Kwa nini ndege huzunguka angani kabla ya kutua? UN yalenga kupunguza ucheleweshaji na kufutwa kwa safari za ndege
Kusubiri kwa saa nyingi uwanja wa ndege baada ya safari kuchelewa, safari kufutwa ghafla, au ndege kutumia muda mrefu angani kutokana na msongamano ni miongoni mwa kero zinazowakabili wasafiri wa anga duniani.
Kero hizo zinaweza kuongezeka zaidi wakati wa hali mbaya ya hewa au kufungwa kwa baadhi ya maeneo ya anga. Kadhalika, kuongezeka kwa teknolojia mpya za usafiri wa anga na matarajio ya ongezeko kubwa la safari za ndege kunafanya usimamizi wa anga kuwa mgumu zaidi.
Lakini sasa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Anga, ICAO, linasema linaongeza kasi ya utekelezaji duniani wa mfumo wa Udhibiti wa Mtiririko wa Trafiki ya Angani Air Traffic Flow Management (ATFM), unaolenga kufanya safari za ndege ziwe za uhakika zaidi, kupunguza ucheleweshaji na kufutwa kwa safari, huku ukipunguza matumizi ya mafuta na uzalishaji wa hewa ukaa.
Mfumo wa ATFM
Kero: Ndege kuchelewa au kufutwa, Suluhu: Ushirikiano kabla ya kuruka
Kupitia ATFM, safari za ndege pamoja na mambo yanayoweza kuathiri uendeshaji wake zitaratibiwa kwa pamoja hata kuvuka mipaka ya nchi kabla ndege haijapaa.
Utaratibu huo uitwao kwa lugha ya kiingereza Airport Collaborative Decision Making (A-CDM), utawezesha mashirika ya ndege, viwanja vya ndege na waongoza ndege kubadilishana taarifa papo kwa papo na kufanya kwa pamoja maamuzi kuhusu wakati na namna ndege zitakavyopaa au kutua.
Uratibu huo pia unapanuliwa katika shughuli nyingine za uwanja wa ndege, ikiwemo mizigo, kujaza mafuta na usafirishaji wa abiria.
Kero: Msongamano angani, Suluhu: Njia za moja kwa moja
Badala ya marubani kulazimika kufuata njia zilizowekwa awali, ICAO inataka kupanua matumizi ya mfumo wa anga la njia huru yani “free route airspace”, utakaowawezesha kuchagua njia ya moja kwa moja na yenye ufanisi zaidi pale inapowezekana.
ICAO pia inataka nchi na viwanja vya ndege viwe na uwezo wa kupima kwa usahihi idadi ya ndege zinazoweza kuhudumiwa kwa usalama kwa wakati mmoja, pamoja na kuboresha umbali wa chini unaotakiwa kati ya ndege ili kuongeza uwezo wa anga bila kuhatarisha usalama.
Katibu Mkuu wa ICAO, Juan Carlos Salazar, amesema lengo ni kujenga mtandao wa kimataifa unaofanya safari kuwa za uhakika zaidi. “Kwa pamoja, tutajenga mtandao uliounganishwa kikamilifu wa usimamizi wa mtiririko wa ndege, utakaowezesha kila safari kuendeshwa kwa namna inayotabirika na yenye ufanisi, huku tukiimarisha usalama na uendelevu.”
Mazungumzo ya kimataifa yanayowakutanisha wadau kutoka maeneo mbalimbali ya uendeshaji wa anga yanatarajiwa kukamilika tarehe 9 Oktoba. Matokeo yake yatatumika katika kuboresha mwongozo wa ICAO kwa nchi wanachama na namna shirika hilo litakavyosaidia nchi kutekeleza maboresho hayo.
Kwa wasafiri, mafanikio ya mpango huo yanaweza kumaanisha jambo rahisi lakini muhimu: safari chache kuchelewa au kufutwa, na safari za anga kuwa za uhakika zaidi.
Mambo muhimu ya kufahamu
Baadhi ya nchi tayari zinatumia mfumo huu, lakini manufaa yake yanabaki kuwa madogo pale mifumo ya kitaifa inaposhindwa kuwasiliana. Baada ya mazungumzo ya siku tano yaliyoitishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), mjini Montreal, Kanada, serikali na wadau wa sekta ya usafiri wa anga waliunga mkono kuharakishwa kwa matumizi ya mfumo huo duniani.
Kwa abiria, hatua hii inatarajiwa kumaanisha kupata taarifa mapema kuhusu kufutwa kwa safari na ucheleweshaji, pamoja na kurejesha shughuli katika hali ya kawaida kwa haraka zaidi matatizo yanapotokea.
“Watu wanapofika uwanja wa ndege, wanasubiri siku nzima na hakuna anayewaeleza kinachoendelea, hilo husababisha matatizo makubwa,” amesema Salazar.
Ameeleza kuwa athari za usumbufu mmoja huendelea kuongezeka. Tatizo linalodumu kwa saa moja au siku nzima linaweza kuathiri safari zote zinazofuata zilizopangwa, huku mfumo wa sasa ukichelewa kurejea katika hali ya kawaida.
Muda, fedha na mafuta
Manufaa ya mfumo huu tayari yanaonekana. Katika majaribio yaliyosaidiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), katika bara la Amerika mwaka 2026, uratibu wa pamoja uliokoa zaidi ya dakika 265,000 za muda wa kuruka, sawa na takribani saa 4,400, na zaidi ya dola milioni 38.9.
Majaribio hayo pia yaliokoa takribani tani 13,330 za mafuta na kuzuia uzalishaji wa tani 42,160 za hewa ukaa, hatua inayochangia lengo la kufikia uzalishaji sifuri wa hewa ukaa kutokana na usafiri wa anga wa kimataifa ifikapo mwaka 2050.
Barani Ulaya, mpango wa EUROCONTROL wa kutabiri athari za hali ya hewa na msongamano wa anga uliepuka takribani dakika milioni 3.1 za ucheleweshaji kati ya Mei na Agosti 2026. Mpango huo uliokoa wastani wa dola milioni 448 na kuufanya mtandao wa usafiri wa anga kuwa thabiti zaidi kwa asilimia 14 katika siku zenye msongamano mkubwa zaidi.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Anga (ICAO),, mashirika ya ndege yalisafirisha karibu abiria bilioni tano kupitia safari milioni 38 mwaka 2025.
Changamoto kubwa ni kushirikishana taarifa
Brazil na Colombia zimekuwa zikitumia mifumo hiyo kwa miaka kadhaa, amesema Salazar, lakini kwa kiasi kikubwa katika ngazi ya kitaifa, ilhali safari za kimataifa hupitia anga za nchi nyingi.
“Teknolojia pekee haitoshi,” alisema. Taarifa zinahitaji kushirikishwa, lakini mara nyingi hilo halifanyiki, wakati mwingine kutokana na ukosefu wa utayari na wakati mwingine kwa kukosekana kwa uwezo wa kuzisambaza kwa wakati halisi.
“Ndege inayosafiri kutoka Ulaya kwenda Australia au New Zealand hupitia maeneo manne au matano ya anga katika mabara tofauti. Hilo linahitaji uratibu wa hali ya juu ambao haupo leo,” alisema. “Hakuna nchi wala eneo linaloweza kusimamia jambo hili peke yake.”
(ICAO), yenye nchi wanachama 193, huweka viwango vya pamoja na kutoa msaada wa kiufundi ili nchi ziweze kuratibu safari bila kujali rasilimali walizonazo. Kanuni mpya za kimataifa kuhusu usimamizi wa mtiririko wa trafiki ya anga zinatarajiwa Novemba 2030, huku warsha za kikanda zikipangwa kufanyika mwaka 2027.
Shinikizo linaongezeka huku (ICAO), ikikadiria kuwa idadi ya abiria wa usafiri wa anga inaweza kufikia bilioni 12.4 ifikapo mwaka 2050.