Siku ya Kahawa duniani: Kusherehekea kahawa na wakulima wenyewe
- Leo ni siku ya kahawa duniani
- Fahamu mchakato wa kuchuma kahawa na uchambuzi
- Kuondoa maganda
- Rwanda na Kenya na harakati za kilimo cha buni
Uchumaji wa kahawa kutoka kwenye mbuni
Katika eneo la Huye kusini mwa Rwanda, kahawa inapogeuka kuwa nyekundu na kuiva, wakulima waliofunzwa huvuna matunda hayo kwa wakati unaofaa kabisa. Wavunaji hufanya kazi kwa utaratibu, wakitoka kwenye kivuli cha mti mmoja wa kahawa na kuingia kwenye mwanga mkali wa jua, kabla ya kuelekea kwenye mti unaofuata. Utulivu wa kazi hiyo hukatizwa tu na milio ya ndege na mlio wa kahawa zilizoiva zinapoangukia kwenye ndoo za plastiki.
Uchambuzi wa kahawa bora
Kahawa nyekundu zilizochaguliwa huhamishwa haraka hadi kwenye vituo vya kazi vya uchambuzi. Vituo hivi vilivyo katika maeneo mapana na wazi vimejisitiri katikati ya vilima vyenye kona vya eneo hilo. Wanaume na wanawake hukaa pande zote za meza ndefu, wakifanya kazi kimya na kuchagua kwa uangalifu kahawa zilizoiva zenye ubora wa juu pekee.
Uchaguzi huo wa kahawa bora iliyoiva hufuatiwa na hatua ya kuosha kahawa. Tofauti na mchakato wa kuvuna na kuchambua, unaofanyika kwa utulivu, kituo cha kuoshea kahawa, kilicho karibu zaidi na vifaa vya uchakataji, hujaa harakati zisizokoma na kelele.
Aphrodis Twagirayezu, mtaalamu wa kilimo na Meneja wa Kituo cha kuoshea kahawa cha Kyarumba, anaeleza: “Baada ya wafanyakazi kuchagua kwa uangalifu kahawa nyekundu zilizoiva na kuondoa zile zilizoiva kupita kiasi, tunaziweka kwenye tanki la kuelea ili kuondoa zile zinazoelea.”
Aphrodis anaeleza kuwa kahawa nyekundu zilizoharibika, ambazo hazijaiva vya kutosha au zilizokauka zinaweza kutambuliwa kupitia kipimo cha kuelea. “Yote yanategemea msongamano. Kahawa yenye ubora wa juu huwa na msongamano mkubwa zaidi ndani ya maji—hizo huzama—wakati kahawa yenye ubora wa chini huelea juu. Tunaondoa kahawa nyekundu zilizoiva zenye ubora wa chini kabla ya kuendelea na uchakataji.”
Hatua hii ya kituo cha kuoshea ni muhimu katika kubaini kahawa bora pekee zinazolengwa kwa ajili ya kahawa maalum ya ubora wa juu. Kahawa hizo nyekundu zilizoiva na kuchaguliwa huendelea na hatua zaidi za uchakataji: kuondoa maganda na ute wa nje, uchachushaji, kuosha na kukausha.
Uoshaji wa kahawa
Kuongezeka kwa vituo vya kuoshea kahawa—pamoja na mafunzo yanayotolewa kwa wakulima, wachambuzi na wafanyakazi wa vituo vya kuoshea kahawa—kumekuwa muhimu katika kubadilisha mavuno ya kahawa ya Rwanda kuwa kahawa maalum ya ubora wa juu inayouzwa kwa bei nzuri zaidi na kulengwa katika masoko maalumu ya nje ya nchi.
Wakati huo huo, nchini Kenya, nchi nyingine inayojulikana kwa kahawa yake, chama cha ushirika cha kahawa katika Kaunti ya Baringo kilijifufua kwa kupitisha uongozi mpya na kutekeleza mfululizo wa mageuzi yaliyolenga kuboresha utawala na usimamizi wa biashara ili kukabiliana na uzalishaji mdogo na kupungua kwa kasi kwa idadi ya wanachama.
Kenya ni mzalishaji mkubwa zaidi wa kahawa kuliko Rwanda, na inajulikana pia kwa aina ya kahawa yake ya Arabica yenye ubora wa juu. Uzalishaji umeenea nchini kote, huku kahawa ikilimwa katika kaunti 33 kati ya 47, na kutoa ajira na riziki muhimu kwa mamilioni ya Wakenya waishio vijijini.
Vyama vya washirika na mchango wao kwa wakulima
Kama ilivyo Rwanda, uzalishaji wa kahawa kwa kiwango kidogo nchini Kenya unategemea kwa kiasi kikubwa vyama vya ushirika, ambavyo huwapa wakulima wa kahawa fursa ya kupata fedha na masoko, vifaa bora vya uchakataji, pamoja na uwezo wa kushiriki katika maamuzi yanayoathiri biashara zao.
Nchi zote mbili hushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) katika kuweka kipaumbele kwenye uzalishaji wa kahawa na kufanya kazi kwa kuendelea kuboresha uzalishaji huo ili kuongeza mapato ya wakulima wao wengi wadogo.
Rwanda na ujumuishaji wa vijana kwenye kuongeza thamani zao la kahawa
Rwanda imechagua kahawa kuwa kipaumbele cha kitaifa katika Mpango wa FAO wa Mkono-kwa-Mkono au (Hand-in-Hand), kwa lengo la kuendeleza na kuwekeza zaidi katika minyororo ya thamani ya kahawa nchini. Kupitia kupewa kipaumbele huko katika mpango wa FAO, Rwanda unalenga kutumia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi pamoja na mifumo bunifu ya biashara ili kuwashirikisha vijana na kuingiza suluhisho za teknolojia ya kilimo katika uzalishaji wa kahawa.
Nchini Kenya, vyama vya ushirika vya Kaunti ya Baringo vilishirikiana na Mpango wa FAO wa Kituo cha Misitu na Mashamba, ambao uliimarisha mageuzi ya chama cha ushirika kwa kukipa ruzuku ya dola 30,000 kupitia Mpango wake wa Ruzuku Ndogo. Mabadiliko yaliyofanyika katika kipindi cha chini ya miaka mitatu yamekuwa makubwa. Idadi ya wanachama imeongezeka kutoka wakulima 756 hadi karibu 1,200. Idadi ya wanawake na vijana miongoni mwa wanachama wa chama cha ushirika iliongezeka kutoka takribani asilimia 10 hadi asilimia 40.
“Wanachama wetu wanahusika katika kila shughuli, kuanzia hatua ya kupanga,” amesema Jackson Lenge, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Tenges huko Baringo. “Tulitoa mafunzo kuhusu uchambuzi na maendeleo ya mnyororo wa thamani wa kahawa, ambapo tulishughulikia masuala yanayohusu uanzishaji wa kilimo cha buni, kuanzia utayarishaji wa ardhi, masuala ya usimamizi wa mazao, matumizi ya mbolea, upogoaji wa miti na vipengele vingine vya usimamizi.”
Afrika huchangia asilimia 17 ya kahawa duniani
Ingawa umuhimu wake hutofautiana kulingana na kiwango, kahawa ni msingi muhimu wa ajira za vijijini, riziki na uchumi wa kitaifa nchini Kenya, Rwanda na nchi nyingine kadhaa za Afrika. Bara la Afrika linachangia asilimia 17 ya uzalishaji wa kahawa duniani na asilimia 12 ya mauzo ya kahawa nje ya nchi duniani. Mauzo hayo ya nje pia huzalisha mapato ya fedha za kigeni na kuanzisha mahusiano muhimu ya kibiashara na masoko kote duniani.
Katika Siku hii ya kwanza ya Kimataifa ya Kahawa, tunaadhimisha zao la kahawa linalosaidia kuimarisha ajira na riziki za watu wa vijijini, pamoja na wakulima wa kahawa nchini Rwanda, Kenya na duniani kote, ambao wanaendelea kubuni mbinu mpya na kuboresha uzalishaji ili kutoa bidhaa ya hali ya juu kwa ajili ya kusafirishwa na kuwafikia watumiaji wa kahawa kote duniani.