Lesotho yasema utamaduni wa amani unahitaji taasisi imara
Lesotho yasema utamaduni wa amani unahitaji taasisi imara
Waziri Mkuu wa Lesotho, Samuel Ntsokoane Matekane, ametoa wito wa kuimarishwa kwa taasisi za kimataifa ili kuzuia migogoro na kudumisha amani.
Akihutubia Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, (UNGA81), Matekane amezungumzia kuhusu hali ya nchi yake, akisema uzoefu wa Lesotho unaonesha umuhimu wa diplomasia ya kuzuia migogoro, akisisitiza kuwa utamaduni wa amani unahitaji taasisi imara na zinazowajibika.
Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, amesema “tishio hilo si la siku zijazo bali ni changamoto ya sasa, likisababisha mafuriko makubwa, ukame na uharibifu wa ardhi na miundombinu. Tunaomba nchi zilizoendelea kuongeza fedha na teknolojia kwa mataifa maskini yanayoathirika zaidi.”
Utekelezaji wa SDGs
Akamulika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs yanayofikia ukomo mwaka 2030 ambapo amesema,” Lesotho inaendelea kujitolea kutekeleza Ajenda ya 2030. Tumeharakisha mageuzi katika maendeleo ya biashara, uwezeshaji wa biashara, usimamizi wa fedha za umma, uwezeshaji wa vijana na nishati jadidifu”
Hata hivyo, amesema kuna changamoto kama vile ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana ambapo kiwango sasa ni asilimia 38.
Mshtuko wa uchumi unaotokana na mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa usawa vinaendelea kuzuia mabadiliko shirikishi ya kiuchumi na kijamii.
“Kwa kuwa imesalia miaka mitatu pekee kufikia mwaka 2030, tunatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutimiza ahadi zao za msaada rasmi wa maendeleo. Kutimiza ahadi hizo ni hatua muhimu katika kurejesha uaminifu,” amesema Waziri Mkuu huyo wa Lesotho.