Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR: "Elimu ni ulinzi” sasa watoto wakimbizi milioni 5.8 wako nje ya shule, ukata ukishika kasi

Wasichana watatu vijana wa Kiafrika waliovaa blauzi nyeupe wameketi kwenye dawati la mbao darasani, wakitabasamu na kutengeneza umbo la moyo kwa mikono yao.
© UNHCR/Charity Nzomo Watoto wakimbizi kutoka Sudan wakiwa darasani nchini Ethiopia

UNHCR: "Elimu ni ulinzi” sasa watoto wakimbizi milioni 5.8 wako nje ya shule, ukata ukishika kasi

Utamaduni na Elimu
  • Watoto wakimbizi milioni 5.8 walikuwa nje ya shule mwaka 2025 .
  • Ni asilimia 32 pekee ya watoto wakimbizi waliojiunga na elimu ya sekondari.
  • “Elimu ni ulinzi” UNHCR yaonya kuwa ukata wa fedha unatishia ulinzi huo na fursa za elimu.
  • Wakimbizi waliojiunga na elimu ya juu wafikia rekodi ya asilimia 11 mwaka 2025.

Takribani watoto wakimbizi milioni 5.8, sawa na asilimia 44 ya watoto wakimbizi milioni 13.1 walio katika umri wa kwenda shule duniani, hawakuwa shuleni mwaka 2025, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).

Ripoti inaonya kuwa kupungua kwa ufadhili wa kibinadamu na maendeleo kunaweza kuwaweka mamilioni zaidi nje ya madarasa na kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana kwa miaka mingi katika elimu ya wakimbizi.

Elimu ya sekondari bado ni mtihani mkubwa

Ripoti hiyo mpya ya UNHCR “Njia za kuelekea mustakbali: Elimu, fursa na kujitegemea” inasema, asilimia 65 ya watoto wakimbizi walio katika umri wa elimu ya msingi waliandikishwa shuleni mwaka 2025, lakini idadi hiyo inashuka kwa kiasi kikubwa wanapofikia elimu ya sekondari, ambapo ni asilimia 32 pekee waliokuwa wakiendelea na masomo.

Kwa wasichana wakimbizi, hali ni mbaya zaidi, imesema ripoti huku umaskini, hatari za ulinzi, ndoa za utotoni na changamoto nyingine zikisababisha wengi kuacha shule wanapofikia umri wa balehe.

Elimu ni ulinzi

Kamishna Mkuu wa UNHCR, Barham Salih, amesema uzoefu wake mwenyewe wa kuwa mkimbizi ulimfundisha umuhimu wa elimu katika kujenga maisha mapya.

“Elimu ni ulinzi. Lakini pia ni njia ya kupata fursa na kujitegemea,” amesema. Salih ameonya kuwa katika kipindi ambacho ufadhili wa kibinadamu na maendeleo uko chini ya shinikizo kubwa, “kupunguzwa kwa fedha za elimu kunahatarisha kurudisha nyuma miongo ya uwekezaji wa pamoja na kufunga fursa kwa kizazi cha vijana.”

Mafanikio yanaonekana elimu ya juu

Pamoja na changamoto hizo, UNHCR imesema maendeleo katika elimu ya juu yanaonesha kile kinachowezekana pale uwekezaji unapodumishwa.

Idadi ya wakimbizi waliojiunga na elimu ya juu ilifikia rekodi ya asilimia 11 mwaka 2025, kutoka asilimia 9 mwaka 2024, huku zaidi ya wakimbizi 450,000 wakijiunga na vyuo na taasisi za elimu ya juu kwa mara ya kwanza.

UNHCR na washirika wake sasa wanaelekea kwenye lengo la kufikisha ushiriki wa wakimbizi katika elimu ya juu hadi asilimia 15 ifikapo 2030, kupitia vyuo vikuu, mafunzo ya ufundi, elimu mtandaoni, ufadhili wa masomo na fursa za kusoma katika nchi za tatu.

Pengo la fursa bado ni kubwa

Hata hivyo, UNHCR imesema upatikanaji wa elimu ya juu bado hauna usawa. Katika zaidi ya asilimia 80 ya nchi zilizotoa taarifa, idadi ya wakimbizi wanaojiunga na elimu ya juu ilikuwa chini ya wastani wa kitaifa.

Katika nchi zenye kipato cha chini na zilizoathiriwa na migogoro, ni asilimia 2 pekee ya wakimbizi waliojiunga na elimu ya juu, ikilinganishwa na asilimia 13 ya raia wa nchi hizo.

UNHCR pia inasisitiza kuwa uwekezaji katika elimu ya wakimbizi lazima uende sambamba na kuimarisha mifumo ya elimu ya kitaifa inayohudumia wakimbizi pamoja na watoto wa jamii zinazowahifadhi.

Ukimbizi hakupaswi kuamua mipaka ya maisha ya mtoto

Shirika la UNHCR linatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na washirika wa maendeleo kulinda ufadhili wa elimu na kuwekeza katika mifumo ya elimu ya nchi zinazowahifadhi wakimbizi.

Salih amesema lengo halipaswi kuwa kuwaweka watoto tu ndani ya madarasa, bali kuhakikisha elimu inawapa uwezo wa kujenga maisha yao ya baadaye. “Ukimbizi haupaswi kuamua mipaka ya maisha ya mtoto,” amesema.

“Mtoto anayepata fursa ya kujifunza leo amejiandaa vyema zaidi kuchangia na kujitegemea kesho.”

Soma ripoti zaidi hapa.