Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano baina ya vizazi ni muhimu zama za sasa za maisha marefu

Mwanamke mzee ameketi kwenye barabara yenye unyevunyevu nchini Indonesia, akiuza vikapu vya petali za maua mekundu na meupe yanayong'aa.
Picha ya UN/Andrea Brizzi Muuzaji wa maua mzee huko Jogyakarta, Indonesia. Kulingana na makadirio UN , asilimia 58 ya wazee duniani wanaishi Asia na Pasifiki, idadi inayotarajiwa kuongezeka katika miaka ijayo.

Ushirikiano baina ya vizazi ni muhimu zama za sasa za maisha marefu

Masuala ya UM
  • Idadi ya wazee duniani kufikia bilioni 2.1 ifikapo 2050
  • Uzee umekuwa ‘mwiba’ kwa wengi
  • Sera sahihi kuwezesha jamii kunufaika na uwepo wa wazee

Kila mtu ni mzee mtarajiwa na leo ni siku ya wazee duniani wakati huu ambapo inaelezwa kuwa kwa zama za sasa uzee ni changamoto kubwa kwani uzee kwa wengi huambatana na ukosefu wa usalama wa maisha na hatari ya kutengwa na maendeleo ya jamii.

Ujumbe wa mwaka huu ni Enzi ya Maisha Marefu: Kufikiria Upya Mifumo kwa Maisha Marefu,” ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anasema inahitaji kubadili mifumo yake ya kijamii na kiuchumi ili kukidhi mahitaji ya idadi inayoongezeka ya watu wanaoishi umri mrefu.

Kwa mujibu wa ujumbe wake, idadi ya watu wenye umri wa miaka 60 na zaidi inatarajiwa kuongezeka kutoka watu bilioni 1.2 hadi bilioni 2.1 ifikapo mwaka 2050. 

“Hii itamaanisha kuwa watu wenye umri huo watawakilisha takribani asilimia 20 ya watu wote duniani,” amesema Katibu Mkuu.

Maisha marefu ni mafanikio na changamoto

Kwa mujibu wa Guterres, kuongezeka kwa umri wa kuishi ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya kizazi cha sasa, yakichangiwa na maendeleo katika huduma za afya na kuimarika kwa mifumo ya ulinzi wa kijamii katika maeneo mengi duniani.

Hata hivyo, amesema “mabadiliko hayo yanaibua changamoto pamoja na fursa mpya, huku yakibadilisha uchumi na jamii kwa namna inayohitaji serikali na taasisi mbalimbali kujipanga upya.”

Guterres ameonya kuwa ubaguzi unaotokana na umri unaweza kudhoofisha haki, ustawi na uwezo wa watu wazee kushiriki kikamilifu katika jamii.

Nini kifanyike?

Sera sahihi, kwa mujibu wa Guterres, zinaweza kusaidia kukabiliana na changamoto hizo, zikiwemo sera kuhusu ajira, pensheni, makazi, huduma za afya na elimu ya maisha yote.

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa wazee si kundi linalopaswa kuonekana kama tegemezi pekee, “bali ni viongozi, walezi na washiriki muhimu katika familia, jamii na uchumi.”

Kwa msingi huo, ametoa wito wa kuimarishwa kwa mshikamano kati ya vizazi ili kuhakikisha watu wa rika zote wanashirikiana na kunufaika katika jamii inayobadilika.

Wito wa maisha marefu yenye utu

Katibu Mkuu huyo amesema dunia ina nafasi ya kubuni sera na mifumo itakayohakikisha kwamba kuishi muda mrefu kunaambatana na maisha yenye uchaguzi, usalama na utu.

“Kukabiliana na ongezeko la wazee kunahitaji mtazamo unaowahusisha vizazi vyote, huku serikali na jamii zikihakikisha kuwa watu wanaweza kuendelea kushiriki kikamilifu bila kujali umri wao,” ametamatisha Guterres.

Shamrashamra za siku hii

Kwa leo tukio hili litaadhimishwa kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi, ilhali Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa yatakuwa na tukio hili tarehe 8 mwezi huu wa Oktoba.

Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha siku hii ya Oktoba Mosi kuwa siku ya wazee duniani tarehe 14 mwezi Desemba mwaka 1990 kwa azimio namba  45/106.