UN yatoa dola milioni 160 kusaidia wahitaji kwenye maeneo 12 yenye migogoro ya kibinadamu
UN yatoa dola milioni 160 kusaidia wahitaji kwenye maeneo 12 yenye migogoro ya kibinadamu
- Afrika yapokea kiwango kikubwa zaidi
- Sudan, Somalia na Sudan Kusini zapatiwa kiwango kikubwa
- Dola milioni 10 kuelekezwa kwa watu wenye ulemavu
Umoja wa Mataifa umetenga dola milioni 160 kutoka Mfuko Mkuu wa Kukabiliana na Dharura (CERF) kusaidia shughuli za kuokoa maisha katika maeneo 12 yenye migogoro kibinadamu duniani ambayo haijapatiwa ufadhili wa kutosha.
Taarifa iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi na New York, Marekani imesema fedha hizo ni sehemu ya juhudi za kuwafikia watu milioni 87 wenye mahitaji makubwa zaidi ya kibinadamu mwaka huu.
Mchanganuo unaonesha kuwa kiwango kikubwa cha fedha hizo kimeelekezwa barani Afrika ambako kuna mizozo mingi zaidi.
Mgawanyo wa fedha
Kati ya fedha hizo, dola milioni 150 zitaelekezwa katika misaada ya kuokoa maisha kama ifuatavyo:
- Afghanistan $18 milioni
- Palestina $18 milioni
- Yemeni $18 milioni.
- Sudan: $16 milioni
- Somalia: $16 milioni
- Sudan Kusini: $15 milioni
- Burkina Faso: $10 milioni
- Mali: $10 milioni
- Niger: $10 milioni
- Chad: $9 milioni
- Cameroon: $6 milioni
- Cuba $4 milioni
Ulemavu waangaziwa
Dola milioni 10 zimetengwa mahsusi kushughulikia mahitaji ya watu wenye ulemavu na kufanya misaada ya kibinadamu iwe jumuishi zaidi.
Taarifa imesema Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia watu wenye ulemavu duniani, (UN Global Disability Fund) wenyewe utaongeza hadi dola milioni 4 za ufadhili na msaada wa kitaalamu.
Kauli ya Mkuu wa OCHA
Tom Fletcher, ambaye ni Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Misaada ya Dhadura, OCHA, amenukuliwa kwenye taarifa hiyo akisema, “fedha hizo zitasaidia kuwafikia watu ambao huenda wakaachwa nyuma.”
Hata hivyo ametoa wito kwa viongozi kuwezesha upatikanaji wa misaada.
Mgao huo umefikisha jumla ya fedha zilizotolewa na CERF mwaka 2026 hadi kufikia dola milioni 483.
Kuhusu CERF na uamuzi wa utoaji wa fedha
CERF hupata michango ya fedha kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, waangalizi, mashirika ya kikanda, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi na watu binafsi, na ni miongoni mwa mifumo ya haraka zaidi ya ufadhili.
Yenyewe hutenga fedha kwa ajili ya mwitikio wa haraka pamoja na dharura ambazo hazijapatiwa ufadhili wa kutosha.
Maamuzi kuhusu mgao wa dharura wa fedha za CERF kwa dharura ambazo hazijapatiwa ufadhili wa kutosha hufanywa kwa kuzingatia uchambuzi wa kina wa zaidi ya viashiria 100 vya kibinadamu, pamoja na mashauriano mapana na washirika.