Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kituo cha tiba dhidi ya Ebola,DRC chatiwa moto, Mratibu wa UN asema ni gharama kubwa

Wafanyakazi wa afya wenye mavazi ya kinga wanajitayarisha kwa ajili ya matibabu ya Ebola huko Bunia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© WHO Wafanyakazi wa afya wakijiandaa kwa kazi katika kituo cha matibabu ya Ebola kilichofunguliwa Bunia, DR Congo.

Kituo cha tiba dhidi ya Ebola,DRC chatiwa moto, Mratibu wa UN asema ni gharama kubwa

Amani na Usalama

Usiku wa kuamkia jana Jumatano kituo cha kutibu Ebola kwenye kituo cha mpito cha kuhifadhi wakimbizi huko Kigonze, karibu na mji wa Bunia jimboni Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC), kilichomwa moto, wakati huu ambapo kimesalia kitupu kutokana na wakimbizi kukimbia mashambulio ya mara kwa mara kutoka makundi yaliyojihami.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola, Julien Harneis akizungumzia tukio hilo amesema imekuwa changamoto kubwa kuanzisha vituo kama hivyo na kuweka wafanyakazi.

Ameiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa kwamba, “tunapopoteza kituo kimoja, ina maana kwamba tunapoteza uwezo wa kutoa huduma, tunapoteza uwekezaji, na tunalazimika kuanza upya. Zaidi ya yote, ina maana kwamba watu hawapati huduma wanazohitaji kwa dhati. Kwa hiyo, hili ni hasara kwetu sote. Tutachunguza pamoja na mamlaka kilichotokea na jinsi tunavyoweza kuhakikisha kwamba jambo hili halitokei tena.”

Kituo hicho ambacho kiko nje ya mji wa Bunia, kilikuwa kinahifadhi watu 18,000 lakini sasa ni kitupu kutokana na mahsambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa makundi yaliyojihami.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limekuwa likisimamia kituo hicho.

Takribani raia 2,000 wakimbilia MONUSCO Drodro kusaka hifadhi

Wakati huo huo ,kupitia ukurasa wa X, zamani Twitter, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, (MONUSCO), umesema Takribani raia 2,000 wamesaka hifadhi kwenye makazi ya muda yaliyoko kituo cha kijeshi cha ujumbe huo.

Kituo hicho kiko eneo la Drodro, jimboni Ituri ambako ni kitovu cha mlipuko wa sasa wa 17 wa Ebola.

MONUSCO inasema wakimbizi walikimbilia eneo hilo Jumatatu ya wiki hii kufuatia milio ya risasi karibu na eneo hilo.

Walinda amani walipelekwa haraka kufanya doria na hatimaye raia waliondoka kwa hiari yao kutoka kituoni hapo majira ya saa 11 jioni kwa saa za mashariki mwa DRC.