Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo wa Mashariki ya Kati wakwamisha mlo kwa wanawake milioni 11.7 kwenye nchi 28 zikiwemo za Afrika – UN Women

Mwanamume na mwanamke mzee wa Nigeria wakisukuma mkokoteni uliojaa mgao wa chakula cha msaada katika kituo cha usambazaji WFP huko Dikwa, Jimbo la Borno, Nigeria.
© WFP/Arete/Khalid Hamza Mwanamke akipokea msaada wa chakula katika kituo cha usambazaji WFP huko Borno Stage, Nigeria.

Mzozo wa Mashariki ya Kati wakwamisha mlo kwa wanawake milioni 11.7 kwenye nchi 28 zikiwemo za Afrika – UN Women

Amani na Usalama
  • Bei za vyakula zimeongezeka
  • Wanawake wanashindwa kupata mlo wakijali wanafamilia
  • Nchi za Afrika ni pamoja na Burkina Faso na Ethiopia

Takriban wanawake na wasichana wengine milioni 11.7 katika nchi 28 wanaweza kukabiliwa na ukosefu wa chakula ifikapo mwishoni  mwa mwaka huu kutokana na kuongezeka kwa mzozo Mashariki ya Kati, limeonya shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake, UN Women.

Akiwasilisha uchambuzi wa shirika hilo katika mataifa hayo mbele ya waandishi wa habari hii leo huko Geneva, Uswisi, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, Nyaradzayi Gumbonzvanda, amesema makadirio hayo ni ya hali inayoweza kutokea, na si utabiri, na kwamba idadi hiyo ni nyongeza kwa wanawake na wasichana milioni 208 waliokuwa tayari wanakadiriwa kutokuwa na uhakika wa mlo au wana utapiamlo katika nchi hizo.

Kwa mujibu wa uchambuzi huo, usumbufu wa usafirishaji kwa njia ya meli kupitia Mlango wa Bahari wa Hormuz umeongeza gharama za nishati, mbolea na usafiri, hali inapandisha bei za chakula na kuongeza shinikizo kwa kaya na shughuli za kibinadamu.

Wanawake hula kidogo na hula mwisho

Gumbonzvanda amesema, “uzoefu wa migogoro iliyopita unaonesha kuwa chakula kinapopungua, wanawake mara nyingi hupunguza kiasi wanachokula au huruka milo ili watoto na wanafamilia wengine wapate chakula.”

Nchini Afghanistan, wanawake na wasichana wanakadiriwa kuwa asilimia 60 ya watu wanaoweza kukabiliwa na ukosefu wa chakula, huku Sudan Kusini ikikabiliwa na hatari kubwa kwa uwiano wa idadi ya wanawake—takriban mwanamke au msichana mmoja kati ya saba.

N. Gumbonzvanda, aliyetambuliwa kwa jina la Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, akizungumza kwenye jukwaa mbele ya mandhari ya bluu UMOJA WA MATAIFA Geneva.
UN WebTV Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, Nyaradzayi Gumbonzvanda, akiwasilisha kwa waandishi wa habari huko Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi, uchambuzi kuhusu athari za kuongezeka kwa mzozo huko Mashariki ya Kati kwa uhakika wa kupata chakula miongoni mwa wanawake na wasichana.

Wanawake wasio na ajira

Nchini Misri, Iraq, Palestina, Sudan na Syria, zaidi ya asilimia 80 ya wanawake hawana ajira, ilhali nchini Afghanistan na Yemen, kiwango hicho kinafikia takribani asilimia 95.

“Miongoni mwa wanawake walioajiriwa, wengi wako katika ajira zilizo hatarini na zisizo na uhakika. Hali hii inawahusu zaidi ya asilimia 80 ya wanawake nchini Afghanistan, Burkina Faso, Ethiopia, Haiti, Mali na Sudan Kusini,” amesema Naibu Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UN Women.

Kutokana na hali hiyo, amesema, mwanamke asiye na akaunti ya benki au fedha kwenye simu yake anaweza pia kushindwa kuweka akiba, kupokea msaada au kutuma na kupokea fedha wakati bei za vyakula zinapopanda.

UN Women yataka hatua za haraka

UN Women inapendekeza kuunganisha msaada wa chakula na fedha na huduma za lishe, ulinzi, ajira na kilimo. Wanawake pia wanapaswa kupata ardhi, mikopo na rasilimali za uzalishaji.

Shirika hilo linasisitiza pia ukusanyaji wa takwimu zinazoonesha nani ndani ya kaya anakula kidogo, anayepoteza kipato na anayebeba mzigo mkubwa wa kazi za bila malipo.

Gumbonzvanda amehitimisha akisema kuwa, “hilo ndilo jawabu, lakini muhimu zaidi, ili kukomesha mateso ya wanawake na wasichana, tunahitaji amani na usalama. UN Women inatoa wito wa kupunguzwa kwa mvutano na kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa.”

Ameunga mkono  wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa pande zote zinazohusika kufanya kazi kuelekea suluhu za kidiplomasia zitakazokuza amani na usalama wa kikanda na kimataifa.

Mataifa 28 yaliyohusika kwenye uchambuzi huu ni:

Afghanistan, Armenia, Bangladesh, Burkina Faso, Misri, Ethiopia, Haiti, India, Indonesia, Iraq, Jordan, Lebanon, Mali, Moldova, Myanmar, Nigeria, Pakistan, Palestina, Ufilipino, Somalia, Sudan Kusini, Sri Lanka, Sudan, Syria, Thailand, Ukraine, Viet Nam and Yemen.