Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maabara ya uchunguzi wa kisayansi ya wanyamapori na misitu nchini Uganda yasaidia kudhibiti uhalifu

Tembo wawili wa Kiafrika wanagusa mikoko na pembe za ndovu katika mazingira ya savanna.
© Adobe/Ward Poppe Tembo wawili wa Kiafrika wakikutana katika hifadhi ya wanyamapori Queen Elizabeth National nchini Uganda.

Maabara ya uchunguzi wa kisayansi ya wanyamapori na misitu nchini Uganda yasaidia kudhibiti uhalifu

Na Isaiah Steinberg
Sheria na Kuzuia Uhalifu

Kifurushi kiliondoka Entebbe nchini Uganda kuelekea Cairo, Misri, kikiwa na kilo 10 za vipande vidogo vilivyoweza kuwa mifupa ya kawaida au pembe za ndovu. Kwa kuviona kwa macho pekee, haikuwa rahisi kujua.

Wapelelezi wa Polisi ya Uganda na wachunguzi wa Mamlaka ya Wanyamapori Uganda walipokinasa kifurushi hicho Januari mwaka 2025, walihitaji zaidi ya tuhuma ili kumchunguza mtu aliyekituma.

Sampuli zilipelekwa katika Maabara ya Uchunguzi wa Kisayansi wa Wanyamapori na Mbao ya Uganda mjini Entebbe, ambayo imekuwa ikipokea msaada kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) tangu mwaka 2019.

Wanasayansi walibaini alama maalum zinazohusishwa na pembe za ndovu, huku vipimo vya vinasaba (DNA) vikithibitisha baadaye kuwa vipande hivyo vilitokana na mnyama tembo.

Fundi wa maabara wa kiume mweusi aliyevaa koti la kijani, barakoa ya kinga na glavu za bluu akishughulikia vichupa vya sampuli kwenye benchi la maabara lenye kifaa cha kusukuma maji na usawa wa kidijitali.
© Umoja wa Ulaya Fundi wa maabara anafanya mtihani katika Maabara ya Upelelezi wa Wanyamapori na Mbao ya Uganda huko Entebbe.

Kutoka kifurushi cha kutatanisha hadi hukumu ya miaka 15

Miezi miwili baadaye, polisi walimkamata mtu aliyetuma kifurushi hicho. Walipopekua makazi yake, wachunguzi walipata pembe nyingine za ndovu pamoja na pembe za ngiri.

Mtu huyo alishtakiwa kwa kujaribu kufanya biashara haramu ya bidhaa za wanyamapori na kuzimiliki kinyume cha sheria. Alihukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani au kulipa faini ya shilingi milioni 140 za Uganda, sawa na zaidi ya dola 35,000 za Marekani.

Kwa Meneja wa maabara hiyo, Patrick Chiyo, kesi hiyo inaonesha umuhimu wa ushahidi wa kisayansi katika mapambano dhidi ya uhalifu wa wanyamapori, hasa pale ambapo wahalifu wamekata au kubadilisha sehemu za wanyama na kuondoa alama zinazoweza kusaidia kuzitambua.

“Majangili wanaondoa alama zinazosaidia kutambua mizoga ya wanyamapori ili wasigundulike,” anasema Chiyo.

Anaongeza kuwa ripoti za DNA zinazidi kuhitajika katika mahakama inayoshughulikia makosa ya wanyamapori nchini Uganda na kwamba washukiwa wanazidi kukiri makosa kutokana na ushahidi unaotolewa na maabara hiyo.

DNA yafichua kile ambacho macho hayawezi kuona

Kazi ya maabara hiyo mara nyingi huanzia mbali na Entebbe. Maafisa wanaweza kukamata magunia yenye vipande vya pembe za ndovu, magamba ya Kakakuona au nyama ya wanyamapori iliyokaushwa kwa moshi.

Kwa sababu baadhi ya mizigo hiyo huwa mikubwa, wataalamu huchukua sampuli katika vituo vya polisi huku kila hatua ikirekodiwa. Ushahidi hupigwa picha kabla ya kufunguliwa na tena baada ya sampuli kuchukuliwa.

Ushahidi halisi hurejeshwa chini ya ulinzi wa polisi, huku sampuli zilizofungwa zikisafirishwa hadi maabara kwa uchunguzi.

Mchakato huo unaweza kuchukua muda, lakini Chiyo anasema unaweza kuwa muhimu katika kesi ambazo mabaki ya wanyama hayajakamilika, yamebadilishwa au ni vigumu kuyatambua.

Mwaka 2023, kwa mfano, Chiyo alisafiri kwa takribani saa nne kuelekea kaskazini mwa Kampala baada ya mshukiwa kukamatwa akiwa na ngozi sita, vichwa sita, magunia mawili ya nyama, miguu 24 yenye kwato na kijusi kilichodhaniwa kuwa cha mnyama pori.

Ngozi hizo zilionekana kuwa za Swala, lakini haikuwezekana kuthibitisha aina yake kwa kuzitazama pekee.

Chiyo na timu yake walichukua sampuli na kutumia vipimo vya vinasaba (DNA), vilivyothibitisha kuwa zilitokana na aina ya Swala, bushbuck. Chiyo baadaye alitoa ushahidi mahakamani na mshukiwa akahukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani.

Chiyo anasema baadhi ya watu huwawinda wanyama kwa ajili ya chakula cha familia, huku wengine wakiwaua kwa manufaa ya kibiashara. Biashara hiyo, amesema, ndiyo tishio kubwa zaidi kwa uhifadhi wa wanyamapori.

Uganda kitovu cha mitandao ya biashara haramu ya wanyamapori

Ushahidi kutoka Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2024 kuhusu Uhalifu wa Wanyamapori unaonesha kuwa Uganda ni kitovu muhimu cha mitandao ya uhalifu uliopangwa inayojihusisha na biashara haramu ya wanyamapori, hususan pembe za ndovu na kakakuona.

Kwa mujibu wa Bashir Hangi wa Mamlaka ya Wanyamapori Uganda, tembo, kakakuona, jamii za nyani na baadhi ya aina za ndege ni miongoni mwa wanyama wanaokabiliwa zaidi na ujangili na biashara haramu nchini humo.

Ingawa Uganda haina soko la ndani la pembe za ndovu na magamba ya kakakuona, Chiyo amesema kuna soko kubwa la nyama ya wanyamapori waliowindwa kinyume cha sheria. Mamlaka zimewahi kukabiliana na kesi zilizohusisha karibu tani moja ya nyama hiyo.

Gari la safari linaendesha gari kwenye njia ya vumbi kupitia msitu wa mvua wenye ukungu na mnene wa kijani huko Bwindi, Uganda.
© Adobe/Pawel Gari la Utalii au Safari linapita katika Msitu wa Bwindi Impenetrable nchini Uganda.

Uhalifu hauishii kwa anayemuua mnyama

Hangi anasema uhalifu dhidi ya wanyamapori unachochewa na mitandao ya uhalifu uliopangwa pamoja na changamoto za kiuchumi zinazokabili baadhi ya jamii.

Athari zake pia huwakumba watu wanaoishi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa, ambako migogoro kati ya binadamu na wanyamapori pamoja na wanyama kuharibu mazao imekuwa changamoto.

Kwa Chiyo, utekelezaji wa sheria haupaswi kumlenga tu mtu anayemuua au kumkamata mnyama, bali pia wale walio juu katika mitandao ya uhalifu ambao hunufaika na biashara hiyo.

Hata hivyo, anasema mfumo wa haki jinai pekee hautoshi. Njia mbadala za kujipatia kipato zinahitajika sambamba na doria za kuzuia ujangili na utekelezaji wa sheria.

“Mnyama aliye hai ana manufaa zaidi kwa watu wengi kuliko mnyama aliyekufa,” anasema Chiyo.

Kutoka pembe za ndovu hadi mbao

Mwezi Aprili mwaka huu 2026, Maabara ya Uchunguzi wa Kisayansi wa Wanyamapori na Mbao ya Uganda ilifunguliwa kwa msaada wa Denmark, Muungano wa Ulaya na UNODC ili kuimarisha juhudi za kukabiliana na biashara haramu ya pembe za ndovu.

Maabara hiyo inaendeleza kazi ya kituo cha kitaifa cha mafunzo na msaada wa kiufundi kilichoanzishwa mwaka 2019 kama maabara ya majaribio ya uchunguzi wa wanyamapori kupitia ushirikiano kati ya UNODC, TRACE Wildlife Forensics Network na Serikali ya Uganda.

Kituo hicho cha awali kimesaidia mamia ya uchunguzi na kesi zinazohusiana na biashara haramu ya wanyamapori.

Sasa maabara hiyo imepanua shughuli zake na kuanza uchunguzi wa kisayansi wa mbao wakati Uganda ikikabiliana na athari za ukataji na biashara haramu ya miti.

Kwa mujibu wa mamlaka za Uganda, eneo la nchi hiyo lililofunikwa na misitu limepungua kutoka asilimia 24 mwaka 1990 hadi takribani asilimia 13 mwaka 2025, huku biashara haramu ya mbao ikitajwa kuwa sababu kubwa ya kupungua huko.

Mbao zaleta changamoto tofauti

Chiyo anasema kesi za mbao ni ngumu zaidi kuliko zile zinazohusisha wanyamapori kwa sababu uvunaji wa miti pia unaruhusiwa na kudhibitiwa kisheria katika mazingira mbalimbali.

Hivyo, kubaini iwapo kipande cha mbao kilipatikana kinyume cha sheria kunaweza kuhitaji hatua zaidi za uchunguzi kuliko kutambua bidhaa zinazotokana na wanyama.

Maabara hiyo ndiyo inaanza kushughulikia kesi za mbao na hadi sasa haijapata ushahidi unaoonesha kuwa mbao haramu zinasafirishwa kupitia mitandao au njia zilezile zinazotumiwa kusafirisha bidhaa haramu za wanyamapori.

Mikono iliyovaa glavu za bluu za nitrile hufunga sampuli ndogo ya silinda kwa kutumia koleo linalofungika huku sehemu ya kuchimba visima ikitoboa ndani yake, na kutoa vumbi dogo kwenye uso mweupe.
© Umoja wa Ulaya Sampuli inajaribiwa katika Maabara ya Uchunguzi wa Wanyamapori na Mbao ya Uganda.

Sayansi katika kulinda urithi wa Uganda

Kwa Gladys Kamasanyu, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Wanyamapori Uganda, maabara hiyo ni muhimu katika mfumo wa haki jinai kwa sababu inatoa ushahidi huru uliothibitishwa kisayansi unaoweza kusaidia mahakama kuwawajibisha wahalifu.

Akizungumza na UNODC mwezi Aprili, Kamasanyu alisema ushahidi huo unaimarisha uwezo wa mahakama kulinda urithi wa asili wa Uganda kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Chiyo naye anatamani kuona katika miaka ijayo Uganda ikiwa na maabara endelevu ya uchunguzi wa wanyamapori na mbao inayoungwa mkono kikamilifu na serikali.

Kwa sasa, kila sampuli inayochunguzwa na kila matokeo ya vipimo vya vinasaba (DNA) yanayothibitishwa yanasaidia kuziba pengo kati ya tuhuma za biashara haramu ya wanyamapori na ushahidi unaoweza kufikisha kesi mahakamani.

Kwa Chiyo, kuimarisha mfumo wa haki kupitia uchunguzi wa kisayansi wa wanyamapori na mbao ni nguzo muhimu katika kulinda mazingira, huku haki ya mazingira ikiwa na manufaa pia kwa watu walio katika mazingira hatarishi zaidi.