Afrika isiwe mtumiaji tu wa AI, bali ishike nafasi katika kuitengeneza – Churchill Otieno
Afrika inapaswa kubadili mtazamo wake kuhusu Akili Mnemba (AI) kutoka kuwa teknolojia inayokuja kutoka nje kwa ajili ya kutumiwa, na badala yake kuona fursa ya Waafrika kushiriki katika kuitengeneza na kuitumia kutatua changamoto zinazolikabili bara hilo.
Hayo ni maoni ya Churchill Otieno, Rais wa wahariri barani Afrika, ambaye ameshiriki katika mikutano kuhusu AI na uadilifu wa habari iliyofanyika pembezoni mwa mjadala wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA81, jijini New York Marekani.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Otieno amesema Afrika tayari ina mchango muhimu katika ukuaji wa teknolojia, ikiwemo kupitia rasilimali zake za madini, lakini mchango huo unapaswa kwenda sambamba na Waafrika kuwa sehemu ya kubuni suluhu.
“Waafrika wengi wanaangalia teknolojia hii kwamba ni ile wameletewa ya kutumia tu. Wengi hawaoni kwamba wana fursa ya wao wenyewe pia kuitengeneza, [na kuitumia] kutatua shida zetu za nyumbani,” amesema.
AI na mustakabali wa uandishi wa habari
Kwa wanahabari, Otieno amesema kuibuka kwa AI kunakuja wakati sekta ya habari tayari inakabiliwa na changamoto, zikiwemo kupungua kwa mapato ya mashirika ya habari.
Hata hivyo, badala ya kuiangalia teknolojia hiyo kama tishio pekee, amesema wanahabari wanapaswa kujifunza namna ya kuitumia kurahisisha kazi na kuwafikia watu kwa njia mpya.
Amesema ingawa wanahabari wengi Afrika wameanza kujaribu AI, bado matumizi yake hayajafika mbali kutokana na hofu na maswali ambayo hayajajibiwa kikamilifu.
“Tunafika hatua ambapo si lazima wewe mwenyewe usafiri kwenda mahali. Teknolojia inaweza kukusafirisha,” amesema, akisisitiza hata hivyo wajibu wa mwanahabari wa kuchakata taarifa na kuieleza kwa namna ambayo hadhira yake itaielewa.
Afro Frequency kuunganisha maarifa na suluhu za Afrika
Otieno amesema moja ya changamoto barani Afrika ni wataalamu katika sekta mbalimbali kufanya kazi kwa kutengana, wakati maarifa au suluhu inayopatikana katika sekta moja inaweza kuwa msaada mkubwa kwa nyingine. Amesema wahandisi, wanasayansi, wanahabari, madaktari na wataalamu wa vyuo vikuu wanapaswa kupata nafasi ya kukutana na kubadilishana maarifa.
Kutokana na hilo, amesema wameanzisha Afro Frequency, jukwaa linalolenga kuwaleta pamoja wataalamu kutoka nyanja tofauti ili suluhu zinazobuniwa sehemu moja ziweze kuwafikia wengine barani Afrika.
“Tumejiuliza ingekuwaje kama tungeweza kupata nyumba kubwa ambayo ingeweza kuleta hawa watu wote pamoja, waweze kusaidiana na kuelimishana. Ndiyo tumeamua kuanzisha movement tunaita Afro Frequency ili iweze kuleta kila mtu pamoja,” amesema Otieno.
Amesema lengo ni kuhakikisha maarifa au ubunifu wa mtu mmoja hauishii kwake, bali unafikishwa kwa jamii nyingine ambazo huenda zinakabiliwa na changamoto inayoweza kutatuliwa kupitia ubunifu huo.
“Tuseme mhandisi amepata jinsi ya kutatua changamoto fulani, isiwe tu siri yake, aweze kuileta jukwaani na wengine pia wanufaike,” amesema Otieno, akiongeza kuwa suluhu inayoonekana ndogo katika eneo moja inaweza kuwa na manufaa kwa jamii nyingine katika nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Senegal.
Taarifa potofu si jukumu la wanahabari pekee
Akizungumzia uadilifu wa habari, Otieno amesema kukabiliana na taarifa potofu hakupaswi kuachiwa wanahabari pekee, kwa kuwa madhara yake yanaweza kuenea katika jamii, kuongeza kutoaminiana na hasira na kuchochea migawanyiko.
Kwa mwananchi wa kawaida, ushauri wake ni mmoja: thibitisha kabla ya kusambaza.
“La kwanza ni kujiuliza kabla hujachukua picha, video ama neno na kulisambaza: limetoka wapi?” amesema.
Amesisitiza kuwa maendeleo ya AI yenyewe si lazima yawe tatizo; muhimu ni namna teknolojia hiyo inavyotumiwa na jamii. Kwa wanahabari wa Afrika, amesema jukumu sasa ni kutafuta mbinu za kisasa za kuendelea kufanya kazi yao ya kuufikisha ukweli kwa umma katika mazingira ya teknolojia yanayobadilika kwa kasi.
Wanahabari 332 wako gerezani duniani
Otieno pia amegusia mazingira magumu ambayo wanahabari wanaendelea kukabiliana nayo, akisema wanahabari wengi wako gerezani duniani kote. “Leo hii wanahabari 332 wako kwenye jela dunia nzima. Kati yao 67 wako kwenye jela za Afrika. Tujiulize, kwa nini hawa wamewekwa korokoroni?”
Amesema takwimu hizo zinapaswa kuibua mjadala kuhusu mazingira ambayo wanahabari wanafanyia kazi na sababu zinazowafanya baadhi yao kufungwa.
Kwa mujibu wake, katika mazingira ambayo baadhi ya watu hawataki ukweli ufikie umma, wanahabari wanapaswa kuendelea kutafuta mbinu za kisasa za kufanya kazi na kukabiliana na changamoto zinazobadilika. “Kwenye jamii kuna watu wengi ambao hawangependa ukweli… Cha muhimu ni kujiuliza tunatatua vipi shida kwa wanahabari,” amesema.