Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Magonjwa ya mishipa ya moyo yaendelea kuwa sababu kuu ya vifo duniani - WHO

Mpishi Mkorea aliyevaa aproni nyekundu anakaanga chakula kwenye pipa kubwa la chuma kwenye kibanda cha chakula cha barabarani.
Unsplash/Markus Winkler Vyakula vyakutumia mafuta ya kukaanga vinakadiriwa kusababisha vifo 500,000 kwa mwaka kutokana na ugonjwa wa moyo.

Magonjwa ya mishipa ya moyo yaendelea kuwa sababu kuu ya vifo duniani - WHO

Afya

Licha ya kwamba hali ya afya duniani inaendelea kubadilika, watu wakiishi kwa muda mrefu zaidi baada ya janga la COVID-19, magonjwa ya mishipa ya moyo yaliendelea  kuongoza kuwa chanzo cha vifo duniani kote mwaka 2023 kama ilivyokuwa mwaka 2022.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti  iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani kuhusu Makadirio ya Afya Duniani, (GHE) yakitaja magonjwa kumi yanayoongoza kwa kusababisha vifo, halikadhalika magonjwa kumi yanayosababisha watu kubadili mwenendo wa maisha yao.

Magonjwa kumi yanayoongoza kwa kusababisha vifo ni magonjwa ya mishipa ya moyo, kiharusi,ugonjwa wa mapafu, maambukizi katika njia ya hewa, ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu, kisukari, saratani ya koo na mapafu, shinikizo la damu, magonjwa ya figo na kuhara.

Magonjwa yasiyoambukiza (NCDs)

Ripoti hiyo inasema magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) yanachangia idadi kubwa ya vifo huku magonjwa kama vile kisukari, magonjwa ya afya ya akili na matatizo yanayohusiana na matumizi ya dawa za kulevya yakichangia kuongezeka na kubadilika kwa mzigo wa magonjwa.

Ripoti hiyo inaangalia jinsi afya ilivyobadilika katika nchi na maeneo mbalimbali kati ya mwaka 2000 na 2023, ikiwemo mwenendo wa umri wa kuishi, sababu za vifo na mzigo wa magonjwa.

Meza imewekwa na sahani mbalimbali za chakula, ikiwa ni pamoja na bakuli kubwa la bluu la machungwa yaliyokatwakatwa na sahani ndogo ya vipande vya tikiti maji.
PAHO/WHO kula vyakula vya afya kunapunguza kupata kwa aina ya 2 ya kisukari.

Afya duniani inarejea, lakini si mafanikio yote yamerudi

Wastani wa umri wa kuishi duniani ulifikia miaka 73.3 mwaka 2023, karibu na miaka 73.4 iliyorekodiwa mwaka 2019. Umri wa kuishi ukiwa na afya njema umeongezeka kwa kasi ndogo zaidi, na kufikia miaka 62.8 mwaka 2023, ambao bado ni miaka 0.4 chini ya kiwango cha mwaka 2019.

Magonjwa yasiyoambukiza yalisababisha asilimia 74ya vifo duniani mwaka 2023, ikilinganishwa na asilimia 58 mwaka 2000. 

“Magonjwa yasiyoambukiza yalikuwa sababu za vifo katika nafasi nane kati ya kumi za sababu kuu za vifo duniani mwaka 2023,” imesema taarifa iliyotolewa leo Geneva, Uswisi na WHO.

Magonjwa na kiwango cha kipato

Mabadiliko haya yanaonekana zaidi katika maeneo ya viwango vyote vya kipato kwani mwaka 2023, kwa mara ya kwanza, magonjwa ya kuambukiza yalisababisha chini ya nusu ya vifo vyote katika nchi zenye kipato cha chini, jambo linaloashiria hatua nyingine katika mabadiliko ya mifumo ya magonjwa duniani.

“Kuishi muda mrefu zaidi ni mojawapo ya mafanikio makubwa ya afya ya umma,” amesema Dkt. Alain Labrique, Mkurugenzi wa Idara ya WHO ya Takwimu, Afya ya Kidijitali, Uchambuzi na Akili Mnemba. “Changamoto inayofuata ni kuhakikisha kwamba miaka hiyo ya ziada inaishiwa katika hali nzuri ya afya, huku mifumo ya afya ikiwa na uwezo wa kukabiliana na mahitaji yanayobadilika ya watu.”

Mtazamo kutoka nyuma wa mzee mwenye nywele za kijivu ameketi kwenye kiti cha magurudumu cha rangi ya hudhurungi kwenye njia ya mawe ya mawe.
Unsplash/ Steven HWG Ingawa shida ya akili ndiyo chanzo kikuu cha vifo duniani, utafiti wake unachangia chini ya 1.5% ya matokeo yote ya utafiti wa afya.

Magonjwa yaliyoongoza kwa vifo

  • Magonjwa ya mishipa ya moyo yanayosababishwa na kuziba kwa mishipa ya moyo yalisababisha takribani vifo milioni 9.5.
  • Hatari ya kufa kutokana na kisukari imeongezeka kwa kiasi kikubwa tangu mwaka 2000, hasa katika nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia. 
  • Ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu (Alzheimer) na aina nyingine za magonjwa ya akili pia vimeongezeka kwa kasi. 
  • Matatizo yanayohusiana na matumizi ya dawa za kulevya 

Kwa ujumla, makadirio haya yanaonesha hali ya afya duniani ambayo kwa upande mmoja inaendelea kupona kutokana na janga, na kwa upande mwingine inaendelea kubadilika.

“Thamani ya makadirio haya haipo katika nambari zenyewe pekee,” amesema Dkt. Labrique akiongeza kuwa,  “kwa kuonesha jinsi sababu za vifo na mzigo wa magonjwa zinavyobadilika kadiri muda unavyopita na katika makundi mbalimbali ya watu, makadirio haya yanaipa nchi ushahidi wa kusaidia kuunda sera na vipaumbele vya afya."

Ameongeza kuwa makadirio hayo pia yanasaidia WHO katika kuunga mkono nchi kujenga miundombinu imara na muhimu ya kidijitali na data, huku ikiimarisha uwezo wa kitaifa na ngazi za chini za kitaifa wa kuchanganua takwimu za afya na kutoa maarifa kwa wakati ambayo yanaweza kuchukuliwa hatua.

Soma ripoti nzima hapa.