Uganda yatoa wito wa mageuzi ya Umoja wa Mataifa, uwakilishi zaidi kwa Afrika
Masuala ya UM
Uganda imetoa wito wa kufanyika kwa mageuzi ya kina katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, yakiwemo kuhakikisha Afrika inapata uwakilishi wa kudumu na usio wa kudumu, ili kulifanya Baraza hilo kuwa lenye usawa, uwazi, demokrasia na uwakilishi zaidi.
Akisoma hotuba ya Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni katika Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Makamu wa Rais Jessica Alupo amesema Uganda inaendelea kujitolea kwa misingi ya ushirikiano wa kimataifa na mfumo wa pande nyingi katika kukabiliana na changamoto za dunia.
Rais Museveni amesema dunia inakabiliwa na nyakati zisizo na uhakika, zikiambatana na tishio linaloendelea la migogoro ya kimataifa, akisisitiza umuhimu wa kurejea katika misingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kushirikiana kuzuia vita.
“Ni muhimu tushirikiane kuzuia vita,” Rais Museveni amesema.
Uganda yaunga mkono mageuzi ya Umoja wa Mataifa na ufadhili wa maendeleo
Uganda pia imeunga mkono mageuzi ya taasisi za fedha za kimataifa ili kuzipa nchi zinazoendelea sauti kubwa zaidi katika kufanya maamuzi, ikisema kuwa huduma ya madeni inaendelea kupunguza rasilimali zinazoweza kutumika katika miundombinu na huduma za kijamii.
Rais Museveni amesema ni asilimia 36 pekee ya malengo 139 ya Maendeleo Endelevu yanayoendelea kufikiwa kwa kasi inayohitajika, akitoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimataifa, mifumo ya haki ya kodi na hatua dhidi ya mtiririko haramu wa fedha.
Kuhusu mkakati wa maendeleo wa Uganda, amesema nchi hiyo inatekeleza Mpango wake wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2025/26–2029/30, unaolenga kuongeza kasi ya maendeleo katika sekta za kilimo na viwanda, utalii, madini, pamoja na sayansi, teknolojia na ubunifu.
Rais Museveni pia amezungumzia mchango wa Uganda katika juhudi za kuleta amani kikanda, kuimarisha mifumo ya afya na maandalizi ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa, akitoa wito wa kuongezwa kwa msaada wa kimataifa ili kuziba mapengo ya ufadhili na kuhakikisha upatikanaji sawa wa dawa, chanjo na zana za uchunguzi.
Uganda, ambayo kwa sasa ni Mwenyekiti wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM), pia imesisitiza kuunga mkono haki ya maendeleo na kutangaza kuwa itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa NAM mjini Kampala kuanzia tarehe 2 hadi 4 Desemba 2026.
Hii ni sehemu ndogo ya hotuba ya Rais Museveni iliyowasilishwa na Makamu wake. Kuona hotuba kamili bofya hapa.