Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika lazima ishirikiane kutengeneza chanjo na dawa zake: Profesa Janabi

Mwanamke Mweusi aliyevaa shati na miwani yenye mistari anamsikiliza mwanaume Mweusi aliyevaa suti ya bluu na tai nyekundu huku wakiwa wameketi mezani wakitazamana wakati wa mahojiano.
UN News Profesa Mohamed Yakub Janabi (kulia), Mkurugenzi wa Afya wa WHO Kanda ya Afrika, akihojiwa na Leah Mushi (kushoto) wa UN News Kiswahili pembezoni mwa kikao cha UNGA81.

Afrika lazima ishirikiane kutengeneza chanjo na dawa zake: Profesa Janabi

Afya

Nchi za Afrika zinapaswa kuacha kutegemea uagizaji wa chanjo na dawa kutoka nje na badala yake kushirikiana kupitia jumuiya za kikanda kujenga uwezo wa kuzalisha bidhaa hizo barani humo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi, katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Kandoni mwa mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani Profesa Janabi amesema “Afrika kwa sasa inaagiza kutoka nje asilimia 100 ya chanjo inazotumia na asilimia 85 ya dawa na vifaa tiba, hali inayoliweka bara hilo katika mazingira magumu wakati wa majanga ya kiafya.”

Profesa Janabi, mwanaume Mweusi aliyevaa miwani yenye fremu nyeusi, suti ya bluu, shati jeupe na tai nyekundu, amesimama kwenye korido ya ndani akiwa amevaa pini ya mviringo yenye rangi mbalimbali.
UN News Dkt. Mohamed Yakub Janabi, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika. katika mahojiano na UN News Kiswahili kandoni mwa hafla inayohusiana na afya ya UNGA81.

Akieleza nini kifanyike amesema “Ushauri wangu mkubwa kwa viongozi wa Afrika ni kutumia jumuiya zetu za maendeleo, kwa mfano Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC na ECOWAS. Kila kanda inaweza kuangalia ni nini inaweza kutengeneza.”

Amesema badala ya kila nchi kuwekeza katika kutengeneza bidhaa zinazofanana, nchi zinapaswa kuratibu uzalishaji kwa kuzingatia uwezo na mahitaji yao, hasa kwa kuwa mtaji uliopo bado ni mdogo.

Kwa mujibu wa Profesa Janabi, uzoefu wa janga la coronavirus">COVID-19 ulionesha umuhimu wa Afrika kuwa sehemu ya maamuzi kuhusu uzalishaji na upatikanaji wa chanjo na tiba.

“Hatuhitaji tu kupata kiti kwenye meza ya chakula. Tunataka na sisi tuwe sehemu ya kutengeneza hiyo meza,” amesema.

Ebola DRC: Ukosefu wa usalama wakwamisha udhibiti

Akizungumzia mlipuko wa Ebola aina ya Bundibugyo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Profesa Janabi amesema mapigano na ukosefu wa usalama ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazokwamisha juhudi za kudhibiti ugonjwa huo.

Amesema ugonjwa huo uligunduliwa kwa kuchelewa, huku vipimo vya maabara vikionesha kuwa ulianza kusambaa takribani miezi minne kabla ya kutangazwa.

Mfanyakazi wa afya mwanamke mweusi aliyevaa koti jeupe akimdunga sindano mtu aliyevaa fulana ya beige ya kukabiliana na dharura, akiwa amezungukwa na wapiga picha na wafanyakazi wa vyombo vya habari ndani ya hema jeupe.
WHO Programu ya utafiti wa chanjo inaendelea turi, Mashariki mwa DRC kwa wahudumu wa afya walio katika hatari ya Ebola

WHO inahitaji kufuatilia takribani asilimia 95 ya watu waliokutana na wagonjwa ili kudhibiti Ebola ipasavyo, lakini katika maeneo yaliyoathirika kiwango hicho kimekuwa karibu asilimia 70 na wakati mwingine kushuka hadi asilimia 60 kutokana na machafuko.

“Vituo vyetu vinashambuliwa, wafanyakazi wanashambuliwa. Sio sehemu salama,” amesema Profesa Janabi.

Hata hivyo amebainisha kuwa takribani wataalamu 350 wako katika eneo hilo wakishirikiana na wadau wengine wakiwemo Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, Africa CDC na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya watotot UNICEF.

Kuhusu chanjo, Profesa Janabi amesema chanjo iliyopo ni ya Ebola aina ya Zaire na sasa inafanyiwa majaribio kuona iwapo inaweza kutoa kinga dhidi ya Bundibugyo, wakati juhudi za kupata chanjo mahsusi kwa aina hiyo zikiendelea.