Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Annalena Baerbock auaga Urais wa Baraza Kuu la UN akiwa mwenye matumaini ya kimfumo

Annalena Baerbock, Rais wa kikao cha 80 cha Baraza Kuu UN , akizungumza kwenye kipaza sauti huku bendera UN ikiwa nyuma.
Picha ya UN/Mark Garten Annalena Baerbock, Rais wa kikao cha 80 cha Baraza Kuu la UN , akiwafahamisha waandishi wa habari kuhusu kufungwa kwa kikao hicho.

Annalena Baerbock auaga Urais wa Baraza Kuu la UN akiwa mwenye matumaini ya kimfumo

Masuala ya UM

Baada ya mwaka mmoja wa kuongoza Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, leo Alhamisi ametetea rekodi ya taasisi hiyo iliyokumbwa na vita na migawanyiko, akisema licha ya changamoto hizo, imeweza kukwepa baadhi ya vikwazo na kuanza mchakato wa mageuzi.

Alipochukua uongozi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo Septemba 2025, Annalena Baerbock alichagua kaulimbiu “Bora Tukiwa Pamoja”
Mwaka mmoja baadaye, huku vita vikiongezeka na Baraza la Usalama likibaki na mkwamo katika kushughulikia migogoro kadhaa mikubwa, kaulimbiu hiyo inaweza kuonekana kama kejeli.
Hata hivyo, leo katika mkutano wake wa mwisho na waandishi wa habari jijini New York, Waziri huyo wa zamani wa Ujerumani ameendelea kuonesha matumaini thabiti ambayo yalitawala kipindi chake cha uongozi.
“Unapaswa kuwa mwenye matumaini ya kimfumo unapofanya kazi katika diplomasia, la sivyo ungekuwa bora kuchagua taaluma nyingine,” amesema Baerbock, akiondoka katika nafasi hiyo. Hata hivyo, ameongeza kuwa “Haimaanishi kwamba wewe si mhalisia.”
Katika hali hii, uhalisia unamaanisha kwanza kukubali hali ya shirika hilo linaloadhimisha miaka 80, huku likikabiliwa na migogoro, kupunguzwa kwa bajeti na changamoto zinazoongezeka dhidi ya mfumo wa ushirikiano wa kimataifa.
“Nyumba hii haiko katika hali nzuri,” amekiri Baerbock, akisema Umoja wa Mataifa hauwezi kuendelea kuishi katika mazingira ya sasa ya migawanyiko bila kuwa na urasimu mdogo, ufanisi zaidi na uwezo wa kuchukua hatua kwa haraka.
Annalena Baerbock akizungumza kwenye jukwaa katika chumba cha Baraza la Usalama UN , huku nembo UN ikionekana ukutani na picha yake ikionyeshwa kwenye skrini kubwa.
Picha ya UN/Eskinder Debebe Rais wa Baraza Kuu Annalena Baerbock (kwenye skrini) akihutubia Siku ya Kimataifa ya Kutafakari na Kukumbuka Mauaji ya Kimbari ya 1995 huko Srebrenica.

Kupiga kura badala ya kusubiri muafaka

Baerbock alichaguliwa mwezi Juni 2025 kwa kura 167 kati ya nchi wanachama 193, licha ya Urusi kutaka uchaguzi huo ufanyike kwa kura ya siri.
Alifika New York akiwa na historia ya kisiasa iliyopanda kwa kasi na yenye matukio mengi. Akiwa mmoja wa viongozi wa chama cha Greens nchini Ujerumani na mgombea wa chama hicho wa nafasi ya Kansela mwaka 2021, miezi michache baadaye akawa mwanamke wa kwanza kuongoza Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani katika serikali ya Olaf Scholz.
Akiwa katika nafasi hiyo, alitetea msimamo mkali dhidi ya Urusi na uungaji mkono mkubwa kwa Ukraine.
Akiwa na umri wa miaka 45, Baerbock, ambaye alikuwa mbunge wa bunge la Ujerumani Bundestag kuanzia mwaka 2013 hadi 2025, aliahidi kulipa Baraza Kuu uzito zaidi. Baraza hilo ni jukwaa ambalo kila moja ya nchi 193 wanachama ina kura moja, wakati Baraza la Usalama lilikuwa likikwamishwa mara kwa mara na kura za turufu za wanachama wake wa kudumu.
Sehemu ya rekodi yake ya uongozi imejengwa juu ya ahadi hiyo.
Baerbock amesema ametoa kipaumbele kwa upigaji kura pale ambapo jitihada za kufikia muafaka zilipotishia kusababisha mkwamo.
Anataja, miongoni mwa mifano, Tamko la New York kuhusu Gaza, lililopitishwa na zaidi ya nchi 140, pamoja na kuundwa kwa jopo la kwanza huru la kimataifa la kisayansi kuhusu akili Mnemba.
Katika matukio kadhaa, amesema, ni nchi chache tu zilizopinga hatimaye maandiko yaliyowasilishwa kwa kura. Kwa maoni yake, hilo ni uthibitisho kwamba nyuma ya taswira ya Umoja wa Mataifa uliogawanyika, “nchi wanachama zilikuwa zimeungana zaidi kuliko zilivyogawanyika.”
Kutokana na mkwamo wa Baraza la Usalama katika baadhi ya masuala, Baraza Kuu pia lilijaribu kuziba pengo hilo.
Baerbock aliitisha mijadala kufuatia kura za turufu kuhusu Gaza na Mlango Bahari wa Hormuz. Kuhusu Ukraine, alisisitiza tena kanuni ya uhuru wa maeneo ya nchi kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Hii ilikuwa njia ya kutambua mipaka ya taasisi hiyo, huku akikataa kuruhusu mipaka hiyo kuwa kisingizio cha kutokuchukua hatua.
Annalena Baerbock, Rais wa Baraza Kuu, amesimama na wanawake wawili katika mtaa wa makazi huko Doha, Qata, wanaposhiriki mlo. Mwanamke mmoja yuko kwenye kiti cha magurudumu.
UN News/Vibhu Mishra Rais wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Annalena Baerbock akizungumza na mwanamke mwenye kwenye makaziya Al -Thumana huko Doha, Qatar yanayojhifadhi wakimbizi wa kipalestina walioondolewa Gaza ili kupatiwa matibabu eneo hili.

Umoja wa Mataifa unaohitaji kurahisishwa

Kazi nyingine imekuwa ngumu zaidi: mageuzi ya ndani ya Umoja wa Mataifa.
Mpango wa UN 80, ulioanzishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, unalenga kupunguza kurudiwa kwa majukumu, kupitia upya maelfu ya mamlaka yaliyokusanywa kwa miongo kadhaa, na kurekebisha shirika ambalo miundo yake bado inaakisi zama zilizopita.
Baerbock ametoa wito, miongoni mwa mambo mengine, kwa kupitishwa kwa bajeti iliyopunguzwa, mabadiliko ya kanuni za kifedha, kurahisishwa kwa baadhi ya mamlaka na kupunguzwa kwa mikutano ya ngazi za juu.
Pia ametaja hatua kama kupunguza muda wa hotuba na kuzimwa kiotomatiki kwa vipaza sauti baada ya muda uliowekwa. Hii ni hatua yenye utata katika taasisi ambayo kutoa maoni na kujieleza ni sehemu muhimu ya kazi yake, lakini Baerbock anaiona kama mapinduzi madogo yanayolenga kuhakikisha kila nchi inapata nafasi ya kusikilizwa kwa kina.
Hata hivyo, Waziri huyo wa zamani anakiri kuwa bado kuna mengi ya kufanywa.
Amesema alishtuka kugundua kwamba Umoja wa Mataifa hauna hata mchoro kamili wa muundo wake wa kiutawala unaoweza kuonesha maeneo ambayo majukumu yanaingiliana kati ya miundo yake mingi.
Alihoji, “Je, kweli tunahitaji zaidi ya wasaodizi 200 wa Katibu Mkuu na manaibu Wasaidizi wa Katibu Mkuu, au tunapaswa kuendelea na mifumo iliyoundwa katika miaka ya 1970 bila kutathmini upya umuhimu wake?”
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na Annalena Baerbock wamepiga picha pamoja na Khalilur Rahman katika Umoja wa Mataifa.
Picha ya UN/Eskinder Debebe Katibu Mkuu António Guterres (kushoto) na Rais wa Baraza Kuu Annalena Baerbock (kulia), pamoja na Khalilur Rahman, Rais mteule wa kikao cha 81 cha Baraza Kuu.

Mustakabali wa uongozi wa Umoja wa Mataifa

Suala moja la mwisho liko karibu zaidi na moyo wa Baerbockni  mchakato wa kumrithi António Guterres kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Baerbock aliandaa midahalo minane shirikishi na wagombea wa nafasi hiyo, akilenga kufanya mchakato huo kuwa wa uwazi zaidi.
Pia alirejesha kwenye mjadala swali ambalo Umoja wa Mataifa umeliepuka tangu kuanzishwa kwake, baada ya wanaume tisa kuongoza taasisi hiyo, je, hatimaye Umoja wa Mataifa utamchagua mwanamke?
Kwa maoni yake, kushindwa hata kulifikiria suala hilo kwa uzito baada ya miaka 80 kungeibua swali kuhusu “uaminifu wa taasisi inayodai kutetea usawa”.
Jumanne, Septemba 8, Waziri wa Mambo ya Nje wa Bangladesh, Khalilur Rahman, atamrithi Baerbock katika kikao cha 81 cha Baraza Kuu.
Rahman alichaguliwa mwezi Juni kwa kura 99 dhidi ya 91 za mgombea kutoka Cyprus.
Atarithi Umoja wa Mataifa ambao bado unakabiliwa na changamoto za kifedha pamoja na hitaji la mageuzi.
Kwa maneno mengine, Annalena Baerbock ametumia mwaka mmoja kuutetea Umoja wa Mataifa, huku akisisitiza mara kwa mara kwamba taasisi hiyo haiwezi kuendelea kuwepo kwa namna ilivyo sasa.