Mtaalamu wa UN: Hatua za kukomesha ukatili dhidi ya watoto hazilingani na kasi ya hatari zinazoongezeka
Mtaalamu wa UN: Hatua za kukomesha ukatili dhidi ya watoto hazilingani na kasi ya hatari zinazoongezeka
Amani na Usalama
Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukatili dhidi ya Watoto ametoa wito wa kuimarishwa kwa hatua za kimataifa za kuwalinda watoto wa kiume na wa kike wanaokabiliwa na ongezeko la migogoro na majanga mbalimbali, akisema juhudi za sasa hazitoshi kukabiliana na hali hiyo.
“Karibu watoto milioni 45 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na migogoro, lakini pia kutokana na majanga ya asili na mzozo wa tabianchi,” amesema Najat Maalla M’jid, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York.
Ukosefu wa uhakika wa upatikanaji wa chakula na kuenea kwa kasi kwa teknolojia pia vinakwamisha juhudi za kupunguza ukatili dhidi ya watoto, amesema Bi. M’jid baada ya kuwasilisha ripoti yake ya mwisho kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Ameitaja ripoti hiyo kuwa ni “kengele ya kuamsha ili kuchochea uhamasishaji na hatua zaidi.”
Uwasilishaji wa ripoti hiyo kwa nchi wanachama umefanyika wakati wa kuadhimisha miaka 20 tangu kutolewa kwa utafiti wa kwanza wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya watoto.
Akizungumzia mabadiliko yaliyotokea duniani tangu wakati huo, amesisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa bado inakabiliwa na “migogoro mingi inayoendelea na yenye utata”, kufuatia janga la COVID-19.
Maisha ya watoto yamekwama katika migogoro
Kwa sasa, mtoto mmoja kati ya watano anaishi katika umaskini uliokithiri, “na si katika nchi maskini pekee, bali pia katika nchi tajiri, licha ya fedha zote zinazotengwa kwa ajili ya uhamisho wa fedha, mafao ya fedha na kadhalika,” amesema.
Masuala mengine yanayotia wasiwasi ni pamoja na kupanda kwa bei duniani na ukosefu wa uhakika wa upatikanaji wa chakula. Aidha, baadhi ya nchi zinashuhudia hatua za kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana katika haki za binadamu.
Hali hiyo inachangiwa pia na kile alichokiita “kuenea kwa kasi kubwa sana kwa teknolojia, ikiwemo akili mnemba (AI), ambayo inatoa fursa lakini pia inafungua mianya mikubwa ya unyonyaji wa kingono wa watoto, unyanyasaji kupitia mitandao, picha na video bandia zinazotengenezwa kwa teknolojia ya kidijitali (deepfakes), pamoja na kuhusishwa kwa watoto katika shughuli za uhalifu.”
Ujumbe ulio wazi
Bi. M’jid alianza hotuba yake kwa kutafakari kuhusu utafiti wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2006, ambao ulionyesha kuwa ukatili dhidi ya watoto hutokea katika kila nchi na katika mazingira yote, iwe nyumbani, shuleni, kwenye jamii au kwingineko.
Amekumbusha miaka ya kazi na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali, wakiwemo watoto na vijana, katika kuandaa utafiti huo.
“Utafiti huu wa kihistoria unaangazia kanuni kuu mbili: ukatili unaweza kuzuiwa kila wakati, na ukatili hauwezi kamwe kuhalalishwa,” amesema, akibainisha kuwa ujumbe huo pia umesisitizwa katika Ajenda ya mwaka 2030 ya Maendeleo Endelevu.
Juhudi bado hazitoshi
Mwakilishi huyo Maalum amesema miongo miwili iliyopita imeshuhudia mageuzi ya sheria na sera, lakini pia “changamoto nyingi katika kuhakikisha utekelezaji wake kwa ufanisi na kufanya huduma zipatikane kwa watoto na walezi wao.”
Ameelekeza kwenye “mafunzo yaliyopatikana”, yakiwemo umuhimu wa dhamira thabiti ya kisiasa inayotafsiriwa kuwa huduma zinazolinda watoto na kuimarisha ustawi wao, zikiungwa mkono na bajeti maalumu.
Pia amesifu ongezeko la ushiriki wa watoto na vijana katika ngazi zote, pamoja na kuimarika kwa huduma jumuishi katika maeneo mbalimbali duniani.
“Lakini tatizo ni kwamba juhudi hizi hazijaenezwa kwa kiwango kinachohitajika, na hatuendi kwa kasi,” amesema. “Tatizo ni kwamba suluhisho zetu daima zinabaki nyuma ya hatari zinazojitokeza.”
“Watoto hawasubiri”
Miaka 20 baada ya ripoti ya kwanza ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya watoto, mafanikio katika kukabiliana na tatizo hilo bado yanategemea ushirikiano madhubuti wa kimataifa, amesema Bi. M’jid. Amehoji jinsi watoto wanavyoweza kwa mara nyingine kuiunganisha dunia ili kuhakikisha wanalindwa na ustawi wao unazingatiwa.
Ametangaza kuwa nchi 55 zimejiunga na Muungano wa Kimataifa wa Nchi Zinazoongoza Juhudi za Kukomesha Ukatili dhidi ya Watoto akiongeza kuwa “nchi nyingine zinaendelea kujiunga.”
Jukwaa hilo lililoanzishwa mwaka 2024 na linaloongozwa na nchi wanachama, linalenga kusaidia nchi kubadili ahadi za kisiasa kuwa hatua madhubuti kupitia mbinu mbalimbali, zikiwemo kujifunza kutoka kwa nchi nyingine, kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu na mbinu bora.
Bi. M’jid amehitimisha hotuba yake kwa kusisitiza kuwa watoto na vijana ni sehemu ya suluhisho la kukomesha ukatili wanaofanyiwa. “Watoto hawasubiri,” amesema. akiongeza kuwa “watoto tayari wanachukua hatua.”