Brazil: Lula ataka diplomasia, mageuzi ya Baraza la Usalama na hatua dhidi ya migogoro
Rais wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva, amesema uaminifu wa Umoja wa Mataifa unakabiliwa na changamoto kubwa ,akisistiza kuwa Umoja wa Mataifa unashindwa kutekeleza kikamilifu jukumu lake la msingi la kulinda ubinadamu dhidi ya vita.
Akihutubia Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Lula amesema nchi duniani zinaathiriwa na kushindwa kwa Baraza la Usalama kuchukua hatua madhubuti. “Sote tumeshikiliwa mateka na kutokuchukua hatua kwa Baraza la Usalama, ambalo limeshindwa kutekeleza jukumu lake,” amesema.
Diplomasia ndiyo njia pekee
Lula amesema mwaka 2025 ulikuwa na idadi kubwa zaidi ya migogoro ya kivita tangu Vita vya Pili vya Dunia, huku matrilioni ya dola yakielekezwa katika mashindano mapya ya silaha.
Amewataka viongozi wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama kukutana na kuchukua hatua dhidi ya vitisho vinavyozidi kuongezeka kwa amani na usalama wa kimataifa.
Akizungumzia vita vya Gaza na Ukraine, Lula ametaka suluhisho la kidiplomasia, akionya dhidi ya kuongezeka kwa mvutano.
Kuhusu Mashariki ya Kati, amesema, “Kutishia ustaarabu kwa kuangamizwa hakutaleta utulivu Mashariki ya Kati.”
Ameongeza kuwa huku Mlango wa Hormuz ukigeuka kuwa uwanja wa mapigano na vita kati ya Urusi na Ukraine vikiendelea, “Sote tunajua hakutakuwa na washindi kwenye uwanja wa vita. Diplomasia ndiyo njia pekee.”
Brazil si uwanja wa nyuma wa mtu yeyote
Akizungumzia Amerika ya Kusini na Karibea, Lula amesisitiza msimamo wa Brazil katika kipindi cha kuongezeka kwa mvutano wa kisiasa na kiusalama, pamoja na ukaribu wa kijiografia wa eneo hilo na taifa lenye nguvu kubwa zaidi kijeshi duniani. “Brazil haiwezi kuwa uwanja wa nyuma wa mtu yeyote,” amesema.
Pia ametoa wito wa ushirikiano mkubwa wa kimataifa katika kukabiliana na uhalifu wa kupangwa, hususan kwa kudhibiti mtiririko wa silaha na fedha unaochochea mitandao ya uhalifu.
Lula amesema amewasilisha binafsi pendekezo hilo kwa Rais wa Marekani.
Hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
Lula pia ameangazia hatari zinazoongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi, zikiwemo mvua kubwa, ukame na moto wanyika unaoweza kuchochewa na hali kali ya El Niño.
Ameahidi kuendelea na juhudi za kupunguza ukataji miti nchini Brazil, akisema ukataji miti katika msitu wa Amazon umepungua kwa nusu na kufikia kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miaka 11.