Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mary Nyiriak kutoka Kakuma hadi Balozi wa UNHCR: “Leo Sudan Kusini, kesho inaweza kuwa nchi yako”

Mwanamke Mweusi mwenye nywele zilizosokotwa na hereni za dhahabu anaongea akiwa amesimama katika duka la nguo lenye rafu za nguo zilizokunjwa.
UN News Mary Nyiriak Maker, Balozi Mwema wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR akizungumza na Flora Nducha of UN News Kiswahili.

Mary Nyiriak kutoka Kakuma hadi Balozi wa UNHCR: “Leo Sudan Kusini, kesho inaweza kuwa nchi yako”

Wahamiaji na Wakimbizi

Kwa miaka 22, Mary Nyiriak Maker aliita kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya kuwa nyumbani. Alifika huko akiwa  na umri wa miaka mitatu na matumaini kwamba angekaa kwa miaka miwili au mitatu tu, bila kujua kwamba maisha yake yangekita mizizi katika kambi hiyo kwa zaidi ya miongo miwili.

Leo, kutoka mbali Sudan Kusini na Kakuma, Mary ni Balozi Mwema wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, akitumia hadithi yake mwenyewe kutetea haki, matumaini na fursa kwa mamilioni ya wakimbizi duniani.

“Nilidhani tutakaa miaka miwili au mitatu kambini”

Mary anatoka Sudan Kusini, lakini safari yake ya maisha ilimpeleka Kenya akiwa mkimbizi. Alipofika, alidhani kukaa kwake kungekuwa kwa muda mfupi.

Badala yake, miaka miwili au mitatu ikageuka kuwa miaka 22. “Nilidhani tutakuwapo kwa miaka miwili ama mitatu. Sikujua nitakaa kwenye hii kambi kwa miaka ishirini na mbili,” anakumbuka.

Kakuma haikuwa tu mahali pa kuishi. Ilikuwa mahali ambapo Mary alikulia, akasoma na baadaye akaanza kufundisha watoto wengine wakimbizi. Kwa kifupi ilikuwa nyumbani.

Alisoma shule ya sekondari Nakuru, Kenya, na baada ya kumaliza alijaribu kuomba nafasi ya chuo kikuu kwa miaka miwili bila mafanikio. Changamoto kubwa ilikuwa gharama na hadhi yake kama mkimbizi.

Elimu ilikuwa tiketi yake ya kutoka kambini

Mary alipojaribu kuingia chuo kikuu nchini Kenya, alikabiliwa na ada kubwa kwa mtu ambaye hakuwa raia wa Kenya.

Hatimaye, akachagua kufundisha wanafunzi katika mazingira ya wakimbizi. Alishuhudia kwa karibu njaa, changamoto za ajira na ndoto za vijana waliokuwa wakitafuta maisha bora.

“Miaka miwili nilianza kufundisha wanafunzi, na wote ni wakimbizi. Unaona kuna njaa, kuna matumaini mengi ya watu kutaka kuwa kwenye nchi na maisha bora. Tatizo kama mkimbizi kupata kazi ni ngumu,” anasema.

Mary anasema uzoefu huo ulimfundisha kwamba wakimbizi mara nyingi wanaonekana kupitia dhana na si kupitia ndoto na uwezo wao.

Baadhi ya ndugu zake mwenyewe walizaliwa katika kambi ya Kakuma, hivyo kwao kambi haikuwa sehemu ya muda tu, bali ndiyo ilikuwa nyumbani waliyoijua.

Wanawake wawili Weusi katika hafla ya pembeni UMOJA WA MATAIFA ; mmoja ameketi katika gauni jeupe anatumia simu huku mwingine akiwa amesimama katika koti jeusi akiwa na koti la UN akiangalia hati mezani.
UN News Mary Nyiriak Maker (kushoto), Balozi Mwema wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR akizungumza na Flora Nducha of UN News Kiswahili.

Kutoka Kakuma hadi chuo kikuu cha Minnesota

Hatimaye, Mary alipata nafasi ya kusoma katika Chuo Kikuu cha Minnesota nchini Marekani.

Lakini kupata nafasi ya chuo hakukumaanisha safari ya ukimbizi ilikuwa imekwisha. Alikabiliwa na changamoto ya nyaraka za kusafiria na utambulisho.

“Huna passport, huna njia ya kupata passport ya wakimbizi inayoitwa Conventional Travel Document. Unaweza kuipata tu Nairobi, inachukua muda mwingi,” anaeleza.

Changamoto hiyo ilimlazimu kutafuta msaada kutoka kwa taasisi na maafisa walioweza kumsaidia kukamilisha taratibu za kusafiri.

Hata suala la kuthibitisha uraia wake lilikuwa gumu pia kwa sababu alikuwa raia wa Sudan Kusini lakini alikuwa hajawahi kuishi nchini humo.

“Mkimbizi ni binadamu pia”

Uzoefu huo ndio unaomfanya Mary azungumze kwa nguvu zote kuhusu umuhimu wa nchi kurahisisha taratibu zinazowapa wakimbizi fursa ya kusoma, kufanya kazi na kusafiri.

Kwa mtazamo wake, utambulisho wa mkimbizi haupaswi kuwa kikwazo cha kumzuia mtu kutimiza na kufikia uwezo wake.

“Hiyo ni changamoto sisi kama wakimbizi tungepanda kuona kama nchi zinaweza kurahisisha suluhisho litakalotufanya tuweze kutembea kwa uhuru kama mkimbizi, kama binadamu,” anasema.

Leo, Mary anaendelea kuishi na utambulisho wa mkimbizi, jambo analotaka dunia ielewe vizuri zaidi.

Kwake, kuwa mkimbizi si mwisho wa safari ya maisha, bali ni hali inayoweza kubadilika na ambayo haifuti utu, ndoto au uwezo wa mtu.

Kundi la wanawake wakimbizi huko Kalobeyei, Kakuma, Kenya, wakionyesha vikapu vyao vilivyotengenezwa kwa mikono na vitu vilivyopambwa kwa shanga katika karakana ya ndani.
UN News Wanawake wakimbizi wanaofuma vikapu na kutunga shanga kwa ajili ya bishara ndondogo Kalobeyei, Kakuma, Turkana.

Kutoka maisha ya ukimbizi hadi kuwa sauti ya wakimbizi

Mary amekuwa akizungumza mara kwa mara kuhusu masuala ya wakimbizi, na uzoefu wake wa kuishi kambini kwa miaka 22, pamoja na kupata fursa ya elimu, ulimfanya achaguliwe kuwa Balozi Mwema wa UNHCR.

“Nimekuwa nikiongea sana na kujaribu kusukuma mambo ya wakimbizi. Kwanza, kwa sababu mimi mwenyewe nimeishi kwenye kambi kwa miaka hiyo yote. Halafu cha pili nilipata fursa ya kuja kusoma. Kwa hivyo najua ni changamoto gani,” anasema.

Sauti yake sasa inawakilisha zaidi ya simulizi yake binafsi. Ni sauti ya watoto wanaokua katika kambi, vijana wanaotafuta elimu, wazazi wanaotafuta usalama na familia zinazotamani siku moja kurejea nyumbani au kujenga maisha mapya kwa heshima na usalama.

Ujumbe kwa wakimbizi: “Sisi ndio viongozi wa kesho”

Kwa wakimbizi wanaokimbia vita na migogoro leo, Mary ana ujumbe mmoja kwao Msikate tamaa.

Anaamini kuwa elimu, urafiki na matumaini vinaweza kufungua milango ambayo mazingira ya sasa yanaonekana kuifunga.

“Siku moja Sudan Kusini itakuwa sawa. Siku moja DRC Congo itakuwa sawa na sisi ndio viongozi wa kesho. Kwa hivyo waendelee kuweka matumaini yao kwenye shule na marafiki,” anasema.

Ni ujumbe unaotokana na maisha yake mwenyewe, mtoto aliyekulia katika kambi, akasubiri fursa ya elimu, akakabiliana na vikwazo vya nyaraka, hatimaye akafika chuo kikuu nchini Marekani na sasa anatumia nafasi yake kuwa sauti ya wakimbizi duniani.

Kwa viongozi wa dunia: “Leo Sudan Kusini, kesho inaweza kuwa nchi yako”

Mary anapowaangalia viongozi wa dunia wanaokutana katika Umoja wa Mataifa kujadili migogoro, amani na mustakabali wa dunia, anataka wakumbuke jambo moja rahisi: hakuna nchi iliyo salama milele dhidi ya janga la kulazimika kukimbia.

Anaamini kwamba “Mtu yeyote anaweza kuwa mkimbizi. Leo nchi yako iko na amani, kesho inaweza kuwa nchi yako unakimbia,” anasema.

Na kwa nchi zinazowapokea wakimbizi, ujumbe wake ni wa ubinadamu na mshikamano, “Mkimbizi akija kwenye nchi yako, umkubali ukijua atakuja kwenye nchi yako. Ni jukumu letu kuweza kusaidia mtu yeyote aliye kwenye shida.”

Mary anabeba matumaini kwamba siku moja nchi yake ya Sudan Kusini itakuwa na amani na ustawi kiasi cha kuweza kuwapokea wengine wanaokimbia vita. Lakini hadi siku hiyo ifike, anaamini dunia ina wajibu wa kuwaona wakimbizi si kama mzigo, bali kama binadamu wenye ndoto, vipaji na mchango wa kutoa.

“Leo Sudan Kusini, kesho inaweza kuwa nchi yako.”