Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israel: Tutaendelea kushinda, tutaendelea kujitetea hatuna chaguo lingine

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akizungumza katika jukwaa la UMOJA WA MATAIFA wakati wa kikao cha Baraza Kuu UN jijini New York.
Picha ya UN/Loey Felipe Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu akihutubia Mjadala Mkuu wa kikao cha 81 cha Baraza Kuu la UN.

Israel: Tutaendelea kushinda, tutaendelea kujitetea hatuna chaguo lingine

Masuala ya UM

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameahidi kwamba taifa lake litaendelea kushinda mabambano dhidi ya magaidi na litaendelea kujitetea na kulinda watu wake kwa sababu hawana chaguo lingine.

Akihutubia Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA81 Waziri Mkuu Netanyahu ametumia hotuba yake kueleza operesheni za kijeshi za Israel kama mapambano ya kulinda uhai wa taifa hilo.

Netanyahu amesema Israel imekabili vitisho kutoka pande mbalimbali akitaja mashambulizi dhidi ya Hamas, Hezbollah, Iran na makundi washirika. Pia ametetea shambulio dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, akisema lililenga kuzuia kile alichokitaja kuwa tishio la kuwepo kwa Israel

 Waziri Mkuu huyo kuhusu Gaza amesema magaidi kutoka kundi la Hamas wameendelea kutekeleza ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya Wayahudi kwa kutekeleza mashambulizi mabaya zaidi yakigaidi na kikatili likiwemo shambulio la Oktoba 7 mwaka 2023 ambapo mamia ya watu waliuawa, kutekwa mateka na kunyanyaswa.

“Tutashinda. Hatuna chaguo jingine”

Akirejea historia ya vita vya Israel na operesheni ya uokoaji ya Entebe ya mwaka 1976 iliyoongozwa na kaka yake, Yoni Netanyahu, Netanyahu amesema historia hiyo imeimarisha azma ya Israel ya kujilinda.

Amesisitiza ujumbe wake kwa kauli, “Tutashinda. Hatuna chaguo jingine,” akisema Israel itaendelea kupambana dhidi ya vitisho inavyovikabili.

Kauli hiyo ilikuwa sehemu kuu ya ujumbe wake wa kuhalalisha hatua za kijeshi za Israel.

Pia ameishukuru serikali ya Uganda kwa kujenga mnara wa Yoni mahali ambapo kaka yake alipoteza maisha huko Entebe mwaka 1976.

Nyuklia ya Iran: ilikua uazmuzi rahisi kuiteketeza

Akigeukia nyuklia ya Iran Netanyahu amesema kuteketeza nyuklia ya Iran ambalo ni jambo gumu sana kwa wengine, kwake ilikuwa ni moja ya maamuzi rahisi sana sana akisema “kwa sababu kama tusingefanya hivyo, sote tungeangamia. Israel pia ilizilinda nchi nyingi ambazo wajumbe wake sasa wameondoka katika ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Kwa kweli, viongozi wengi walitushukuru kwa siri” kwa kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran.

Idadi ya wajumbe kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa waliondoka katika ukumbi wa Baraza Kuu muda mfupi baada ya Netanyahu kuingia kutoa hotuba yake.

Israel haifanyi mauaji ya kimbari inayazuia

Kuhusu tuhuma za Israel kufanya mauaji ya kimbari Netanyahu amesema Israel imechukua hatua za kupunguza vifo vya raia, zikiwemo kutoa tahadhari za uhamishaji, kupiga simu na kusambaza vipeperushi, pamoja na kuwezesha uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu na chanjo.

“Ni utawala gani unaodaiwa kulenga kufanya mauaji ya kimbari ambao unapeleka kwa wakazi wa upande unaoupinga dozi milioni moja za chanjo ya polio? Ni utawala gani unaodaiwa kulenga kufanya mauaji ya kimbari ambao unawezesha kupelekwa kwa tani milioni mbili za chakula katika Ukanda wa Gaza? Hiyo ni sawa na tani moja kwa kila mtu. Tuhuma kwamba Israel inafanya mauaji ya kimbari ni uongo mkubwa zaidi wa karne,” alisema Waziri Mkuu wa Israel.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema hali ya Gaza imekuwa na kiwango kikubwa cha mauaji na uharibifu, na amesisitiza kwamba pande zote zinapaswa kuzingatia sheria za kimataifa na maagizo ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki.

Kinachofanywa na Walozi Ukingo wa Magharibi si vurugu

Pia amepuuza mjadala kuhusu vurugu zinazofanywa na walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi. Amesema Israel imechukua hatua kubwa za kuwalinda raia, zaidi ya jeshi lolote jingine duniani.

Awakosoa wakosoaji wa Israel na kumlenga Mamdani

Netanyahu pia amezishutumu baadhi ya serikali, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwa kile alichokiita kueneza simulizi za chuki dhidi ya Israel na chuki dhidi ya Wayahudi.

Amezikosoa nchi kadhaa za Magharibi, akisema viongozi wao wamechagua kusalimu amri mbele ya “makundi ya watu wanaopinga Wayahudi.”

Amezitaja Qatar na Uturuki kuwa miongoni mwa wakosoaji wake, huku akimkosoa pia Meya wa New York Zohran Mamdani akisema “Wayahudi wengi hawajihisi salama mjini New York tangu alipoingia madarakani.

 Aidha, akirejea Iran, Netanyahu amesema uongozi wa nchi hiyo bado ni tishio kuu la kimkakati kwa Israel, lakini amedai mabadiliko ya kisiasa nchini Iran hatimaye yatatoka kwa wananchi wake.