Dadaab yaonesha uwezo wa kuzalisha chakula katika ardhi yenye ukame
Dadaab yaonesha uwezo wa kuzalisha chakula katika ardhi yenye ukame
- Ni kutokana na usaidizi na muongozo kutoka WFP
- Wakulima sasa wanavuna mboga za maji na matunda
- Maji ndio uti wa mgongo wa ufugaji na kilimo Dadaab
Mandhari ya Dadaab kambi ya wakimbizi iliyoko kaunti ya Garissa, kaskazini - mashariki mwa Kenya barani Afrika kwa muda mrefu yamehusishwa na ukame, uhaba wa maji na utegemezi wa misaada. Lakini mashamba ya mboga yanayochanua katikati ya ardhi kavu yanaonesha kuwa eneo hilo lina uwezo mkubwa wa kuzalisha chakula.
Katika mashamba yanayoungwa mkono na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), wanawake wanapanda na kuvuna bamia na mboga nyingine.
Chapisho kwenye wavuti wa WFP likibeba tafakuri ya Mkurungenzi Mkazi wa shirika hilo nchini Kenya Betty Ka, linaeleza kuwa baadhi ya mazao hutumiwa na familia, huku ziada ikiuzwa kwa ajili ya kupata kipato.
Tumulike uwezo wa maeneo badala ya changamoto pekee – Betty Ka
Bi Ka, katika chapisho hilo anasema katika mwaka wake wa kwanza nchini Kenya, ametembelea baadhi ya maeneo kame, kuanzia Garissa na Dadaab kaskazini-mashariki hadi Kakuma katika Kaunti ya Turkana kaskazini-magharibi.
“Nimeona mazao kutoka kwenye mashamba ya kilimo cha bustani yanayoungwa mkono na WFP—nyanya, matikiti maji, pilipili hoho na mboga za majani—yakimea katika maeneo ambayo kwa kawaida huonekana kuwa makavu zaidi wakati mvua inapokosekana.”
Uzoefu huo, anasema, unaonesha umuhimu wa kuangalia uwezo wa maeneo kame badala ya kuzingatia changamoto pekee.
“Maji ndiyo uti wa mgongo. Tukipata hilo sawa, mambo mengine mengi yanawezekana,” amesema Bi. Ka.
Maji yanafungua fursa za kilimo- Mabwawa ya kuhifadhi maji ya mvua
Katika kambi ya Hagadera, ambayo ni sehemu ya Dadaab, WFP inaunga mkono matumizi ya mabwawa ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua kwa ajili ya umwagiliaji.
Wakulima wanaotumia maji hayo wameanza kuzalisha mazao ambayo hapo awali yalikuwa magumu kulimwa katika mazingira hayo. Mapema mwezi huu, walivuna matikiti maji kwa mara ya kwanza.
“Changamoto bado ni kubwa. Ukame haujatoweka, na jamii bado zinakabiliwa na uhaba wa maji, mabadiliko ya tabianchi na mazingira magumu ya kiuchumi,” anasema Bi. Ka, huku akiongeza kuwa, “upatikanaji wa maji unawawezesha wakulima kuongeza aina ya mazao, kuboresha chakula cha familia na kupata kipato kutokana na mauzo.”
Kuunganisha uzalishaji na masoko
WFP inasema maji pekee hayatoshi. Wakulima wanahitaji masoko ya kuuza mazao, wakati jamii zinahitaji miundombinu, huduma na taarifa za hali ya hewa.
Shirika hilo linawasaidia wakulima wadogo kukusanya mazao na kuyafikisha sokoni, ikiwa ni pamoja na shule zinazopata chakula kutoka kwa wazalishaji wa ndani kupitia programu za Serikali za mlo shuleni.
Mwaka 2025, mipango ya WFP ya mifumo ya chakula inayostahimili mabadiliko ya tabianchi iliwafikia karibu watu 650,000. Wakulima waliounganishwa na mipango hiyo waliuza takriban tani 83,000 za mazao yenye thamani ya dola milioni 21 za Marekani.
Kutoka kukabiliana na majanga hadi kujenga uwezo
Kwa WFP, lengo si kukabiliana na dharura pekee, bali kusaidia familia kuwa na uwezo wa kustahimili ukame na misukosuko mingine.
Kwa Dadaab, mashamba yaliyostawi na yenye ukijani katikati ya ardhi kame yanaonesha uwezekano wa kuongeza uzalishaji wa chakula, kipato na kujitegemea wakati jamii inapowezeshwa kupata maji, ardhi yenye afya na masoko.
Soma makala nzima hapa.