Kutoka mkimbizi hadi balozi wa UNHCR: Toussaint Chiza, sauti ya matumaini toka DRC
Akiwa mtoto mdogo, Toussaint Chiza alikimbia vita nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), bila kujua alikokuwa akienda wala wazazi wake walikuwa wap. Walipotezana vita ilipozuka wakielekea kwenye kambi ya wakimbizi nchini Uganda.
Leo, miaka kadhaa baadaye, Chiza ni mwanamuziki anayefahamika nchini Sweden na Balozi wa Mwema wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) wa Sweden.
Safari yake kutoka mtoto mkimbizi hadi msanii aliyewakilisha Sweden katika mashindano makubwa ya muziki barani Ulaya ni simulizi ya machungu, kupona, matumaini na nguvu ya kupewa fursa.
Lakini nyuma ya mafanikio hayo kuna kumbukumbu za majonzi za utotoni alizobeba kwa miaka mingi, kumbukumbu za vita, kutengana na familia na maisha ya ukimbizi.
“Sikujua tunakwenda wapi”
Chiza anakumbuka siku aliyoondoka DRC akiwa mtoto mdogo wa umri wa miaka mitano tu. Gari lilisafiri gizani, huku yeye akiwa hajui kinachoendelea wala kama angewaona tena wazazi wake aliopotezana nao.
“Nilikuwa naogopa sana. Sikujua kama tunakwenda wapi. Sikujua mama yuko wapi, wala baba yuko wapi” anakumbuka.
Alikumbuka tu gari lililosafiri gizani na watu waliowakaribisha baada ya kufika mahali salama kwenye kambi ya wakimbizi inayoendeshwa na UNHCR.
“Walisema, ‘Karibu, tutakusaidia. Walitupatia chakula kidogo, nguo… lakini siku zote nilikuwa nauliza, mama yuko wapi? Baba yuko wapi?”
Safari hiyo hatimaye ilimfikisha katika kambi ya wakimbizi nchini Uganda, ambako aliishi kwa takribani miaka mitatu.
Lakini akiwa huko, swali kuhusu wazazi wake lilibaki bila jawabu.
Kambi ya wakimbizi ikawa chimbuko la muziki
Ni katika mazingira hayo ya ukimbizi ambako Chiza alianza kugundua nguvu ya muziki.
Kanisani, alikutana na watu waliokuwa wakiimba na kumtukuza Mungu. Hatua kwa hatua, yeye pia akaanza kuimba.
“Muziki unanisaidia kusahau kila kitu,kusahau magumu na machungu niliyopitia” anasema.
Kwa Chiza, kuimba hakukuwa tu burudani. Kulikuwa njia ya kukabiliana na maumivu na kupata nafasi ya kuishi katika wakati uliopo.
“Maisha yanaweza kuwa mabaya kwa sababu ya vita, lakini tunaimba tu… na ninapoimba inanifanya kusahau matatizo yote na kuwa katika wakati huo.”
Muziki ukawa sehemu ya maisha yake, hata wakati ambapo habari kuhusu wazazi wake ilikuwa ikizidi kuwa nzito.
“Nilizani wote Mama na baba walikufa”
Baada ya miaka mitatu Uganda, Chiza alihamishiwa Sweden kupitia mpango wa Shirika la UNHCR wa kuwapeleka wakimbizi katika nchi ya tatu.
Alifika katika nchi hiyo akiwa mtoto aliyebeba kumbukumbu za vita na ukimbizi na habari ambayo angebeba maisha yake yote: wazazi wake walikuwa wamefariki dunia.
“Miaka mitatu yote nilijua mama yangu na baba yangu walikufa,” anakumbuka. Lakini sasa amebaini baba yake mzazi yuko hai ila mama yake alipoteza maisha vitani.
Akiwa Sweden, alianza shule na kuendelea na muziki.
Katika kipindi hicho, kuimba kulimpa faraja ambayo haikuwa rahisi kuipata mahali pengine.
“Unapoimba, unasahau yote. Unakuwa katika wakati huo,” anasema.
Kwa mtoto aliyekuwa amepoteza familia yake na makazi yake, muziki ukawa zaidi ya sauti, ukawa sehemu ya safari ya kujenga maisha mapya.
Kutoka ukimbizi hadi jukwaa la Eurovision
Miaka baadaye, safari hiyo ilimpeleka Chiza kwenye moja ya majukwaa makubwa ya muziki barani Ulaya, Eurovision ambako aliiwakilisha Sweden.
Kwa mtu ambaye aliwahi kukimbia vita akiwa mtoto, tukio hilo lilikuwa ishara ya jinsi maisha yanavyoweza kubadilika pale fursa inapopatikana.
“Ilikuwa ni jambo kubwa sana, kwangu” anasema kuhusu fursa hiyo.
Lakini ujumbe wake unaenda zaidi ya mafanikio yake binafsi. “Ilinipa matumaini makubwa kwamba kila kitu kinawezekana.”
Chiza anasema alikutana na watu nchini Sweden waliomsaidia kujifunza lugha na kumkaribisha katika jamii.
“Walisema, ujifunze lugha yetu. Walinionesha kuwa ni muhimu na kwamba wanampenda mtu kama mimi.”
Kwa kijana aliyefika Sweden akiwa mkimbizi, kukubalika na kupewa nafasi kulimsaidia kujenga maisha mapya.
“Usisahau ulikotoka”
Leo, Chiza anatumia hadithi yake kuwapa moyo watoto na vijana ambao, kama yeye, wamelazimika kukimbia vita makwao.
Anawaambia wakimbizi wasiache ndoto zao kwa sababu ya mazingira waliyomo leo.
“Usisahau kwenye matatizo ulikotoka. Usisahau jina yako na masomo,” anasema.
Anakumbuka kwamba alipokuwa mtoto hakujua Kiingereza na hakuwa na uhakika wa maisha yake ya kesho. Anawashauri kwamba
“Hatufahamu ya kesho. Tunajua tu leo. Kama unajua jinsi ya kuimba, anza kuimba. Kama unajua sayansi, endelea na masomo.”
Kwa Chiza, ujumbe huo ni rahisi lakini una nguvu: mazingira yanaweza kubadilika, lakini kipaji, elimu na matumaini vinaweza kuwa daraja la kuelekea maisha mapya.
“Usiwafukuze wakimbizi”
Kama Balozi wa Mwema wa UNHCR, Chiza sasa anataka viongozi na jamii duniani waone zaidi ya neno “mkimbizi”.
Anaamini wakimbizi si watu wanaohitaji msaada pekee, bali pia wana uwezo wa kuchangia jamii zinazowapokea iwapo watapewa fursa.
“Usiwafukuze wakimbizi,” anawaambia viongozi wa dunia.
“Wapatie fursa. Wape nafasi ya kusoma, kufanya kazi na kutumia vipaji vyao. Yote watakayofanya yatakuwa na faida na yataleta maendeleo.”
Maneno hayo yanatokana na uzoefu wake mwenyewe.
Mtoto aliyewahi kukimbia vita bila kujua wazazi wake walikuwa wapi, aliyeishi miaka katika kambi ya wakimbizi na baadaye kupoteza mzazi wake, sasa anatumia sauti yake kuzungumzia matumaini ya mamilioni ya watu waliolazimika kuacha makazi yao kutokana na vita na migogoro.
Na kwa Chiza, ujumbe wake kwao ni mmoja, Usikate tamaa. Kesho inaweza kuwa tofauti na leo.