Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ruto: Rasilimali za Afrika ziwe mwanzo wa viwanda, si mwisho wa mchango katika mnyororo wa thamani

Rais William Samoei Ruto wa Kenya akizungumza kwenye jukwaa lenye nembo ya UMOJA WA MATAIFA wakati wa kikao rasmi UN .
Picha ya UN/Loey Felipe Rais William Samoei Ruto wa Kenya akihutubia Mjadala Mkuu wa kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Ruto: Rasilimali za Afrika ziwe mwanzo wa viwanda, si mwisho wa mchango katika mnyororo wa thamani

Masuala ya UM

Rais wa Kenya William Ruto amesema rasilimali za Afrika lazima ziwe mwanzo wa maendeleo ya viwanda barani humo, badala ya kuwa mwisho wa mchango wa Afrika katika mnyororo wa thamani.

Akihutubia Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo, Rais Ruto amesema uchimbaji umeainisha kwa kiasi kikubwa historia ya Afrika, akisisitiza kuwa uwekezaji lazima uwe msingi wa mustakabali wa bara hilo.
 
“Rasilimali za Afrika lazima ziwe mwanzo wa maendeleo ya viwanda barani Afrika, na si mwisho wa mchango wa Afrika katika mnyororo wa thamani. Uchimbaji umeainisha kwa kiasi kikubwa historia yetu ya nyuma.
 
Uwekezaji lazima uwe msingi wa mustakabali wetu,” amesema.
 

Mabadiliko kuelekea uzalishaji zaidi Afrika

 
Rais Ruto amesema mabadiliko hayo tayari yanaanza kujitokeza, akitolea mfano nchi zinazozalisha kakao ambazo, kwa mujibu wake, zinabadilika kutoka kuuza punje hadi kujenga chapa zao, huku wazalishaji wa pamba wakijenga minyororo ya thamani ya nguo.
 
Amesema Afrika imeweka wazi msimamo wake kwamba mabadiliko kuelekea nishati safi hayapaswi kuwa mabadiliko mengine ya uchimbaji.
 
“Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika lazima liwe zaidi ya soko la bidhaa ambazo Afrika tayari inazalisha; lazima liwe jukwaa ambalo Afrika inazalisha zaidi ya bidhaa ambazo sasa inaziagiza,” amesema.
 

Kenya na kiwanda cha kusafisha mafuta Lamu

 
Rais Ruto amesema Kenya inakusudia kuwa sehemu ya mabadiliko hayo, akieleza kuwa ndani ya wiki moja nchi hiyo inatarajia kuweka jiwe la msingi la kiwanda cha kusafisha mafuta Afrika Mashariki huko Lamu.
Amesema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuchakata mapipa 700,000 ya mafuta kwa siku, kwa uwekezaji wa takribani dola bilioni 16.
 
Kwa mujibu wa Rais Ruto, umuhimu wa mradi huo unaenda zaidi ya mradi mmoja au nchi moja.
“Unawakilisha Afrika tunayotaka kuijenga: kuongeza thamani ndani ya nchi, kuunda ajira kwa watu wetu na kujenga viwanda vyenye uwezo wa kuhudumia masoko ya bara na dunia,” amesema.
 
Taarifa za hivi karibuni kuhusu maandalizi ya mradi huo zinaeleza kuwa Kenya inapanga kuweka jiwe la msingi la kiwanda hicho huko Lamu tarehe 30 Septemba.
 

Kutumia mitaji ya Afrika

 
Rais Ruto amesema mabadiliko hayo yanapaswa kugharamiwa kwa kutumia rasilimali za kigeni na za ndani, ikiwemo zaidi ya dola trilioni nne za mitaji ya ndani iliyopo katika mifuko ya pensheni, mali za bima, mifuko ya utajiri wa kitaifa, benki na taasisi nyingine barani Afrika.
 
Amesema jukumu ni kuhamasisha zaidi ya mtaji huo kuelekezwa kwenye uwekezaji wenye tija, huku kukijengwa mifumo ya ulinzi, miradi inayoaminika na nyenzo za kifedha ambazo wawekezaji wa muda mrefu wanahitaji.
 

“Afrika lazima iwe na sehemu katika uamuzi”

 
Rais Ruto amesema ukosefu wa usawa hauhusu fedha pekee, bali pia sauti ya Afrika katika taasisi zinazosimamia fedha duniani.
 
“Nchi 54 za Afrika zina takribani mtu mmoja kati ya kila watu watano duniani, lakini ushawishi wetu katika taasisi zinazosimamia fedha za dunia bado ni mdogo kwa kiasi kikubwa. Hatuwezi kubeba majukumu makubwa chini ya mfumo fulani huku tukibaki pembezoni katika kuunda kanuni zake. Ikiwa Afrika ina sehemu katika kubeba mzigo huo, Afrika lazima iwe na sehemu katika uamuzi,” amesema.
 
Amesema hilo si ombi la kutendewa kwa namna ya pekee, bali ni pendekezo la ustawi wa pamoja.
“Afrika yenye viwanda zaidi itaongeza mahitaji duniani. Afrika yenye usalama zaidi wa chakula itaongeza utulivu duniani. Afrika iliyounganishwa vizuri zaidi itafanya minyororo ya ugavi duniani kuwa yenye mseto zaidi. Na Afrika inayoweza kugharamia sehemu kubwa zaidi ya maendeleo yake yenyewe itakuwa mshirika mwenye nguvu zaidi kwa dunia,” amesema.
 
Hii ni sehemu ndogo tu ya hotuba nzima ya Rais William Ruto. Kutazama hotuba kamili bofya hapa.