira salama,” amesema Bwana Rukeisa.
Pia wameonya kuwa akili mnemba (AI) na teknolojia zinabadilisha ajira, hivyo mitaala inapaswa kusasishwa mara kwa mara kupitia mazungumzo ya kijamii ili wafanyakazi waweze kujiandaa kwa kazi mpya.
wamehitimisha kuwa mafanikio yanahitaji majukumu yaliyo wazi, fedha za kutosha, viwango vya ubora na ushiriki wa waajiri pamoja na wafanyakazi katika maamuzi. Lengo ni kujenga mfumo unaowawezesha vijana kubadilisha ujuzi wao kuwa fursa halisi za ajira zenye staha.
Wiki ya Ujuzi Afrika iliyoanza jumatatu Oktoba 12 itamalizika Ijumaa hii.