Eritrea: Mfumo wa dunia lazima ujengwe katika haki na usawa
Eritrea imesema kujenga mfumo mpya wa kimataifa unaozingatia haki, usawa na kuheshimu haki ya mataifa kumiliki na kunufaika na rasilimali zao ni muhimu katika kufikia amani, utulivu na maendeleo endelevu duniani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Eritrea, Osman Saleh Mohammed, amesema hayo akihutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA81, jijini New York, Marekani, akimuwakilisha Rais wa nchi hiyo.
Amesema moja ya changamoto kubwa zinazokabili dunia ni ukosefu wa haki kiuchumi, akisisitiza umuhimu wa watu na mataifa kuwa na mazingira yanayowawezesha kuzalisha mali na kunufaika kwa haki na matunda ya kazi na rasilimali zao.
“Dhamira kuu ni kumiliki kwa haki rasilimali za kiuchumi na matunda ya kazi, na kusonga katika njia endelevu ya maendeleo na ustawi kutoka kizazi kimoja hadi kingine,” amesema.
Kwa mujibu wa Waziri Saleh, ukuaji wa uchumi na ustawi hauwezi kutenganishwa na amani, utulivu na haki. Pia ametaka kuimarishwa kwa kuheshimiana na ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
Afrika isimame pamoja
Saleh amesema Waafrika ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa kile alichokitaja kuwa mfumo wa kimataifa usio na usawa, hivyo akatoa wito kwa nchi za bara hilo kuandaa mikakati madhubuti na kuimarisha umoja katika kusukuma mbele haki na usawa.
Migogoro ya dunia na Pembe ya Afrika
Akizungumzia hali ya amani na usalama duniani, Saleh ametaka kukomeshwa kwa vita nchini Iran na Ukraine, huku akisema pia hatua zinahitajika kukabiliana na migogoro na machafuko katika maeneo yanayoizunguka Eritrea.
“Vita nchini Ukraine, pamoja na athari zake za aina mbalimbali, lazima pia vikomeshwe,” amesema Saleh.
Ametaja pia Bonde la Mto Nile, Pembe ya Afrika, Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden kuwa miongoni mwa maeneo yanayohitaji hatua za kukomesha migogoro na kuimarisha utulivu. Aidha, ametaja mabadiliko ya tabianchi kuwa changamoto inayohitaji suluhu za kudumu.