Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Navi Pillay kutoka Afrika Kusini ndiye mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka 2026

Mwanamke wa Asia Kusini mwenye nywele fupi nyeusi na miwani isiyo na mirija amevaa koti jeupe na skafu ya rangi ya chungwa angavu huku akiangalia kamera.
UN Photo/Jean-Marc Ferré Navi Pillay, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mwaka 2026

Navi Pillay kutoka Afrika Kusini ndiye mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka 2026

Haki za binadamu
  • Ni kwa mchango wake wa kukuza amani na sheria za kimataifa
  • Amewahi kuwa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu
  • Alikuwa Jaji kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai Rwanda
  • Hivi sasa ni Jaji kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki, (ICJ)
Tweet URL

Kamati ya tuzo ya Nobel nchini Norway imemtangaza Navanethem “Navi” Pillay kuwa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2026 kutokana na mchango wake katika kukuza amani na sheria za kimataifa.

Akitoa tangazo hilo kutoka Oslo, mji mkuu wa Norway, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Jørgen Watne Frydnes amesema ushindi wa Pillay unatokana na mchango wake katika kuhakikisha wahusika wa uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kimbari wanawajibishwa.

“Leo hii Pillay ni jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ambako kwenye kesi ambayo Myanmar inatuhumiwa kwa mauaji ya kimbari,” amesema Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Tuzo ya Nobel.

Kamishna Mkuu wa OHCHR yfurahia ushindi wa Pillay

Kufuatia taarifa hizo, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu, (OHCHR) imeeleza kufurahishwa na taarifa za ushindi wa Bi. Pillay ambaye amewahi kuwa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu kuanzia mwaka 2008 hadi 2014, akiwa ndiye mwanamke wa pili na wa kwanza nje ya bara la Ulaya kushika wadhifa huo.

Volker Turk  amesema, “Leo tuna furaha sana kwa sababu ya mwenzetu. Kusema kwamba tuzo hii inamstahili kabisa ni kauli inayopunguza mno thamani ya mchango wake, hasa katika kipindi hiki ambapo haki za binadamu zinakabiliwa na mashambulizi katika nyanja nyingi, yakiwemo mashambulizi kutoka kwa watu wenye mamlaka makubwa, tuzo hii ina umuhimu wa kipekee.”

Bwana Turk ameendelea kusema kwamba, “Tuzo hii ni ya wote duniani wanaojitolea maisha yao kutetea haki za binadamu, mara nyingi wakihatarisha usalama wao wenyewe. Na kwa Navi Pillay kutunukiwa tuzo hii ni utambuzi na uthibitisho mpya kwamba haki za binadamu, utawala wa sheria, haki na uwajibikaji ni misingi muhimu ya kila kitu — amani, usalama na ustawi.”

Pillay na harakati dhidi ya ubaguzi wa rangi

Kamati hiyo ya tuzo ya amani ya Nobel imesema kuwa mshindi huyo wa tuzo mwaka huu alijipatia umaarufu kama mwanasheria aliyepinga ubaguzi na kutetea haki za binadamu, akiwemo hayati Nelson Mandela na wapiganiaji wengine dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Amekuwa Mwenyekiti pia wa Kamisheni Huru ya Umoja wa Mataifa inayochunguza ukiukaji wa haki za binadamu kwenye eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli ambapo katika ripoti waliyoitoa mwaka jana alieleza bayana kuwa Israeli inahusika na muaji ya kimbari Palestina.

Kuhusu Bi. Pillay na alichowahi kufanya

Pillay, ambaye anakuwa muafrika wa 13 kupokea tuzo hiyo ya amani ya Nobel, ni raia wa Afrika Kusini mwenye asili ya kabila la watamil kutoka India, na alizaliwa Durban, Afrika Kusini, wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi. 

Katika taaluma yake, amehudumu kama jaji katika Mahakama Kuu ya Afrika Kusini, Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ya Rwanda, (ICTR)  na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Kamati inaeleza bayana kuwa Bi. Pillay amewajibisha nchi na viongozi wa kitaifa kwa matendo yao na kuleta matumaini kwa waathiriwa wa vitendo vya ukatili na migogoro. 

Wakati akiwa jaji ICTR

Mathalani, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Rwanda ilipobaini kuwa ubakaji na ukatili wa kingono vinaweza kuchukuliwa kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, na pia kuwa sehemu ya mauaji ya kimbari, mchango wake akiwa jaji kwenye chombo hicho kati ya mwaka 1995 hadi 2003 ulikuwa na ushawishi mkubwa. 

“Katika kesi hiyo hiyo, Bi. Pillay alichangia kwa kiasi kikubwa katika hatua nyingine muhimu ya kisheria: kwa mara ya kwanza, mshtakiwa alikabiliwa na mashtaka ya uchochezi wa kutenda mauaji ya kimbari kwa msingi wa kueneza propaganda pekee," imesema Kamati hiyo.

Tuzo ya amani ya Nobel, inasisitiza umuhimu wa sheria, haki na ushirikiano wa kimataifa katika kujenga amani endelevu duniani na ilianza kutolewa mwaka 1901 ambapo Henry Dunant (muasisi wa Shirika la Msalaba Mwekundu) na Frédéric Passy (Mwanaharakati wa amani) walishinda kwa pamoja tuzo hiyo ya amani.

Kuhusu tuzo ya amani ya Nobel

  • Mshindi wa mwaka 2026: Navi Pillay, Mwanasheria kutoka Afrika Kusini na jaji wa mahakama ya kimataifa, ametunukiwa tuzo hiyo kwa juhudi zake za kuendeleza amani na sheria za kimataifa.
  • Mshindi wa mwaka 2025: María Corina Machado kutoka Venezuela, kwa mchango wake katika kuendeleza haki za kidemokrasia.
  • Chombo cha uteuzi: Kamati ya Nobel ya Norway yenye wajumbe watano, inayoteuliwa na Bunge la Norway
  • Mshindi hukabidhiwa tuzo mjini Oslo, Norway, tarehe 10 Desemba, siku ya kumbukumbu ya kifo cha Alfred Nobel.
  • Tuzo Inajumuisha medali ya dhahabu, cheti cha tuzo na zawadi ya fedha.
  • Asili ya tuzo: Ilianzishwa kupitia wosia wa mwanakemia na mvumbuzi kutoka Sweden, Alfred Nobel, na kutolewa kwa mara ya kwanza mwaka 1901.
  • Tangu mwaka 1901 hadi sasa 2026, tuzo ya Amani ya Nobel imetolewa mara 107 kwa washindi 144 (watu binafsi 113 na mashirika 31)
  • Kati ya washindi binafsi wanawake sasa ni 21 na wanaume 92.