Burundi yazungumzia ushiriki kamilifu wa vijana kwenye amani na maendeleo Afrika
Burundi yazungumzia ushiriki kamilifu wa vijana kwenye amani na maendeleo Afrika
- Vijana washiriki kwenye michakato ya amani
- Wao ni washirika wa leo kwa mustakabali wa kesho.
- Azungumzia pia haki za binadamu asema michakato ya kimataifa ina mrengo
Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye, amezungumzia umuhimu wa kuimarishwa kwa nafasi ya vijana katika ujenzi wa amani, maendeleo na mchakato wa maamuzi barani Afrika, akisema vijana hawapaswi kuonekana kama viongozi wa kesho pekee bali washiriki wa leo katika mustakabali wa bara hilo.
Sikiliza hotuba hapa kwa lugha ya kifaransa.
Akihutubia Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani Rais Ndayishimiye ambaye pia ni Mwenyekiti wa sasa wa Muungano wa Afrika, (AU), amesema kuwa kama kinara wa Ajenda ya Vijana, Amani na Usalama ya AU, Burundi imeendelea kusukuma mbele ushiriki wa vijana katika masuala ya usalama na maendeleo.
Majadiliano ya Bujumbura yathibitisha nguvu ya vijana
Rais huyo amesema Burundi iliandaa Toleo la Tano la Majadiliano ya Bara kuhusu Vijana, Amani na Usalama pamoja na Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama, yaliyofanyika Bujumbura nchini Burundi, mwezi Agosti mwaka huu.
“Mijadala hiyo ilidhihirisha hamasa kubwa ya vijana na wanawake katika kujenga Afrika yenye mshikamano, umoja na amani kwa kuzingatia falsafa ya Ubuntu,” amesema Rais Ndayimishiye.
Ameeleza kuwa vijana wa Afrika wameonesha nia ya kuishi pamoja, kushirikiana na kujenga jamii zenye maridhiano, lakini akatahadharisha kuwa “bado zipo baadhi ya nchi zinazochochea ubaguzi, chuki dhidi ya wageni na mgawanyiko miongoni mwa watu.”
AU yaomba vijana wapewe nafasi rasmi
Rais Ndayishimiye amesema, “hakuna amani ya kudumu Afrika bila ushiriki kamili, wenye tija na uliowekwa kisheria wa vijana katika kuzuia migogoro, usuluhishi, maridhiano na ujenzi wa amani,” na kwamba “Ajenda ya Vijana, Amani na Usalama ya Muungano wa Afrika inapaswa kupewa rasilimali za kutosha ili kufikia malengo yake.”
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukizungumza kuhusu vijana kama kizazi kitakachochukua nafasi baadaye. Lakini vijana wa Afrika siyo tu mustakabali wa bara letu, bali ni sehemu ya sasa ya maendeleo yake,” amesema.
Burundi yapinga utaratibu wa baraza la haki za binadamu
Katika hotuba yake, Rais Ndayishimiye pia ameikosoa namna Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu linavyoshughulikia baadhi ya nchi. “Taasisi hii lazima itende kwa misingi ya usawa na haki kwa mataifa yote.”
Burundi imesisitiza upinzani wake dhidi ya kuwepo kwa Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini humo, ikisema “uteuzi huo ulifanyika bila mazungumzo na makubaliano ya awali na serikali ya Burundi.”
Wito wa kuwekeza kwa vijana wa Afrika
Akihitimisha hotuba yake, Mwenyekiti huyo wa Muungano wa Afrika amezitaka nchi na washirika wa maendeleo kuwekeza zaidi katika elimu, ujuzi, ubunifu na uongozi wa vijana.
“Kuwapa vijana nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya kisiasa, amani na maendeleo kutasaidia kujenga Afrika yenye ustawi, utulivu na matumaini kwa vizazi vijavyo.”