Mpango wazinduliwa Kenya kuhakikisha udongo wa kilimo unafaa kwa mazao
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO kwa kushirikiana na serikali ya Kenya wamezindua Mradi uitwao SoilFer unaohusisha kuwa na ramani ya aina za udongo za taifa hilo la Afrika Mashariki kwa lengo la kuwa na mfumo wa kilimo chenye mnepo.
Ndani ya Mpango huo kuna mipango mikuu mitatu ambayo ni ule wa Ubia kuhusu Udongo nchini Kenya, Maabara ya Kitaifa ya Udongo na Mpango wa Kimataifa wa Madaktari wa Udongo.
Naibu Mkurugenzi wa FAO anayeongoza kitengo cha Ardhi na Maji Nora Berrahmouni, amemweleza Stella Vuzo wa Kituo cha Habari za Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, Kenya kwamba, “mpango huu umekuwa ukisaidia nchi saba zilizomo kwenye mradi, ikiwemo Kenya, kuelewa hali ya udongo wao. Tumesaidia KALRO kuandaa na kukamilisha kile tunachokiita utafiti wa udongo.”
KALRO ni shirika la Kenya la Utafiti wa Kilimo na Mifugo.
Amefafanua kuwa “tayari tumekusanya zaidi ya sampuli 3,672 za udongo kutoka maeneo mbalimbali nchini Kenya. Sampuli hizi huchambuliwa katika maabara ya KALRO, ili kubadilisha taarifa za udongo kuwa maarifa yanayoweza kuwasaidia wakulima kuelewa mahitaji ya mashamba yao na udongo wao.
Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi huyo wa FAO, “taarifa hizi huwasaidia wakulima kujua ni virutubisho gani vinavyohitajika, ni mazao gani yanayofaa kupandwa, wapi yapandwe na namna ya kuyapanda. “
Halikadhalika, huwasaidia kujua kiasi gani cha mbolea kinachohitajika kutumia, aina gani ya mbolea inayofaa, pamoja na pembejeo nyingine, mabaki ya viumbe hai na mbinu nyingine za usimamizi wa udongo katika mashamba yao, ili kupata uzalishaji bora zaidi.
Katika nchi hizo 7, nchi tano ziko barani Afrika, ikiwemo Kenya, pamoja na nchi zingine mbili zilizoko Amerika ya Kati.
Ametamatisha akisema, “udongo wenye afya ndio msingi wa uzalishaji endelevu wa chakula, mifumo endelevu na inayostahimili changamoto ya kilimo na chakula, pamoja na uhakika wa kupata chakula na lishe na lishe bora.”