Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makubaliano ya amani DRC yashindwa kusitisha mapigano huku Ebola ikizidisha mgogoro

Wachimbaji madini wa kienyeji hubeba magunia makubwa ya madini kwenye kilima chenye miamba katika mgodi wa Mudere katika eneo la Kivu Kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© Adobe Stock/Erberto Zani Kobalti inachimbwa huko Rubaya, mashariki mwa Congo, eneo linalodhibitiwa na wanamgambo.

Makubaliano ya amani DRC yashindwa kusitisha mapigano huku Ebola ikizidisha mgogoro

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana Jumanne ya Septemba 29 mjini New York,Marekani kujadili hali katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambako mapigano kati ya majeshi ya Serikali na waasi wa M23 yanaendelea mashariki mwa nchi hiyo licha ya kuwepo kwa mfululizo wa makubaliano ya amani.

Mabalozi wanatarajiwa kujadili ufuatiliaji wa usitishaji mapigano, kuongezeka kwa mvutano kati ya DRC na Rwanda, pamoja na mlipuko mbaya zaidi wa Ebola kuwahi kutokea nchini humo, ambao hadi sasa umesababisha vifo vya zaidi ya watu 3,900.

Mambo muhimu:

  • DRC na Rwanda zilitia saini Makubaliano ya Washington mwezi Desemba 2025, huku Kinshasa na M23 zikitia saini mfumo wa amani wa Doha mwezi mmoja kabla.
  • DRC inadai kuwa zaidi ya watu 300 waliuawa mwezi Juni na Julai katika maeneo yanayodhibitiwa na majeshi ya Rwanda na M23. Rwanda imekanusha madai hayo.
  • Tarehe 8 Septemba, wapiganaji 120 wa zamani wa FDLR, wapiganaji wengine wa kigeni waliowahi kushiriki mapigano pamoja na wategemezi wao walirejeshwa Rwanda.
  • Kufikia tarehe 26 Septemba, mlipuko wa Ebola ulikuwa umeathiri majimbo saba, ukiwa na zaidi ya wagonjwa 8,000 waliothibitishwa na vifo 3,901.
  • Mamlaka ya MONUSCO yanatarajiwa kufanyiwa upya mwezi Desemba.

DRC yalitaka Baraza lisitishe ushiriki wa Rwanda katika operesheni za kulinda amani za UN

Zenon Ngay Mukongo, Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, amesema Baraza haliwezi kubaki bila kuchukua hatua wakati ukosefu wa usalama ukiendelea katika mashariki mwa nchi hiyo.

Akizungumza kuhusu kile alichokiita “kutokuwa na nia njema wazi” kwa washambuliaji, amesema Kinshasa itaendelea kulinda eneo lake.

Akilaani shambulio la ndege isiyo na rubani linalodaiwa kufanywa na Jeshi la Ulinzi la Rwanda dhidi ya eneo la DRC huko Pinga tarehe 20 Septemba, ambapo watu watano waliuawa, alisema:

“Baraza haliwezi kudai utekelezaji wa ahadi bila kuhakikisha kuwa ahadi hizo zinatekelezwa na pande zote.”

Kwa msingi huo, amelitaka Baraza lisitishe ushiriki, kupelekwa na kubadilishana vikosi vya Rwanda katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa hadi majeshi ya nchi hiyo yatakapoondoka katika ardhi ya DRC.

“Baraza haliwezi kuwavumilia wanachama wa operesheni zake za kulinda amani ambao kwa wakati mmoja wanajifanya wazima moto na wachomaji moto,” amesema, akiongeza:

“Mamlaka yenyewe ya Baraza hili na uaminifu wa maamuzi yake viko hatarini.”

Burundi yasema nchi zinazowahifadhi wakimbizi lazima ziungwe mkono

Zéphyrin Maniratanga, Mwakilishi wa Kudumu wa Burundi, amesema eneo la Maziwa Makuu hususan mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limekumbwa na “mizunguko mibaya ya ghasia” kwa miongo kadhaa.

Amesema sababu za mgogoro huo zinajulikana, na Baraza limepitisha maazimio kadhaa katika kukabiliana nao.

Hata hivyo, amesema swali la sasa ni “utekelezaji madhubuti wa maamuzi ambayo tayari yamepitishwa.”

“Hatuwezi kusubiri mlipuko mwingine wa ghasia ndipo tupitishe azimio jipya, wakati ahadi za awali bado hazijatekelezwa kikamilifu,” amesema.

Amesisitiza kuwa ni wakati wa kuondoka katika mtazamo wa kukabiliana na migogoro baada ya kutokea na kuelekea katika “kuzuia migogoro, utekelezaji na uwajibikaji.”

Akizungumzia pia gharama zinazobebwa na nchi jirani, alisema Burundi inawahifadhi idadi kubwa ya wakimbizi kutoka Kongo.

“Mshikamano huu unaweka mzigo mkubwa kwa nchi yenye rasilimali chache na kwa jamii zinazowahifadhi familia hizi,” amesema, akitaka hali hiyo izingatiwe kikamilifu katika juhudi za kimataifa za kuleta amani na usalama katika eneo hilo.

Mpango wa misaada ya kibinadamu lazima ufadhiliwe, Tanzania yasema

Togolani Edriss Mavura, Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameeleza wasiwasi kuhusu vifo vya raia, watu wengi kulazimika kuyakimbia makazi yao, kuongezeka kwa ukatili wa kingono na ukatili wa kijinsia, pamoja na mlipuko mkubwa unaoendelea wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Katika hali hiyo, alitoa wito wa kuongezwa kwa msaada kwa mpango wa mwitikio wa kibinadamu wa mwaka 2026 ambao hadi sasa umefadhiliwa kwa nusu tu, akisema: “Ukosefu wa fedha unapaswa kuifanya dhamiri yetu ijitafakari.”

Kuhusu hali ya usalama, alisema “jambo muhimu katika kupunguza mvutano ni kuheshimu kikamilifu makubaliano ya kusitisha mapigano,” huku akiikaribisha MONUSCO kwa juhudi zake za kufuatilia usitishaji mapigano katika maeneo kama mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

Pia aliunga mkono mbinu zinazozihusisha jamii katika mchakato wa kuwaondoa wapiganaji kwenye makundi yenye silaha, kuwarejesha katika maisha ya kawaida na kuwaunganisha tena na jamii.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kwa mazungumzo kati ya MONUSCO na Serikali mwenyeji kuhusu uwepo wa Operesheni hiyo na muundo wake wa baadaye.

Rwanda yasema FDLR lazima iondolewe kama tishio

Akikumbusha kwamba Umoja wa Mataifa umetumia zaidi ya dola bilioni 30 tangu mwaka 1999 kushughulikia mgogoro wa usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Karoli Martin Ngoga, Mwakilishi wa Kudumu wa Rwanda, alisema: “Hata hivyo, changamoto kuu za kiusalama ambazo mara kwa mara zimeufikisha mgogoro huu wa kikanda mbele ya Baraza bado hazijatatuliwa.”

Amesisitiza kuwa “FDLR [Forces démocratiques de libération du Rwanda] lazima iondolewe kama tishio, na hatua hiyo lazima iwe kamili, madhubuti na iweze kuthibitishwa.”

Amesema uwepo unaoendelea wa kundi hilo mashariki mwa DRC, pamoja na “itikadi yake ya mauaji ya kimbari na ushirikiano na msaada unaoendelea kutoka kwa Serikali ya DRC,” ni “tishio la moja kwa moja na la kuwepo kwa Rwanda.”

Amesisitiza: “Hivyo ndivyo Rwanda inavyoelewa tishio hili, na hivyo ndivyo tunavyopaswa kulishughulikia. Ni tishio la sasa; si tishio la mbali.”