DRC yazindua utafiti wa chanjo ya Ebola kwa wahudumu wa afya Ituri
DRC yazindua utafiti wa chanjo ya Ebola kwa wahudumu wa afya Ituri
Mpango wa utafiti wa chanjo ya Ebola umeanzishwa katika jimbo la Ituri, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ukiwalenga wahudumu wa afya na wafanyakazi wengine walio mstari wa mbele ambao wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi vya Ebola.
Kupitia ukurasa wake wa X, zamani Twitter, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO, Kanda ya Afrika imesema, katika mpango huo, takribani dozi 20,000 za chanjo ya ERVEBO dhidi ya Ebola, zinatarajiwa kutumika kama sehemu ya utafiti unaojulikana kama BRAVO.
Utafiti huo unaongozwa na Wizara ya Afya ya DRC, chini ya usimamizi wa kisayansi wa Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Dawa, (INRB), huku Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) likihusika katika utekelezaji.
WHO, Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika, (Africa CDC) pamoja na washirika wengine wanaunga mkono mpango huo.
Lengo la utafiti ni nini?
Lengo kuu la utafiti ni kuongeza uelewa wa matumizi ya chanjo katika kukabiliana na virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo, iliyokumba taifa hilo la Maziwa Makuu tangu mwezi Mei mwaka huu, huku wakati huo huo ukilenga kuwakinga watu walio katika hatari kubwa ya kuathiriwa na ugonjwa huo.
Mlipuko wa Ebola ya Bundibugyo nchini DRC ulithibitishwa mwezi Mei 2026 katika jimbo la Ituri. WHO imesema mlipuko huo unahusisha aina ya virusi vya Bundibugyo, na kwamba hakuna chanjo iliyoidhinishwa au tiba maalumu iliyopo kwa sasa dhidi ya aina hiyo ya virusi.
WHO inasema wahudumu wa afya ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa wakati wa milipuko ya Ebola kutokana na mawasiliano yao ya karibu na wagonjwa.
Hadi sasa, WHO imeripoti kwamba wahudumu wanne wa afya waliokuwa wameambukizwa Ebola ya Bundibugyo katika mlipuko huu walipona na kuruhusiwa kutoka hospitalini mjini Bunia mwezi Mei.
Matarajio ya mpango wa sasa
Kwa ujumla, dozi 70,000 za ERVEBO zimewekwa katika mpango wa msaada kwa DRC, kwa ajili ya kusaidia mwitikio dhidi ya mlipuko pamoja na shughuli za utafiti zinazohusiana na ugonjwa huo.
Mpango wa BRAVO unatarajiwa kutoa ushahidi zaidi wa kisayansi kuhusu matumizi ya chanjo hiyo katika mazingira ya mlipuko wa virusi vya Bundibugyo.
Kwa mujibu wa WHO, matokeo yake yanaweza kusaidia wataalamu wa afya kuelewa zaidi namna ya kutumia chanjo katika kuwalinda watu walio katika hatari kubwa wakati wa milipuko ya baadaye.
WHO inaendelea kusaidia DRC katika maeneo mbalimbali ya mwitikio wa mlipuko huo, yakiwemo ufuatiliaji wa magonjwa, uchunguzi wa maabara, huduma za wagonjwa na udhibiti wa maambukizi.