Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana wa Afrika wasiwe watazamaji katika maamuzi yanayogusa mustakabali wao – Paul Siniga

Paul kutoka Tanzania amevalia suti ya kijivu na shati la bluu nyepesi huku mikono yake ikiwa imevuka dhidi ya mandhari nyeupe isiyo na dosari.
UN News Paul Siniga, Mchechemuzi wa Tanzania katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs na mleta mabadiliko wa watoto kupitia shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Tanzania.

Vijana wa Afrika wasiwe watazamaji katika maamuzi yanayogusa mustakabali wao – Paul Siniga

Masuala ya UM

Vijana wa Afrika wanahitaji kupewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maamuzi kuhusu akili mnemba, mifumo ya fedha duniani, amani na usalama, badala ya kubaki wahudhuriaji wa mikutano na watazamaji wa maamuzi ambayo athari zake zinagusa moja kwa moja maisha na mustakabali wao.

Hayo yamesemwa na Paul Siniga, mchechemuzi wa Tanzania katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs, na mleta mabadiliko wa watoto kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya watoto UNICEF nchini Tanzania, katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa baada ya kukamilika kwa Mjadala Mkuu wa ngazi ya juu wa Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA81.

Siniga amemueleza Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kuwa mijadala ya viongozi wa dunia imeonesha umuhimu wa kuwajibika kwa vizazi vijavyo wakati dunia ikikabiliwa na ukosefu wa usawa, mabadiliko ya tabianchi na kasi ya maendeleo ya akili mnemba, AI. 

AI: Vijana wa Afrika wanahitaji zaidi ya kuwa watumiaji

Akizungumzia akili mnemba, Siniga amesema vijana wa Afrika wanahitaji mambo makuu manne ambayo ni miundombinu, ujuzi, mitaji na masoko, lakini pia sauti ya pamoja katika maamuzi kuhusu utawala wa AI.

Amesema ujuzi katika maeneo kama sayansi ya data, teknolojia na ujasiriamali unaweza kuwasaidia vijana kutumia AI kutatua changamoto zinazolikabili bara lao.

“Kijana wa Dar es Salaam au Lilongwe au Kinshasa au Accra anaweza kujenga kampuni ya teknolojia yenye uwezo wa akili mnemba na kutatua changamoto za Afrika na kimataifa kwa ujumla.” 

Kwa Siniga, Afrika pia inapaswa kuwa na sauti katika kutengeneza sera zitakazosimamia matumizi ya teknolojia hiyo, badala ya kuwa mpokeaji wa maamuzi yaliyofanywa kwingine.

Madeni yasibane uwekezaji kwa vijana

Suala jingine ni mzigo wa madeni kwa nchi za Afrika. Siniga amesema sehemu kubwa ya mapato ya serikali inapotumika kuhudumia madeni, nafasi ya kuwekeza katika elimu, afya, ujuzi, teknolojia na biashara inapungua.

Kwa hiyo, anasema mjadala kuhusu uwezo wa nchi kulipa deni unapaswa kwenda sambamba na swali la iwapo nchi hizo bado zinaweza kuwekeza katika kizazi kijacho.

“Tusipime tu nchi inaweza kulipa deni. Tupime pia kama inaweza kulipa deni huku ikiendelea kuwekeza katika mustakabali wa vijana wake.” 

Ametaka pia madeni yaelekezwe zaidi katika uwekezaji wenye tija unaoweza kuchochea biashara, ajira na mapato mapya.

Mwanamke aliyevaa suti nyekundu ameketi kwenye kiti cha studio akiwa ameshika karatasi, huku nembo UMOJA WA MATAIFA ikiwa imeonyeshwa kwenye skrini ya bluu nyuma yake.
UN News Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa akiwakatika mahojiano na Paul Siniga (hayupo pichani) kwa njia ya mtandao kuhusu mkutano wa UNGA81.

Kwa nini kiti cha Afrika ndani ya Baraza la Usalama kinamhusu kijana?

Hoja za wazungumzaji wengi katika UNGA81 zilijikita katika haja ya Afrika kuwa na  viti vya kudumu pamoja na kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Siniga amesema mjadala huo kuhusu uwakilishi wa Afrika katika Baraza la Usalama si suala la kidiplomasia pekee, kwa kuwa maamuzi kuhusu amani na usalama yana athari za moja kwa moja kwa maisha ya vijana.

“Amani inapovunjika, shule zinafungwa, biashara zinakufa, uwekezaji unapungua, ajira zinapotea, familia zinahama.” 

Amesema vijana wanapaswa kujali mjadala huo kwa sababu wao ni miongoni mwa wanaoishi na matokeo ya maamuzi yanayofanywa katika mifumo ya kimataifa ambako, kwa mtazamo wake, Afrika bado haijawakilishwa ipasavyo.

“Tuna ahadi nyingi, changamoto ni utekelezaji”

Mjadala Mkuu wa ngazi ya juu wa UNGA81 ulianza tarehe 22 Septemba na kufunga pazia Jumatatu tarehe 28 Septemba, baada ya viongozi wa nchi na serikali kujadili masuala mbalimbali ya kimataifa.

Lakini kwa Siniga ambaye ni mchechemuzi wa Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs, kumalizika kwa mkutano huo hakupaswi kuwa mwisho wa ajenda zilizojadiliwa.

Anataka ushiriki wa vijana uondoke katika kuwaalika kwenye mikutano pekee na kuelekea katika kuwapa nafasi ya kushiriki katika sera, uwekezaji, matumizi ya rasilimali na uwajibikaji.

“Tayari tuna mikakati mingi, tuna maazimio mengi, tuna ahadi nyingi, lakini changamoto ni utekelezaji.” Amesema

Amesema hatua inayofuata ni kuhakikisha mijadala hiyo inatafsiriwa kuwa utekelezaji unaoonekana katika maisha ya vijana, huku wao wenyewe wakipewa nafasi ya kushiriki katika maamuzi yanayohusu mustakabali wao. 

Jina la Katibu Mkuu kwenye dawati la mbao katika Jumba la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, likiwa na viti vya bluu na picha kubwa ya ukuta.
UN Photo/Loey Felipe Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huzungumza mara kwa mara katika Baraza la Usalama. (pichani)

Katibu Mkuu mpya: Siniga atamani awe mwanamke

Akizungumzia mustakabali wa Umoja wa Mataifa, Siniga amesema anatumaini Katibu Mkuu ajaye atakuwa mwanamke, akiamini hatua hiyo inaweza kuonesha zaidi nafasi na uwezo wa wanawake katika uongozi wa ngazi za juu duniani. 

Amesema Katibu Mkuu ajaye pia atakuwa na jukumu la kuendeleza juhudi za kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.

“Naamini akiwa mwanamke itadhihirisha kwa dunia kuwa mwanamke akipewa kijiti hiki cha nafasi kubwa katika Umoja wa Mataifa… anaweza.” 

Kwa Siniga, uteuzi wa uongozi mpya ni fursa ya kuendeleza mijadala kuhusu aina ya Umoja wa Mataifa ambayo vijana wanataka kuiona katika miaka ijayo.