UNGA81: Urusi yazishutumu nchi za magharibi kutaka kuendelea kuhodhi utawala wa dunia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov, amesema mabadiliko makubwa yanaendelea katika siasa za kimataifa na kwamba dunia inaelekea kwenye mfumo ambao nchi nyingi zinakuwa na ushawishi na nguvu kubwa mkubwa, badala ya nguvu kutawaliwa na nchi moja au kundi dogo la nchi.
Akihutubia Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Lavrov amesema nchi za Kusini na Mashariki mwa dunia zinazidi kujitokeza kama vituo huru vya maendeleo na usalama.
Amesema Urusi inaunga mkono mwelekeo huo kupitia ushirikiano na BRICS, Shirika la Ushirikiano la Shanghai na jumuiya nyingine.
Lavrov amezikosoa nchi za Magharibi akisema zinajaribu kulinda nafasi na upendeleo wao na kulazimisha kanuni zao kwa nchi nyingine.
Mashariki ya Kati na Palestina
Kuhusu Mashariki ya Kati, Lavrov amesema Urusi inaunga mkono juhudi za kujenga amani na usalama katika eneo hilo, ikiwemo kuimarisha uaminifu kati ya Iran na nchi za Kiarabu za Ghuba.
Kuhusu Palestina, amesema suluhisho la msingi ni kuanzishwa kwa dola ya Palestina kwa kuzingatia uamuzi wa Umoja wa Mataifa.
Amesema hali ya kibinadamu Gaza bado ni mbaya, huku akionya kuwa upanuzi wa makazi ya Israel katika Ukingo wa Magharibi unaweza kufanya uanzishwaji wa dola ya Palestina kuwa mgumu.
Ametaka hatua za haraka za kimataifa pia kuchukuliwa kuhusu migogoro na hali za kibinadamu katika Lebanon, Syria, Yemen, Iraq, Sudan, Somalia na Sudan Kusini.
Ukraine na usalama wa Ulaya
Akizungumzia Ukraine, Lavrov amezishutumu nchi za Magharibi kwa kuendelea kupeleka silaha kwa Kyiv na kuzuia juhudi za kufikia suluhu ya amani.
Amesema Urusi itaendelea na operesheni yake ya kijeshi hadi malengo yake yatakapofikiwa na vitisho kwa usalama wa Urusi kuondolewa.
Mageuzi ya Umoja wa Mataifa
Lavrov ametaka mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuongeza uwakilishi wa Afrika, Asia na Amerika ya Kusini.
Amesema Urusi inaunga mkono Brazil na India kuwa wanachama wa kudumu wa Baraza hilo, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia madai ya Afrika kupitia Mwafaka wa Ezulwini na Azimio la Sirte.
Pia amesema Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa anapaswa kuwa mwadilifu na kuwakilisha jumuiya nzima ya kimataifa.
Akili Mnemba na mfumo mpya wa dunia
Lavrov amesema Umoja wa Mataifa unapaswa kuwa kitovu cha juhudi za kuweka kanuni za kimataifa kuhusu Akili Mnemba (AI) na usalama wa mtandao.
Ameunga mkono ushiriki wa nchi zote katika kuandaa kanuni hizo na pia ametaja mpango wa China, unaoungwa mkono na Urusi, wa kuanzisha shirika la kimataifa la ushirikiano kuhusu AI.
Akihitimisha, Lavrov amesema amani ya kudumu inaweza kupatikana kwa kuheshimu kanuni ya usalama sawa kwa nchi zote, bila nchi moja kuhakikisha usalama wake kwa gharama ya usalama wa nyingine.
Amesema Urusi inaunga mkono kuanzishwa kwa mfumo mpana wa usalama na ushirikiano barani Ulaya na Asia, akisema dunia inaelekea kwenye mfumo wenye nguvu zilizosambaa katika nchi na maeneo mbalimbali.
Aidha ameitumia hotuba hiyo kukemea hatua ya Marekani kumteka rais wa Venezuela na kumpeleka katika jela ya Marekani, pia akatoa wito wa kukomeshwa kwa vikwazo dhidi ya Cuba.