Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mioto ya nyika na mawimbi ya joto vyatishia mafanikio ya dunia ya kuboresha ubora wa hewa- WMO

Moto wa misitu unawaka kwenye kilima nyuma ya mji kwenye kisiwa cha Corfu, Ugiriki, wakati wa machweo.
UN News/Katy Dartford Moto wa msituni huko kaskazini mashariki mwa kisiwa cha Corfu, Ugiriki, unaweza kuonekana wazi kutoka mji wa Corfu

Mioto ya nyika na mawimbi ya joto vyatishia mafanikio ya dunia ya kuboresha ubora wa hewa- WMO

Tabianchi na mazingira
  • Hewa inavyokuwa chafu, afya ya binadamu hatarini
  • Chembechembe ndogo za uchafuzi wa hewa (PM 2.50 zinaingia kwenye mapafu na mfumo wa damu
  • China ina unafuu
Kuongezeka kwa uchafuzi wa hewa unaosababishwa na mioto ya nyika na mawimbi ya joto kali vinatishia juhudi za kimataifa za kuboresha ubora wa hewa na kulinda afya ya binadamu na mazingira, imesema Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Hewa, WMO, iliyotolewa leo huko Geneva ,Uswisi.
Ikipatiwa jina Chapisho la Ubora wa Hewa na Tabianchi, ripoti hiyo ya kurasa 12, imetolewa leo ambayo ni siku ya kimataifa ya Hewa Safi kwa Anga la Bluu, ambapo inasisitiza uhusiano wa karibu kati ya mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa hewa.
 
Tweet URL
Inaonya kwamba changamoto hizi mbili zinapaswa kushughulikiwa kwa pamoja kupitia sera zilizoratibiwa na ufuatiliaji madhubuti wa mazingira.

Matokeo muhimu

Mioto ya nyika husababisha uchafuzi hatari wa chembechembe
  • Chembechembe ndogo za uchafuzi wa hewa (PM2.5), ambazo zinaweza kupenya ndani kabisa ya mapafu na kuingia kwenye mfumo wa damu, zilibaki juu ya wastani wa muda mrefu katika maeneo kadhaa mwaka 2025.

    Maeneo yaliyoathirika yalijumuisha: Kaskazini mwa Canada, Maeneo ya Urusi, Afrika Magharibi na Kati, ambako kuongezeka kwa shughuli za mioto ya nyika kulichangia viwango vya juu vya uchafuzi, Kaskazini-magharibi mwa Hispania, ambako kulishuhudiwa moto wa misitu usio wa kawaida mwishoni mwa majira ya joto

  • China ina unafuu: Kinyume chake, viwango vya PM2.5 katika anga la juu la hewa nchini China viliendelea kupungua kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa uchafuzi unaosababishwa na shughuli za binadamu.
  • India iliendelea kuwa na viwango vilivyo juu ya wastani kutokana na uchomaji wa mabaki ya mimea na vyanzo vingine vya uchafuzi.
Moshi wa mioto ya nyika unaongeza hatari za kiafya
  • WMO inasema matukio makali ya mioto ya nyika yanazidi kuwa ya mara kwa mara na yanasababisha madhara makubwa kiafya.
  • Utafiti uliotajwa katika ripoti hiyo ulibaini kuwa matukio makali ya moshi yameongezeka mara tatu duniani kote tangu miaka ya 1990.
  • Uchafuzi wa hewa unaohusiana na mioto hiyo huenda ulichangia karibu vifo vya ziada 100,000 kila mwaka kati ya 2010 na 2018.
  • Watafiti wanaonya kwamba tathmini za sasa za hatari za kiafya huenda zikawa zinapunguza makadirio ya sumu ya moshi wa moto wa misitu na athari zake katika vifo.
Mawimbi ya joto yanazidisha uchafuzi wa tabaka la ozoni
  • Uchafuzi wa ozoni katika tabaka la chini la anga, ambao hudhuru afya ya binadamu, mazao na mifumo ikolojia, unazidi kuwa mbaya wakati wa mawimbi ya joto.
  • Joto la juu, hewa isiyosogea na mwanga mkali zaidi wa jua huunda mazingira yanayoongeza uundaji wa ozoni.
  • Tafiti za hivi karibuni nchini Marekani, Ulaya na China zinaonesha kuwa mawimbi ya joto yanaongeza kwa kiasi kikubwa viwango vya kukabiliwa na ozoni.
  • WMO inaonya kwamba hatari za kiafya zinazohusiana na ozoni zinatarajiwa kuongezeka siku zijazo.
Mtazamo wa angani wa anga ya London wakati wa machweo huku Mto Thames ukipita katikati ya jiji.
© Adobe Stock/Moofushi Jiji la London nchini Uingereza linazidi kuwa na joto kali katika wimbi lake la tano la joto la msimu wa joto uliovunja rekodi.

Umuhimu wa kufuatilia kwa ubora zaidi

Shirika hilo limeitaka dunia kupanua mitandao ya ufuatiliaji ili kufuatilia mambo kadhaa zikiwemo chembechembe ndogo za uchafuzi wa hewa (PM2.5) na chembechembe ndogo za plastiki.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vichafuzi hivi vingi vimeenea katika maeneo mbalimbali lakini bado havifuatiliwi kwa kiwango cha kutosha.

Afrika ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika

Taarifa hiyo imetaja Afrika Magharibi na Kati kuwa miongoni mwa maeneo ambayo viwango vya PM2.5 vilikuwa juu ya wastani wa muda mrefu mwaka 2025, hasa kutokana na kuongezeka kwa shughuli za moto wa misitu.
Matokeo hayo yanaonesha changamoto zinazoongezeka za ubora wa hewa zinazokabili baadhi ya maeneo ya Afrika huku hatari ya moto inayochochewa na mabadiliko ya tabianchi ikiongezeka.

Ujumbe wa WMO

WMO imeonya kwamba kufikia miongozo ya ubora wa hewa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) kutazidi kuwa vigumu kadiri mabadiliko ya tabianchi yanavyochochea hali mbaya zaidi za hewa zinazohusiana na moto na mawimbi ya joto.
 
Shirika hilo limetaka kuwepo kwa mikakati jumuishi ya kushughulikia tabianchi na ubora wa hewa, likisema kwamba masuala haya mawili hayawezi kutenganishwa na yanahitaji hatua zilizoratibiwa ili kulinda afya ya umma na mifumo ikolojia.