UNICEF: Mapigano yakiongezeka kaskazini mwa Ethiopia maisha ya watoto yanawekwa rehani
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeelezea wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa mapigano kaskazini mwa Ethiopia, likisema watoto na familia zao wako katika hatari kubwa kutokana na ghasia hizo.
Mkurugenzi wa UNICEF Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Etleva Kadilli, amesema kuna taarifa za watoto kuuawa au kujeruhiwa, huku maeneo ya makazi na miundombinu ya umma yakiharibiwa.
Kasdilli ameongeza kuwa“UNICEF ina wasiwasi mkubwa kutokana na kuongezeka kwa mapigano kaskazini mwa Ethiopia na athari zake kwa watoto na familia zao.”
Miundombinu na watoto lazima walindwe
Kadilli amezitaka pande zote zinazohusika katika mzozo kujizuia na kulinda watoto dhidi ya madhara, pamoja na kuhakikisha miundombinu ya kiraia inalindwa.
Amesisitiza pia kuwa wajibu chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu lazima iheshimiwe.
Amesema ni muhimu pia kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia watu kwa usalama, haraka na bila vikwazo, ili jamii ziendelee kupata huduma muhimu wanazozitegemea.
“Watoto tayari wameteseka vya kutosha”
UNICEF imesema watoto wa kaskazini mwa Ethiopia tayari wamepitia kipindi kigumu kutokana na migogoro na ukosefu wa usalama, na hawapaswi kuingizwa tena katika mzunguko mwingine wa ghasia.
Kadilli amesisitiza kuwa “Watoto tayari wameteseka vya kutosha. Hawawezi kuwekwa tena katika kipindi kingine cha ghasia na ukosefu wa usalama.”
Amesema jamii katika maeneo ya kaskazini mwa Ethiopia zimefanya juhudi kubwa kujenga upya shule, huduma za afya, mifumo ya maji na fursa nyingine kwa watoto, na kwamba mafanikio hayo yaliyopatikana kwa taabu yanapaswa kulindwa.
“Zaidi ya yote, watoto na familia nchini Ethiopia wanahitaji usalama na utulivu ili waweze kujenga mustakbali wao” amesema Kadilli.